Add parallel Print Page Options

Watu Wamsifu Mungu Mbinguni

19 Baada ya hili nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu mbinguni. Walikuwa wakisema:

“Haleluya![a]
Ushindi, utukufu na nguvu ni vyake Mungu wetu.
    Hukumu zake ni za kweli na za haki.
Mungu wetu amemwadhibu kahaba.
    Ndiye aliyeiharibu dunia kwa uzinzi wake.
Mungu amemwadhibu kahaba kulipa kisasi cha vifo vya watumishi wake.”

Pia, watu hawa walisema:

“Haleluya!
    Anaungua na moshi wake utasimama milele na milele.”

Ndipo wazee ishirini na nne na viumbe wenye uhai wanne wakaanguka chini kusujudu wakamwabudu Mungu, akaaye kwenye kiti cha enzi. Wakasema:

“Amina! Haleluya!”

Sauti ikatoka kwenye kiti cha enzi na kusema:

“Msifuni Mungu wetu,
    ninyi nyote mnaomtumikia!
Msifuni Mungu wetu,
    ninyi nyote mlio wadogo na wakubwa mnaomheshimu!”

Kisha nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu. Kilikuwa na kelele kama mawimbi ya bahari au radi. Watu walikuwa wakisema:

“Haleluya!
    Bwana Mungu wetu anatawala.
    Ndiye Mwenye Nguvu, Mungu Mwenyezi.
Tushangilie na kufurahi na
    kumpa Mungu utukufu!
Mpeni Mungu utukufu, kwa sababu arusi ya Mwanakondoo imewadia.
    Na bibi arusi wa Mwanakondoo amekwisha jiandaa.
Nguo ya kitani safi ilitolewa kwa bibi arusi ili avae.
    Kitani ilikuwa safi na angavu.”

(Kitani safi inamaanisha mambo mazuri ambayo watakatifu wa Mungu waliyatenda.)

Kisha malaika akaniambia, “Andika hili: Heri ni kwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo!” Kisha malaika akasema, “Haya ni maneno ya Mungu mwenyewe.”

10 Kisha nikaanguka chini mbele miguuni pa malaika ili nimwabudu. Lakini malaika akaniambia, “Usiniabudu! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako na dada zako walio na ushuhuda kuhusu Yesu Kristo. Hivyo mwabudu Mungu! Kwa sababu ushuhuda kuhusu Yesu ndiyo roho ya unabii.”

Mpanda Farasi Juu ya Farasi Mweupe

11 Kisha nikaona mbingu zimefunguka, na nikamwona farasi mweupe. Mpanda farasi aliitwa Mwaminifu na Kweli, kwa sababu ni wa haki katika maamuzi yake na kufanya vita. 12 Macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. Alikuwa na taji nyingi kichwani mwake. Jina lilikuwa limeandikwa juu yake, lakini yeye peke yake ndiye aliyejua maana ya jina hilo. 13 Alivaa vazi lililochovywa katika damu, na aliitwa Neno la Mungu. 14 Majeshi ya mbinguni yalikuwa yanamfuata mpanda farasi mweupe. Walikuwa wanaendesha farasi weupe pia. Walikuwa wamevaa kitani nzuri, nyeupe na safi. 15 Upanga mkali ulikuwa unatoka kwenye kinywa chake, upanga ambao angeutumia kuyashinda mataifa. Na atayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Atazikanyaga zabibu katika shinikizo la ghadhabu ya Mungu Mwenye Nguvu. 16 Kwenye vazi lake na kwenye mguu wake alikuwa ameandikwa jina lake:

mfalme wa wafalme na bwana wa mabwana.

17 Kisha nikaona malaika amesimama katika jua. Kwa sauti kuu malaika akawaambia ndege wote wanaoruka angani, “Kusanyikeni kwa ajili ya karamu kuu ya Mungu. 18 Kusanyikeni mle miili ya watawala, majemadari na watu maarufu. Njooni mle miili ya farasi na wanaowapanda na miili ya watu wote, walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”

19 Kisha nikamwona mnyama na watawala wa dunia. Majeshi yao yalikusanyika pamoja ili kufanya vita kupigana na mpanda farasi mweupe na jeshi lake. 20 Lakini mnyama na nabii wa uongo walikamatwa. Nabii wa uongo ndiye aliyefanya miujiza[b] kwa ajili ya mnyama. Alitumia miujiza hii kuwahadaa wale waliokuwa na alama ya mnyama na walioabudu sanamu yake. Nabii wa uongo na mnyama walitupwa kwenye ziwa la moto linalowaka kwa baruti. 21 Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kwenye kinywa cha mpanda farasi. Ndege wote walikula miili hii mpaka wakashiba.

Footnotes

  1. 19:1 Haleluya Yaani “Msifuni Mungu!” Pia katika mstari wa 3,4,6.
  2. 19:20 miujiza Miujiza ya uongo ama matukio ya ajabu yanayofanywa kwa kutumia nguvu ya mwovu.