Add parallel Print Page Options

Mwanamke Juu ya Mnyama Mwekundu

17 Mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli sa akaja kuzungumza nami. Akasema, “Njoo, nami nitakuonesha adhabu itakayotolewa kwa kahaba maarufu. Ndiye yule aketiye juu ya maji mengi. Watawala wa dunia walizini pamoja naye. Watu wa dunia walilewa kutokana na mvinyo wa dhambi yake ya uzinzi.”

Kisha malaika akanichukua mbali kwa Roho Mtakatifu mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke amekaa juu ya mnyama mwekundu. Mnyama alikuwa ameandikwa majina ya kumkufuru Mungu katika mwili wake wote. Alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. Mwanamke aliyekuwa juu yake alikuwa amevaa nguo za zambarau na nyekundu. Alikuwa anang'aa kutokana na dhahabu, vito na lulu alizokuwa amevaa. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu. Kikombe hiki kilijaa maovu na machukizo ya dhambi yake ya uzinzi. Alikuwa na jina kwenye kipaji cha uso wake. Jina hili lina maana iliyofichwa. Hiki ndicho kilichoandikwa:

babeli mkuu

mama wa makahaba

na machukizo ya dunia.

Nikatambua kuwa mwanamke alikuwa amelewa. Alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu wa Mungu. Alikuwa amelewa kwa damu ya wale walioshuhudia imani yao katika Yesu Kristo.

Nilipomwona mwanamke, nilishangaa sana. Kisha malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Nitakuambia maana iliyofichwa kuhusu mwanamke huyu na mnyama mwenye vichwa saba na pembe kumi anayeendeshwa na mwanamke huyu. Mnyama unayemwona alikuwa hai kwanza, lakini sasa si hai. Hata hivyo, atapanda kutoka kuzimu na kwenda kuangamizwa. Watu wanaoishi duniani watashangaa watakapomwona mnyama, kwa sababu aliwahi kuwa hai, hayuko hai, lakini atakuwa hai tena. Hawa ni watu ambao majina yao hayajawahi kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu.

Unahitaji hekima kulielewa hili. Vichwa saba juu ya mnyama ni milima saba ambako mwanamke amekaa. Pia ni watawala saba. 10 Watawala watano wamekwisha kufa tayari. Mmoja wa watawala anaishi sasa, na mtawala wa mwisho anakuja. Atakapokuja, atakaa kwa muda mfupi tu. 11 Mnyama ambaye hapo kwanza alikuwa hai, lakini haishi tena ni mtawala wa nane. Naye ni mmoja wa watawala saba wa kwanza. Naye ataangamizwa.

12 Pembe kumi ulizoziona ni watawala kumi. Watawala hawa kumi hawajapata falme zao, lakini watapata nguvu ya kutawala pamoja na mnyama kwa saa moja. 13 Lengo la watawala hawa wote kumi linafanana. Nao watampa mnyama nguvu na mamlaka yao. 14 Watafanya vita kinyume na Mwanakondoo. Lakini Mwanakondoo atawashinda, kwa sababu ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Pamoja naye watakuwepo wateule wake na wafuasi waaminifu, watu aliowaita kuwa wake.”

15 Kisha malaika akaniambia, “Uliyaona maji ambako kahaba amekaa. Maji haya ni watu wengi, wa asili, mataifa, na lugha tofauti ulimwenguni. 16 Mnyama na pembe kumi ulizoziona watamchukia kahaba. Watachukua kila kitu alichonacho na kumwacha akiwa uchi. Watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto. 17 Mungu aliweka wazo katika akili zao kutenda yale yatakayotimiza kusudi lake. Walikubaliana kumpa mnyama nguvu zao kutawala mpaka yale aliyosema Mungu yamekamilika. 18 Mwanamke uliyemwona ni mji mkuu ambao unatawala juu ya wafalme wa dunia.”