Add parallel Print Page Options

Babeli Inaangamizwa

18 Kisha nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Malaika huyu alikuwa na nguvu kuu. Utukufu wa malaika ukaing'arisha dunia. Malaika akapaza sauti akasema:

“Ameteketezwa!
    Mji mkuu Babeli umeteketezwa!
Umekuwa nyumba ya mapepo.
    Mji ule umekuwa najisi.
Mji uliojaa kila aina ya ndege najisi.
    Ni mahali ambapo kila mnyama najisi
    na anayechukiwa anaishi.
Watu wote wa dunia wamekunywa mvinyo
    wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu.
Watawala wa dunia walizini pamoja naye,
    na wafanya biashara wa ulimwengu walitajirika
    kutokana na utajiri wa anasa zake.”

Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema:

“Enyi watu wangu, tokeni katika mji huo,
    ili msishiriki katika dhambi zake.
    Ili msiteseke kwa adhabu yoyote kuu atakayoipata.
Dhambi za mji huo zimerundikana na kufika mbinguni.
    Mungu hajasahau makosa aliyotenda.
Upeni mji huo sawasawa na ulivyowapa wengine.
    Mlipeni mara mbili kadiri ya alivyotenda.
Mwandalieni mvinyo ulio na nguvu mara mbili
    ya mvinyo aliowaandalia wengine.
Alijipa utukufu mwingi na kuishi kitajiri.
    Mpeni mateso mengi na huzuni nyingi.
    Kama vile utukufu na starehe aliyoifurahia.
Hujisemea mwenyewe, ‘Mimi ni malkia nikaaye kwenye kiti changu cha enzi.
    Mimi si mjane;
    Sitakuwa na huzuni.’
Hivyo katika siku moja atateseka
    kwa njaa kuu, maombolezo na kifo.
Atateketezwa kwa moto,
    kwa sababu Bwana Mungu anayemhukumu ni mwenye nguvu.”

Watawala wa dunia waliozini pamoja naye na kushiriki utajiri wake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watalia na kuhuzunika kwa sababu ya kifo chake. 10 Wataogopa mateso yake na kukaa mbali sana. Watasema:

“Inatisha! Inatisha sana, Ee mji mkuu,
    ee Babeli, mji wenye nguvu!
Adhabu yako imekuja katika saa moja!”

11 Na wafanya biashara wa dunia watalia na kuhuzunika kwa ajili yake. Watahuzunika kwa sababu hakutakuwa hata mmoja wa kununua vitu wanavyouza; 12 dhahabu, fedha, vito, lulu, nguo za kitani safi, nguo za zambarau, hariri na nguo nyekundu, aina zote za mti wa udi, na aina zote za vitu vilivyotengenezwa kutokana na pembe za wanyama, miti ya thamani, shaba, chuma, na marimari. 13 Na mdalasini, viungo, uvumba, marhamu, ubani, mvinyo, mafuta ya mzeituni, unga safi, ngano, ng'ombe, kondoo, farasi, magari na watumwa, ndiyo hata maisha ya watu. Wafanya biashara watalia na kusema:

14 “Ee Babeli, mambo mazuri uliyoyataka yamekuacha.
Utajiri wako wote na vitu vya fahari vimetoweka.
    Hautakuwa navyo tena.”

15 Wafanya biashara wataogopa mateso yake na watakaa mbali naye. Hawa ni wale waliotajirika kwa kumwuzia vitu hivyo. Watalia na kuhuzunika. 16 Watasema:

“Inatisha! Inatisha kwa mji mkuu!
    Alivalishwa kitani safi;
    alivaa zambarau na nguo nyekundu.
    Alikuwa anang'aa kwa sababu ya dhahabu, vito na lulu!
17 Utajiri wote huu umeteketezwa kwa saa moja!”

Kila nahodha, wote ambao husafiri katika meli, mabaharia na wote ambao hupata pesa kutokana na bahari walisimama mbali na Babeli. 18 Waliuona moshi wa kuungua kwake. Walilia kwa sauti, “Hakukuwa na mji kama mji huu mkuu!” 19 Walirusha mavumbi juu ya vichwa vyao na kulia kwa sauti kuu kuonesha huzuni kuu waliyokuwa nayo. Walisema:

“Inatisha! Inatisha sana kwa mji mkuu!
    Wote waliokuwa na meli baharini walitajirika kwa sababu ya utajiri wake!
    Lakini umeteketezwa katika saa moja!
20 Ufurahi kwa sababu ya hili, Ee mbingu!
    Furahini, watakatifu wa Mungu, mitume na manabii!
Mungu amemhukumu kwa sababu ya kile alichowatendea ninyi.”

21 Kisha malaika mwenye nguvu akainua jiwe kubwa. Jiwe hili lilikuwa kubwa kama jiwe kubwa la kusagia. Malaika akalitupia jiwe baharini na kusema:

“Hivyo ndivyo mji mkuu Babeli utakavyotupwa chini.
    Hautaonekana tena.
22 Ee Babeli, muziki wa wapigao vinanda na ala zingine waimbaji na tarumbeta,
    hautasikika tena ndani yako.
Hakuna mfanyakazi afanyaye kazi atakayeonekana ndani yako tena.
    Sauti ya jiwe la kusagia haitasikika ndani yako tena.
23 Mwanga wa taa hautang'aa ndani yako tena.
    Sauti za maarusi hazitasikika ndani yako tena.
Wafanyabiashara wako walikuwa watu wakuu wa ulimwengu.
    Mataifa yote yalidanganyika kwa uchawi wako.
24 Una hatia ya vifo vya manabii, na watakatifu wa Mungu,
    na vya wote waliouawa duniani.”