Add parallel Print Page Options

Yesu Afundisha Kuhusu Kutoa

Mnapofanya jambo jema, kuweni waangalifu msilifanye mbele za watu wengine ili wawaone. Mtakapofanya hivyo hamtapata thawabu kutoka kwa Baba yenu wa mbinguni.

Unapowapa maskini na wahitaji, usilipigie mbiu sana jambo hilo. Maana hivyo ndivyo wanavyofanya wanafiki kwenye makusanyiko.[a] Wao hupiga mbiu kabla ya kutoa ili watu wawaone, kwa kuwa hutaka kila mtu awasifu. Ukweli ni kuwa, hiyo ndiyo thawabu yote waliyokwishapata. Hivyo unapowapa maskini, mtu yeyote asijue unachofanya.[b] Kutoa kwako kunapaswa kufanyika sirini kwa kuwa Baba yako huona mambo yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.

Yesu Afundisha Kuhusu Maombi

(Lk 11:2-4)

Mnapoomba, msiwe kama wanafiki. Wanapenda kusimama kwenye masinagogi na kwenye pembe za mitaa na kuomba kwa kupaza sauti. Wanapenda kuonwa na watu. Ukweli ni kuwa hiyo ndiyo thawabu yote watakayopata. Lakini unapoomba, unapaswa kuingia katika chumba chako cha ndani na ufunge mlango. Kisha mwombe Baba yako aliye mahali pa siri. Yeye anayaona mambo yanayofanyika katika siri na hivyo atakupa thawabu.

Na unapoomba usiwe kama watu wasiomjua Mungu. Wao kila wanapoomba wanarudia maneno yale yale, tena na tena, wakidhani kuwa wanapoyarudia maneno hayo mara nyingi watasikiwa na Mungu na kujibiwa maombi yao. Msiwe kama wao. Baba yenu anajua yale mnayohitaji kabla hamjamwomba. Hivyo, hivi ndivyo mnapaswa kuomba:

‘Baba yetu uliye mbinguni,
    Jina lako lipewe utukufu.
10 Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike hapa dunia,
    kama yanavyofanyika huko mbinguni.
11 Utupe leo chakula tunachohitaji.
12 Utusamehe dhambi zetu,
    kama tunavyowasamehe wale wanaotukosea.
13 Usiruhusu tukajaribiwa,
    lakini utuokoe na Yule Mwovu.’[c]

14 Mkiwasemehe wengine makosa waliyowatendea, Baba yenu wa mbinguni naye atawasamehe makosa yenu pia. 15 Lakini msipowasamehe wengine, Baba Yenu wa mbinguni hatawasamehe ninyi.

Yesu Afundisha Kuhusu Kufunga

16 Mnapofunga, msijionyeshe kuwa na huzuni kama wanafiki wanavyofanya. Hukunja nyuso zao kwa kuonesha kuwa wana huzuni ili watu wawaone kuwa wamefunga. Ukweli ni kuwa wamekwishapata thawabu yao yote. 17 Hivyo unapofunga, nawa uso wako na ujiweke katika mwonekano mzuri, 18 ili watu wasijue kuwa umefunga, isipokuwa Baba yako, aliye nawe hata sirini. Anaweza kuona yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.

Huwezi Kuwatumikia Mabwana Wawili

(Lk 12:33-34; 11:34-36; 16:13)

19 Msijiwekee hazina hapa duniani, mahali nondo na kutu[d] huiharibu. Na wezi wanaweza kuvunja nyumba yako na kuziiba. 20 Badala yake jiwekeeni hazina mbinguni ambako haziwezi kuharibiwa na nondo wala kutu na ambako wezi hawawezi kuvunja na kuziiba. 21 Kwa kuwa roho yako itakuwa mahali ilipo hazina yako.

22 Jinsi unavyowaangalia watu wengine ndivyo inavyoonyesha jinsi wewe mwenyewe ulivyo ndani yako. Ukiwaangalia watu kwa nia njema utajawa na nuru ndani yako. 23 Lakini ukiwaangalia watu kwa nia mbaya, utajawa na giza ndani yako. Na ikiwa yote yanayoonekana ndani yako ni giza peke yake, basi unalo giza baya zaidi![e]

24 Hamwezi kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Mtamchukia mmoja na kumpenda yule mwingine au mtakuwa waaminifu kwa mmoja na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na pesa.[f]

Utangulizeni Kwanza Ufalme wa Mungu

(Lk 12:22-34)

25 Kwa hiyo ninawaambia, msiyahangaikie mahitaji ya mwili; mtakula nini, mtakunywa nini au mtavaa nini. Uhai ni zaidi ya chakula na mavazi. 26 Waangalieni ndege wa angani. Hawapandi, hawavuni wala kutunza chakula ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, hamjui kuwa ninyi mna thamani zaidi ya ndege? 27 Hamwezi kujiongezea muda wa kuishi kwa kujisumbua.

28 Na kwa nini mna wasiwasi kuhusu mavazi? Yaangalieni maua ya kondeni. Yatazameni namna yanavyomea. Hayafanyi kazi wala kujitengenezea mavazi. 29 Lakini ninawaambia kuwa hata Suleimani, mfalme mkuu na tajiri, hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya maua haya. 30 Ikiwa Mungu anayafanya majani yanayoota mashambani kuwa mazuri mnafikiri atawafanyia ninyi kitu gani? Hayo ni majani tu, siku moja yako hai na siku inayofuata hutupwa katika moto. Lakini Mungu anajali kiasi cha kuyafanya kuwa mazuri ya kupendeza. Muwe na hakika basi atawapa ninyi mavazi mnayohitaji. Imani yenu ni ndogo sana!

31 Msijisumbue na kusema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Haya ndiyo mambo ambayo watu wasiomjua Mungu huyawazia daima. Msiwe na wasiwasi, kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua kuwa mnayahitaji haya yote. 33 Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na mambo yote ambayo Mungu anahesabu kuwa ni mema na yenye haki. Ndipo Mungu atakapowapa yote mnayohitaji. 34 Msiisumbukie kesho. Kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Kila siku ina mahangaiko yake ya kutosha.

Footnotes

  1. 6:2 makusanyiko Au “masinagogi”.
  2. 6:3 asijue unachofanya Kwa maana ya kawaida, “Mkono wako wa kushoto usijue kile ambacho mkono wako wa kushoto unafanya.”
  3. 6:13 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza: “Kwa kuwa ufalme na nguvu na utukufu ni vyako milele na milele. Amina.”
  4. 6:19 nondo na kutu Pia katika mstari wa 20.
  5. 6:22-23 Kwa maana ya kawaida, 22 Taa ya mwili ni jicho. Hivyo, jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru tele. 23 Lakini jicho lako likiwa na uovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Hivyo ikiwa nuru ndani yako ni giza, giza hilo ni linatisha.
  6. 6:24 pesa Au “mamona”, neno la Kiaramu linalomaanisha “utajiri”.