Add parallel Print Page Options

Yerusalemu Mpya

21 Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu na dunia ya kwanza vilikwisha kutoweka. Na sasa bahari haikuwepo. Nikauona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya,[a] ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu. Ulikuwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyevalishwa kwa ajili ya mumewe.

Nikasikia sauti kuu kutoka kwenye kiti cha enzi. Ikisema, “Makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu. Yeye ataishi pamoja nao. Na wao watakuwa watu wake. Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao naye atakuwa Mungu wao. Atafuta kila chozi kutoka machoni mwaona. Hakutakuwa na kifo tena, huzuni, kilio wala maumivu. Namna zote za zamani zimepita.”

Aliyekaa kwenye kiti cha enzi akasema, “Tazama, sasa ninakiumba kila kitu upya!” Kisha akasema, “Andika hili, kwa sababu maneno haya ni kweli na ya kuaminiwa.”

Akaniambia, “Imekwisha! Mimi ni Alfa na Omega,[b] Mwanzo na Mwisho. Kila mwenye kiu nitampa bure maji kutoka kwenye chemichemi ya maji ya uzima. Wale wote watakaoshinda watapokea yote haya. Na nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watoto wangu. Lakini waoga, wanaokataa kuniamini, wafanyao mambo ya kuchukiza, wauaji, wazinzi, wachawi, waabuduo sanamu na waongo, nitawatupa katika ziwa linalowaka moto. Hii ni mauti ya pili.”

Mmoja wa malaika saba akaja kwangu. Huyu alikuwa mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli saba zilizojaa mapigo saba ya mwisho. Malaika akasema, “Njoo huku. Nitakuonesha bibi arusi, mke wa Mwanakondoo.” 10 Malaika akanichukua kwa Roho Mtakatifu mpaka kwenye mlima mkubwa na mrefu. Akanionyesha mji mtakatifu wa Yerusalemu. Mji ulikuwa ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu.

11 Mji ulikuwa unang'aa kwa utukufu wa Mungu. Ulikuwa unang'aa kwa uangavu kama yaspi, kito cha thamani sana. Ulionekana kwa uwazi kama kioo. 12 Mji ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mbili. Kulikuwa malaika kumi na mbili kwenye milango. Kwenye kila mlango kuliandikwa jina la kabila moja la Israeli. 13 Yalikuwepo malango matatu upande wa mashariki, malango matatu kaskazini, malango matatu kusini, na malango matatu magharibi. 14 Kuta za mji zilijengwa kwenye mawe kumi na mbili ya msingi. Kwenye mawe kulikuwa kumeandikwa majina ya mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo.

15 Malaika aliyezungumza na mimi alikuwa na fimbo ya kupimia iliyotengenezwa kwa dhahabu. Alikuwa na fimbo hii ili kuupima mji, malango na ukuta wake. 16 Mji ulijengwa kimraba. Urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Malaika aliupima mji kwa fimbo. Mji ulikuwa na urefu wa kilomita 2,400,[c] upana wake ulikuwa kilomita 2,400, na kimo chake kwenda juu kilikuwa kilomita 2,400. 17 Malaika akaupima ukuta pia. Kimo cha ukuta kilikuwa ni mita 60[d] kwenda juu. (Malaika alikuwa anatumia vipimo ambavyo watu hutumia.) 18 Ukuta ulijengwa kwa yaspi. Mji ulijengwa kwa dhahabu safi, iliyo safi kama kioo.

19 Mawe ya msingi wa ukuta wa mji yalikuwa na kila aina ya vito vya thamani ndani yake. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa yaspi, la pili lilikuwa yakuti samawi, la tatu lilikuwa kalkedoni, la nne lilikuwa zumaridi, 20 la tano lilikuwa sardoniki, la sita lilikuwa akiki, la saba lilikuwa krisolitho, la nane lilikuwa zabarajadi, la tisa lilikuwa yakuti ya manjano, la kumi lilikuwa krisopraso, la kumi na moja lilikuwa hiakintho na la kumi na mbili lilikuwa amethisto. 21 Malango kumi na mbili yalikuwa lulu kumi na mbili. Kila lango lilitengenezwa kwa lulu moja. Mitaa ya mji ilitengenezwa kwa dhahabu safi, inayong'aa kama kioo.

22 Sikuona hekalu ndani ya mji. Bwana Mungu Mwenye Nguvu na Mwanakondoo ndiyo waliokuwa hekalu la mji. 23 Mji haukuhitaji jua wala mwezi kuung'arizia. Utukufu wa Mungu uliupa mji mwanga. Mwanakondoo ndiye alikuwa taa ya mji.

24 Mataifa watatembea katika mwanga unaotoka katika mji ule.[e] Watawala wa dunia wataleta utukufu wao katika mji. 25 Milango ya mji haitafungwa hata siku moja, kwa sababu hakutakuwa usiku huko. 26 Ukuu na heshima ya mataifa vitaletwa katika mji. 27 Kilicho najisi hakitaingia katika mji. Atendaye mambo ya kuchukiza na mwongo hawataingia katika mji huo. Walioandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwanakondoo tu, ndiyo watakaoingia katika mji huo.

Footnotes

  1. 21:2 Yerusalemu mpya Mji wa kiroho ambako Mungu ataishi pamoja na watu wake.
  2. 21:6 Alfa na Omega Herufi ya kwanza na ya mwisho katika mfumo wa herufi wa Kiyunani, hapa inamaanisha “wa Kwanza na wa Mwisho”. Pia katika 22:13.
  3. 21:16 kilomita 2,400 Kwa maana ya kawaida, “stadia 12,000”.
  4. 21:17 mita 60 Sawa na dhiraa 144 ama futi 197. Dhiraa moja ni urefu wa mkono wa mtu kuanzia kwenye kiwiko cha mkono mpaka kwenye nje ya kidole kidogo, kama nusu mita.
  5. 21:24 Yaani, “Mwanakondoo”.