Add parallel Print Page Options

Yesu Aomba Akiwa Peke Yake

(Mk 14:32-42; Lk 22:39-46)

36 Kisha Yesu akaondoka pamoja na wafuasi wake na kwenda mahali panapoitwa Gethsemane. Akawaambia, “Kaeni hapa wakati ninakwenda mahali pale kuomba.” 37 Alimwambia Petro na wana wawili wa Zebedayo waende pamoja naye. Kisha akaanza kuhuzunika na kuhangaika. 38 Yesu akamwambia Petro na wana wa Zebedayo, “Moyo wangu ni mzito na wenye huzuni hata kujisikia kana kwamba huzuni hiyo itaniua. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.”

39 Kisha Yesu akaenda mbele kidogo. Akainama hadi chini uso wake ukiigusa nchi akiomba na akasema, “Baba yangu, ikiwezekana, usifanye nikinywee kikombe hiki cha mateso.[a] Lakini fanya lile ulitakalo na si lile ninalolitaka mimi.” 40 Kisha akarudi walipokuwa wafuasi wake na akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Je hamkuwa na uwezo wa kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? 41 Amkeni kesheni na kuomba ili muyashinde majaribu. Roho zenu zinataka kufanya mambo sahihi, lakini miili yenu ni dhaifu.”

42 Kisha Yesu akaenda mara ya pili na akaomba akisema, “Baba yangu, ikiwa ni lazima nikinywee kikombe hiki na haiwezekani nikakwepa, basi mapenzi yako na yatimizwe.”

43 Kisha akarudi na kwenda walipokuwa wafuasi wake, akawakuta wamelala tena. Hawakuweza kukesha. 44 Hivyo akawaacha akaenda tena kuomba. Mara hii ya tatu alipokuwa anaomba akasema kama alivyosema hapo mwanzo.

45 Kisha Yesu akawarudia wafuasi wake na akasema, “Bado mnalala na kupumzika? Wakati wa Mwana wa Adamu kukabidhiwa kwa wenye dhambi umewadia. 46 Simameni! Tuondoke. Tazama yeye atakayenikabidhi anakuja.”

Read full chapter

Footnotes

  1. 26:39 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao.