Mashahidi Wawili

11 Ndipo nikapewa kipimo kama fimbo, nikaambiwa, “Nenda kapime Hekalu la Mungu pamoja na madhabahu na uwahesabu watu waabuduo humo. Lakini usipime uwanja wa nje ya Hekalu, uache, kwa sababu uwanja huo wamepewa mataifa wasiomjua Mungu. Wao wataukanyagakanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili. Nami nitawapa uwezo mashahidi wangu wawili watoe unabii kwa muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini na mbili, wakiwa wamevaa magunia.”

Manabii hao wawili ni ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana na mbele ya nchi yote. Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka vinywani mwao na kuwateketeza adui zao. Na hivyo ndivyo atakavyokufa mtu ye yote atakayetaka kuwad huru. Watu hawa wanayo mamlaka ya kuyafunga mawingu ili mvua isinyeshe wakati wote watakapokuwa wanatoa unabii wao. Watakuwa na mamlaka juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuleta maafa ya kila aina ulimwenguni, kama wapendavyo. Lakini wakishamaliza kutoa unabii huo, yule mnyama atokaye katika shimo la kuzimu ata wapiga vita na kuwashinda na kuwaua. Maiti zao zitabaki katika barabara ya mji mkuu ambao kwa fumbo unaitwa Sodoma na Misri, ambapo Bwana wao alisulubiwa. Kwa muda wa siku tatu na nusu, watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti zao, na hawataruhusu wazikwe. 10 Watu waishio duniani watafura hia kifo cha manabii hao wawili na kushangilia kwa kupeana zawadi kwa sababu manabii hao waliwatesa watu waishio ulimwenguni.

11 Lakini baada ya zile siku tatu na nusu, pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu. 12 Kisha wale manabii wawili wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njooni huku juu!” Nao wakapaa mbinguni katika wingu, wakati maadui zao wakiwatazama. 13 Wakati huo huo, kukatokea tetemeko kuu la nchi, na sehemu moja ya kumi ya mji ikaanguka. Watu elfu saba wakauawa katika tetemeko hilo na waliosalimika wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.

14 Maafa ya pili yamekwisha kupita. Lakini maafa ya tatu yanakuja upesi.

Tarumbeta Ya Saba

15 Kisha malaika wa saba akapiga tarumbeta yake. Na sauti kuu zikasikika mbinguni zikisema, “Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na Kristo wake, naye atatawala milele na milele.” 16 Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vyao vya enzi wakaanguka kifudifudi wakamwabudu Mungu, 17 wakisema, “Tunakushukuru, Bwana Mungu Mwenyezi uli yeko na uliyekuwako; kwa kuwa umeuchukua uweza wako mkuu na ukaanza kutawala. 18 Watu wa mataifa walikasirika kwa kuwa wakati wa ghadhabu yako umefika. Wakati umefika wa kuwahukumu wafu na kuwapa tuzo watumishi wako manabii na watakatifu walioli tukuza jina lako, wakubwa kwa wadogo; na wakati umefika wa kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.”

19 Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa na sanduku la agano lake likaonekana Hekaluni mwake. Kukatokea umeme, sauti, ngurumo na tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.

Mashahidi Wawili

11 Kisha nilipewa fimbo ya kupimia, ndefu kama fimbo ya kutembelea. Nikaambiwa, “Nenda ukalipime hekalu[a] la Mungu na madhabahu na uwahesabu watu wanaoabudu humo. Lakini usipime eneo lililo nje ya hekalu. Liache. Eneo hilo wamepewa watu wasio wa Mungu. Wataonesha nguvu zao juu ya mji mtakatifu kwa miezi 42. Nami nitawapa nguvu mashahidi wangu wawili, watatabiri kwa siku 1,260. Nao watakuwa wamevaa magunia.”

Mashahidi hawa wawili ni mizeituni miwili na vinara viwili vya taa vinavyosimama mbele za Bwana wa dunia. Ikiwa mtu yeyote atajaribu kuwadhuru mashahidi hawa, moto utatoka katika vinywa vyao na kuwaua adui zao. Yeyote atakaye jaribu kuwadhuru atakufa. Mashahidi hawa wana nguvu ya kuzuia mvua isinyeshe katika wakati ambao watakuwa wanatabiri. Pia wana uwezo wa kugeuza maji kuwa damu. Wana uwezo wa kutuma kila aina ya pigo duniani. Wanaweza kufanya hivi kadri wanavyotaka.

Mashahidi wawili watakapomaliza kuutangaza ujumbe wao, mnyama atokaye kuzimu atapigana nao. Atawashinda na kuwaua. Miili ya mashahidi hawa wawili italala kwenye mtaa wa mji mkuu. Mji huu unaitwa Sodoma na Misri. Majina ya mji huu yana maana maalumu. Huu ni mji ambako Bwana aliuawa. Watu kutoka kila asili, kabila, lugha na taifa wataiangalia miili ya mashahidi hawa wawili kwa siku tatu na nusu. Watu watakataa kuwazika. 10 Na Kila aishiye duniani atafurahi kwa sababu mashahidi hawa wawili wamekufa. Watu watafanya sherehe na kupeana zawadi kwa sababu manabii hawa wawili walileta mateso mengi kwa watu waishio duniani.

11 Lakini baada ya siku tatu na nusu, Mungu akawarudishia uhai mashahidi hawa wawili. Wakasimama kwa miguu yao. Na wale waliowaona wakajaa hofu. 12 Kisha mashahidi wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikisema, “Njooni huku juu!” Na wote wawili wakaenda juu mbinguni katika wingu, adui zao wakiangalia wanavyokwenda.

13 Katika wakati huo huo kulitokea tetemeko kuu la ardhi. Sehemu ya kumi ya mji ikateketea, na watu elfu saba wakafa. Wale ambao hawakufa waliogopa sana. Wakampa utukufu Mungu wa mbinguni.

14 Kitisho cha pili kimepita. Kitisho cha tatu kinakuja haraka.

Mlio wa tarumbeta ya Saba

15 Malaika wa saba alipopuliza tarumbeta yake, zikatokea sauti kuu mbinguni, zikasema:

“Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Masihi wake sasa.
    Na atatawala milele na milele.”

16 Kisha wazee 24 wakaanguka chini nyuso zao zikiwa chini wakamwabudu Mungu. Hawa ni wazee ambao wanakaa kwenye viti vyao vya heshima mbele za Mungu. 17 Wazee wakasema:

“Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi.
    Wewe ndiye uliyepo na ambaye daima umekuwepo.
Tunakushukuru kwa sababu umetumia uweza wako mkuu
    na umeanza kutawala.
18 Mataifa walikasirika,
    lakini sasa ni wakati kwa ajili ya hasira yako.
    Sasa ni wakati wa waliokufa kuhukumiwa.
Ni wakati wa kuwapa thawabu watumishi wako, manabii,
    na kuwapa thawabu watu wako watakatifu,
    wakubwa na wadogo, wanaokuheshimu wewe.
Ni wakati wa kuwaangamiza watu wanaoiangamiza dunia!”

19 Kisha hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa. Sanduku la Agano likaonekana ndani ya hekalu lake. Kisha kukatokea miali ya radi na miungurumo ya radi, kelele, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.

Footnotes

  1. 11:1 hekalu Nyumba ya Mungu. Mahali ambapo watu wa Mungu humwabudu na kumtumikia. Yohana hapa analitazama kama jengo maalumu katika mji wa Yerusalemu kwa ajili ya ibada za Kiyahudi. Pia katika mstari wa 19.