Mwana-Kondoo Na Waliokombolewa Wa Kwanza

14 Kisha nikatazama na mbele yangu nikamwona Mwana-Kondoo amesimama juu ya Mlima Sioni akiwa pamoja na watu 144,000 ambao kwenye vipaji vya nyuso zao waliandikwa jina la Mwana-Kondoo na jina la Baba yake. Basi nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maporomoko ya maji mengi na kama sauti ya ngurumo ya radi kubwa. Na sauti hiyo niliyoisikia, ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao. Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu 144,000 waliokombolewa kutoka duniani. Hao ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa kuhusiana na wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Hao ndio wanaomfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Wame nunuliwa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa matunda ya kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. Hawajapata kusema uongo kamwe; hawana hatia yo yote.

Malaika Watatu

Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani akiwa na Injili ya milele ya kuwatangazia watu wote waishio duniani: kwa mataifa yote, makabila yote, kwa watu wa lugha zote na watu wa aina zote. Akasema kwa sauti kuu, “Mcheni Mungu na kumtu kuza kwa maana saa ya kutoa hukumu yake imefika. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”

Malaika wa pili akafuata akisema, “Babiloni umeanguka! Babiloni mkuu umeanguka, ule mji mkuu ambao uliwanywesha mataifa yote divai yake, divai kali ya uzinzi wake.”

Malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kuu, “Kama mtu ye yote anamwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake kwenye kipaji cha uso wake au kwenye mkono wake, 10 yeye naye atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu ambayo imemiminiwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchan ganywa na maji. Naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya mal aika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. 11 Moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele; wala hakuna nafuu, mchana au usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake au kwa ye yote anayepokea alama ya jina lake.” 12 Jambo hili linahitaji watu wa Mungu, wale ambao wanazishika amri zake, wawe wavumilivu na kumwamini Yesu.

13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika haya: Wamebarikiwa watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa ndani ya Bwana.” “Naam,” asema Roho, “watapumzika baada ya taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”

Mavuno

14 Nikatazama, na mbele yangu nikaona wingu jeupe na mtu anayeonekana kama ‘mwana wa mtu’ akiwa ameketi juu yake. Alikuwa na taji ya dhahabu kichwani mwake na mundu mkali mkononi mwake. 15 Na malaika mwingine akaja kutoka Hekaluni na kwa sauti kubwa akamwita yule aliyekuwa ameketi juu ya wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa saa ya kuvuna imefika, maana mavuno ya dunia yamekomaa.” 16 Basi yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akauzungusha mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa.

17 Kisha malaika mwingine akatoka Hekaluni mbinguni, naye pia akiwa na mundu mkali.

18 Na malaika mwingine, ambaye alikuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kuu, akasema, “Chukua mundu wako mkali ukayakate matawi ya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.”

19 Basi malaika huyo akauzungusha mundu wake duniani akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya mtambo mkubwa wa kusindika zabibu wa ghadhabu ya Mungu. 20 Zabibu zikakamuliwa ndani ya mtambo huo wa kusindika zabibu uliokuwa nje ya mji, na damu ika tiririka kama mafuriko kutoka katika mtambo huo na urefu wa mafu riko hayo ulikuwa kama kilometa mia tatu, na kina chake kiasi cha meta moja na nusu.

Watu wa Mungu Waimba Wimbo Mpya

14 Kisha nikatazama, na mbele yangu alikuwepo Mwanakondoo, amesimama juu ya Mlima Sayuni.[a] Watu 144,000 walikuwa pamoja naye. Jina lake na la Baba yake yalikuwa yameandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao.

Nikasikia sauti kutoka mbinguni yenye kelele kama mafuriko au ngurumo ya radi. Lakini ilisikika kama sauti ya wapiga vinubi wapigao vinubi vyao. Watu waliimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na viumbe wenye uhai wanne na wazee. Walioujua wimbo mpya ni wale 144,000 tu walionunuliwa kutoka duniani. Hakuna mwingine tena aliyekuwa anaujua.

Hawa ni wale ambao hawakuzini na wanawake.[b] Walijiweka safi. Na Sasa wanamfuata Mwanakondoo kila aendako. Walinunuliwa kutoka miongoni mwa watu wa dunia ili kuwa wa kwanza, kuwa sadaka kwa Mungu na Mwanakondoo. Hawana hatia ya kusema uongo; hawana kosa.

Malaika Watatu

Kisha nikaona malaika mwingine akipaa juu angani, akitangaza Habari Njema ya milele kwa watu waishio duniani, watu wa kila taifa, kabila, lugha na rangi. Malaika akasema kwa sauti kuu, “Mcheni Mungu na msifuni yeye. Wakati wa Mungu kuwahukumu watu wote umefika. Mwabuduni Mungu. Aliumba mbingu, dunia, bahari na chemichemi za maji.”

Kisha malaika wa pili akamfuata malaika wa kwanza na kusema, “Ameteketezwa! Mji mkuu Babeli umeteketezwa! Aliwafanya mataifa yote kunywa mvinyo wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu.”

Malaika wa tatu aliwafuata malaika wawili wa kwanza. Malaika huyu wa tatu alisema kwa sauti kuu, “Mungu atawaadhibu wote wanaomwabudu mnyama na sanamu ya mnyama na kukubali kuwa na alama ya mnyama katika vipaji vya nyuso zao au kwenye mkono wao. 10 Watakunywa mvinyo wa ghadhabu ya Mungu.[c] Mvinyo huu umeandaliwa kwa nguvu zake zote katika kikombe cha ghadhabu ya Mungu. Watateseka kwa maumivu ya moto uwakao kwa kiberiti mbele ya malaika watakatifu na Mwanakondoo. 11 Na moshi kutokana na kuungua kwao utasimama milele na milele. Hakutakuwa mapumziko, usiku na mchana kwa wale wamwabuduo mnyama au sanamu yake au wale wavaao alama ya jina lake.” 12 Hii inamaanisha kuwa ni lazima watakatifu wa Mungu wawe na subira. Ni lazima wazitii amri za Mungu nakuendelea kumwamini Yesu.

13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Liandike hili: Kuanzia sasa heri wale wanaokufa wakiwa wa Bwana.”

Roho Mtakatifu anasema, “Ndiyo, hilo ni kweli. Watapumzika kutokana na kazi yao ngumu. Yale waliyotenda yatakaa pamoja nao.”

Dunia Yavunwa

14 Nikatazama, na mbele yangu, katika wingu jeupe, alikuwepo mmoja aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa na taji ya dhahabu kwenye kichwa chake na mundu mkali mkononi mwake. 15 Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, akamwambia aliyekaa kwenye wingu, “Chukua mundu wako na ukusanye kutoka duniani. Wakati wa kuvuna umefika, na tunda limeiva duniani.” 16 Hivyo aliyekaa kwenye wingu akaupitisha mundu wake juu ya dunia. Na dunia ikavunwa.

17 Ndipo malaika mwingine akatoka hekaluni mbinguni. Malaika huyu naye alikuwa na mundu mkali. 18 Na malaika mwingine, aliyekuwa msimamizi wa moto wa madhabahu akatoka madhabahuni. Akamwita malaika mwenye mundu mkali na kusema, “Chukua mundu wako wenye makali na ukusanye mafungu ya zabibu kutoka shamba la mizabibu duniani. Zabibu zimeiva duniani.” 19 Malaika akaupitisha mundu juu ya dunia. Akakusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. 20 Zabibu zikaminywa kwenye shinikizo nje ya mji. Damu ikatiririka kutoka kwenye shinikizo, ikanyanyuka juu kama vichwa vya farasi kwa urefu wa kilomita mia tatu.[d]

Footnotes

  1. 14:1 Mlima Sayuni Jina jingine la Yerusalemu, hapa limetumika kumaanisha mji wa kiroho ambamo watu wa Mungu wanaishi pamoja naye.
  2. 14:4 hawakuzini na wanawake Ubikira au kuwa safi dhidi ya zinaa ni ishara ya kuwa na imani kwa Mungu kwa kupinga majaribu na kila aina ya ibada ya sanamu.
  3. 14:10 Watakunywa … Mungu Wayunani na Warumi wa kale walikuwa na kawaida ya kunywa mvinyo uliochanganywa na maji. Anachokisema malaika hapa ni kwamba mvinyo huu wa ghadhabu ya Bwana umemwagwa pasipo kuchanganywa na maji. Ni mvinyo ulio na nguvu yake yote pasipo kulainishwa na maji.
  4. 14:20 kilomita mia tatu Kwa maana ya kawaida, “stadia 1,600”.