Mashahidi Wawili

11 Ndipo nikapewa kipimo kama fimbo, nikaambiwa, “Nenda kapime Hekalu la Mungu pamoja na madhabahu na uwahesabu watu waabuduo humo. Lakini usipime uwanja wa nje ya Hekalu, uache, kwa sababu uwanja huo wamepewa mataifa wasiomjua Mungu. Wao wataukanyagakanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili. Nami nitawapa uwezo mashahidi wangu wawili watoe unabii kwa muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini na mbili, wakiwa wamevaa magunia.”

Manabii hao wawili ni ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana na mbele ya nchi yote. Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka vinywani mwao na kuwateketeza adui zao. Na hivyo ndivyo atakavyokufa mtu ye yote atakayetaka kuwad huru. Watu hawa wanayo mamlaka ya kuyafunga mawingu ili mvua isinyeshe wakati wote watakapokuwa wanatoa unabii wao. Watakuwa na mamlaka juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuleta maafa ya kila aina ulimwenguni, kama wapendavyo. Lakini wakishamaliza kutoa unabii huo, yule mnyama atokaye katika shimo la kuzimu ata wapiga vita na kuwashinda na kuwaua. Maiti zao zitabaki katika barabara ya mji mkuu ambao kwa fumbo unaitwa Sodoma na Misri, ambapo Bwana wao alisulubiwa. Kwa muda wa siku tatu na nusu, watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti zao, na hawataruhusu wazikwe. 10 Watu waishio duniani watafura hia kifo cha manabii hao wawili na kushangilia kwa kupeana zawadi kwa sababu manabii hao waliwatesa watu waishio ulimwenguni.

11 Lakini baada ya zile siku tatu na nusu, pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu. 12 Kisha wale manabii wawili wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njooni huku juu!” Nao wakapaa mbinguni katika wingu, wakati maadui zao wakiwatazama. 13 Wakati huo huo, kukatokea tetemeko kuu la nchi, na sehemu moja ya kumi ya mji ikaanguka. Watu elfu saba wakauawa katika tetemeko hilo na waliosalimika wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.

14 Maafa ya pili yamekwisha kupita. Lakini maafa ya tatu yanakuja upesi.

Tarumbeta Ya Saba

15 Kisha malaika wa saba akapiga tarumbeta yake. Na sauti kuu zikasikika mbinguni zikisema, “Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na Kristo wake, naye atatawala milele na milele.” 16 Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vyao vya enzi wakaanguka kifudifudi wakamwabudu Mungu, 17 wakisema, “Tunakushukuru, Bwana Mungu Mwenyezi uli yeko na uliyekuwako; kwa kuwa umeuchukua uweza wako mkuu na ukaanza kutawala. 18 Watu wa mataifa walikasirika kwa kuwa wakati wa ghadhabu yako umefika. Wakati umefika wa kuwahukumu wafu na kuwapa tuzo watumishi wako manabii na watakatifu walioli tukuza jina lako, wakubwa kwa wadogo; na wakati umefika wa kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.”

19 Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa na sanduku la agano lake likaonekana Hekaluni mwake. Kukatokea umeme, sauti, ngurumo na tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.