Add parallel Print Page Options

Malaika Na Kitabu kidogo

10 Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni akiwa amevikwa wingu na upinde wa mvua ulizunguka kichwa chake. Uso wake ulikuwa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto. Malaika alikuwa ameshika kitabu kidogo kilichofunguliwa. Akaweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na mguu wa kushoto nchi kavu. Alipaza sauti yake kama simba anavyounguruma na sauti za radi saba zikasikika.

Radi saba ziliongea, na nikaanza kuandika. Lakini nilisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Usiandike ambacho radi saba zinasema. Yaache mambo hayo yawe siri.”

Kisha nikamwona malaika aliyesimama juu ya bahari na nchi kavu akinyoosha mkono wake kuelekea mbinguni. Malaika akaapa kwa nguvu ya yule aishiye milele na milele. Ndiye aliyeziumba mbingu na vyote vilivyomo ndani yake. Aliumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, na aliumba bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Malaika alisema, “Hakutakuwa kusubiri tena! Katika siku ambazo malaika wa saba atakuwa tayari kupuliza tarumbeta yake, mpango wa siri wa Mungu utakamilika, nao ni Habari Njema ambayo Mungu aliwaambia watumishi wake, manabii.”

Kisha nikasikia tena sauti ile ile kutoka mbinguni. Ikaniambia, “Nenda ukachukue kitabu kilicho wazi mkononi mwa malaika, aliyesimama juu ya bahari na nchi kavu.”

Hivyo nilimwendea malaika nikamwomba anipe kitabu kidogo. Naye aliniambia, “Chukua kitabu na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako lakini kitakuwa kitamu kama asali mdomoni mwako.” 10 Hivyo nilichukua kitabu kidogo kutoka mkononi mwa malaika na kukila. Mdomoni mwangu kilikuwa na ladha tamu kama asali, lakini baada ya kukila, kilikuwa kichungu tumboni mwangu. 11 Kisha nikaambiwa, “Ni lazima uwatabirie tena watu wa asili tofauti, mataifa, lugha na watawala.”