Add parallel Print Page Options

Kufuata Mafundisho ya Kweli

Lakini wewe Tito daima uwaambie waaminio mambo yanayokubaliana na mafundisho ya kweli na yenye uzima. Wanaume wazee wanapaswa kuwa na kiasi na kufanya mambo yenye kuleta heshima. Wanapaswa kuwa na busara katika maisha yao. Kuwa na nguvu katika imani kwa Mungu, upendo kwa wengine, na uvumilivu.

Vivyo hivyo wafundishe wanawake wazee wawe na mwenendo mzuri. Wafundishe wasiwe wachochezi na wasiwe watumwa wa mvinyo. Wanapaswa kufundisha yale yaliyo mema. Kwa jinsi hiyo wataweza kuwakumbusha wanawake vijana jinsi wanavyopaswa kuishi. Wanawake vijana wanapaswa kuwaonesha upendo waume zao na kuwapenda watoto wao. Wanapaswa kuwa na busara na wasafi kiroho, wakizitunza nyumba zao, kuwa wakarimu, na kuwa tayari kuwatumikia waume zao wenyewe, ili asiwepo atakayeudharau ujumbe wa Neno la Mungu.

Kadhalika endelea kuwahimiza wanaume vijana kuwa na busara. Katika kila kitu ujioneshe kuwa wewe ni mfano wa matendo mema. Katika mafundisho yako onesha kuwa una moyo safi na uko makini. Ufundishe kile ambacho ni sahihi kwa wazi, ili asiwepo yeyote atakayepinga mafundisho yako. Tumia mazuri ambayo hayatasemwa vibaya ili wale wanaokupinga waaibishwe kwa ajili ya kukosa lo lote baya la kusema dhidi yetu.

Wafundishe watumwa kuwatii bwana zao katika kila jambo, wajitahidi kuwapendeza na sio kubishana nao 10 wala kwa siri wasiwaibie bali waudhihirishe uaminifu kamili, ili katika mambo yote wayapatie sifa njema mafundisho kutoka kwa Mungu, Mwokozi wetu.

11 Maana Mungu ameidhihirisha neema yake inayookoa kwa watu wote. 12 Hiyo inatufundisha kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia ili tuishi katika ulimwengu wa sasa kwa njia ya werevu, haki na kuionesha heshima yetu kwa Mungu, 13 kadri tunavyosubiri ile Siku iliyobarikiwa tunayoitumaini ambapo utukufu wa Mungu wetu mkuu na Mwokozi Yesu Kristo itakapofunuliwa. 14 Alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili aweze kutuweka huru sisi kutoka katika uovu wote na kuweza kutusafisha kwa ajili yake watu walio wake mwenyewe, wale walio na shauku ya kufanya matendo mema.

15 Endelea kufundisha ukihimiza na kukemea kuhusu mambo haya, na fanya hivyo kwa mamlaka yote, na mtu yeyote asikudharau.