Add parallel Print Page Options

Watu wa Mungu Waimba Wimbo Mpya

14 Kisha nikatazama, na mbele yangu alikuwepo Mwanakondoo, amesimama juu ya Mlima Sayuni.[a] Watu 144,000 walikuwa pamoja naye. Jina lake na la Baba yake yalikuwa yameandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao.

Nikasikia sauti kutoka mbinguni yenye kelele kama mafuriko au ngurumo ya radi. Lakini ilisikika kama sauti ya wapiga vinubi wapigao vinubi vyao. Watu waliimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na viumbe wenye uhai wanne na wazee. Walioujua wimbo mpya ni wale 144,000 tu walionunuliwa kutoka duniani. Hakuna mwingine tena aliyekuwa anaujua.

Hawa ni wale ambao hawakuzini na wanawake.[b] Walijiweka safi. Na Sasa wanamfuata Mwanakondoo kila aendako. Walinunuliwa kutoka miongoni mwa watu wa dunia ili kuwa wa kwanza, kuwa sadaka kwa Mungu na Mwanakondoo. Hawana hatia ya kusema uongo; hawana kosa.

Malaika Watatu

Kisha nikaona malaika mwingine akipaa juu angani, akitangaza Habari Njema ya milele kwa watu waishio duniani, watu wa kila taifa, kabila, lugha na rangi. Malaika akasema kwa sauti kuu, “Mcheni Mungu na msifuni yeye. Wakati wa Mungu kuwahukumu watu wote umefika. Mwabuduni Mungu. Aliumba mbingu, dunia, bahari na chemichemi za maji.”

Kisha malaika wa pili akamfuata malaika wa kwanza na kusema, “Ameteketezwa! Mji mkuu Babeli umeteketezwa! Aliwafanya mataifa yote kunywa mvinyo wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu.”

Malaika wa tatu aliwafuata malaika wawili wa kwanza. Malaika huyu wa tatu alisema kwa sauti kuu, “Mungu atawaadhibu wote wanaomwabudu mnyama na sanamu ya mnyama na kukubali kuwa na alama ya mnyama katika vipaji vya nyuso zao au kwenye mkono wao. 10 Watakunywa mvinyo wa ghadhabu ya Mungu.[c] Mvinyo huu umeandaliwa kwa nguvu zake zote katika kikombe cha ghadhabu ya Mungu. Watateseka kwa maumivu ya moto uwakao kwa kiberiti mbele ya malaika watakatifu na Mwanakondoo. 11 Na moshi kutokana na kuungua kwao utasimama milele na milele. Hakutakuwa mapumziko, usiku na mchana kwa wale wamwabuduo mnyama au sanamu yake au wale wavaao alama ya jina lake.” 12 Hii inamaanisha kuwa ni lazima watakatifu wa Mungu wawe na subira. Ni lazima wazitii amri za Mungu nakuendelea kumwamini Yesu.

13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Liandike hili: Kuanzia sasa heri wale wanaokufa wakiwa wa Bwana.”

Roho Mtakatifu anasema, “Ndiyo, hilo ni kweli. Watapumzika kutokana na kazi yao ngumu. Yale waliyotenda yatakaa pamoja nao.”

Dunia Yavunwa

14 Nikatazama, na mbele yangu, katika wingu jeupe, alikuwepo mmoja aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa na taji ya dhahabu kwenye kichwa chake na mundu mkali mkononi mwake. 15 Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, akamwambia aliyekaa kwenye wingu, “Chukua mundu wako na ukusanye kutoka duniani. Wakati wa kuvuna umefika, na tunda limeiva duniani.” 16 Hivyo aliyekaa kwenye wingu akaupitisha mundu wake juu ya dunia. Na dunia ikavunwa.

17 Ndipo malaika mwingine akatoka hekaluni mbinguni. Malaika huyu naye alikuwa na mundu mkali. 18 Na malaika mwingine, aliyekuwa msimamizi wa moto wa madhabahu akatoka madhabahuni. Akamwita malaika mwenye mundu mkali na kusema, “Chukua mundu wako wenye makali na ukusanye mafungu ya zabibu kutoka shamba la mizabibu duniani. Zabibu zimeiva duniani.” 19 Malaika akaupitisha mundu juu ya dunia. Akakusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. 20 Zabibu zikaminywa kwenye shinikizo nje ya mji. Damu ikatiririka kutoka kwenye shinikizo, ikanyanyuka juu kama vichwa vya farasi kwa urefu wa kilomita mia tatu.[d]

Footnotes

  1. 14:1 Mlima Sayuni Jina jingine la Yerusalemu, hapa limetumika kumaanisha mji wa kiroho ambamo watu wa Mungu wanaishi pamoja naye.
  2. 14:4 hawakuzini na wanawake Ubikira au kuwa safi dhidi ya zinaa ni ishara ya kuwa na imani kwa Mungu kwa kupinga majaribu na kila aina ya ibada ya sanamu.
  3. 14:10 Watakunywa … Mungu Wayunani na Warumi wa kale walikuwa na kawaida ya kunywa mvinyo uliochanganywa na maji. Anachokisema malaika hapa ni kwamba mvinyo huu wa ghadhabu ya Bwana umemwagwa pasipo kuchanganywa na maji. Ni mvinyo ulio na nguvu yake yote pasipo kulainishwa na maji.
  4. 14:20 kilomita mia tatu Kwa maana ya kawaida, “stadia 1,600”.