Add parallel Print Page Options

Mungu Amesema Kupitia Mwanaye

Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa kuwatumia manabii. Alisema nao mara nyingi na kwa njia nyingi tofauti. Lakini sasa katika siku hizi za mwisho Mungu amesema nasi tena kupitia Mwana wake. Mungu aliuumba ulimwengu wote kupitia Mwana wake. Na alimchagua Mwana kumiliki mambo yote. Huyo Mwana huuonesha utukufu wa Mungu. Yeye ni nakala halisi ya asili yake Mungu, na huviunganisha vitu vyote pamoja kwa amri yake yenye nguvu. Mwana aliwasafisha watu kutoka katika dhambi zao. Kisha akaketi upande wa kuume[a] wa Mungu, aliye Mkuu huko Mbinguni. Mwana akawa mkuu zaidi kuliko malaika, na Mungu akampa jina lililo kuu zaidi kuliko lolote katika majina yao.

Mungu kamwe hajamwambia malaika yeyote maneno haya:

“Wewe ni Mwanangu.
    Mimi leo hii nimekuwa Baba yako.”(A)

Mungu pia kamwe hajasema juu ya malaika,

“Nitakuwa Baba yake,
    naye atakuwa mwanangu.”(B)

Na kisha, pale Mungu anapomtambulisha Mwanaye mzaliwa wa kwanza ulimwenguni,[b] anasema,

“Basi malaika wote wa Mungu wamwabudu yeye.”[c]

Hivi ndivyo Mungu alivyosema kuhusu malaika:

“Yeye huwabadilisha malaika zake kuwa upepo[d]
    na watumishi wake kuwa miali ya moto.”(C)

Lakini hivi ndivyo alivyosema kuhusu Mwana wake:

“Mungu, ufalme wako utadumu milele na milele.
    Unatumia mamlaka yako kwa haki.
Unapenda kilicho sahihi na kuchukia kilicho na makosa.
    Hivyo Mungu, Mungu wako, amekuchagua wewe,
    na amekupa heshima na furaha zaidi kupita yeyote aliye kama wewe.”(D)

10 Pia Mungu alisema,

“Ee Bwana, mwanzo uliiumba dunia,
    na mikono yako ikaliumba anga.
11 Vitu hivi vitatoweka, lakini wewe utaendelea kuwepo.
    Vyote vitachakaa kama mavazi makuu kuu.
12 Utavikunja hivyo kama koti,
    navyo vitabadilishwa kama mavazi.
Lakini wewe hubadiliki,
    na uhai wako hautafikia mwisho.”(E)

13 Na Mungu hakuwahi kusema haya kwa malaika:

“Ukae mkono wangu wa kuume
    hadi nitakapowaweka adui zako chini ya uwezo wako.”[e](F)

14 Malaika wote ni roho ambao humtumikia Mungu nao hutumwa kuwasaidia wale watakaoupokea wokovu.

Footnotes

  1. 1:3 upande wa kuume Mahali pa heshima na mamlaka (nguvu).
  2. 1:6 ulimwenguni Hii inaweza kumaanisha ulimwengu ambamo Yesu alizaliwa (tazama Lk 2:1-14) au inaweza kuwa na maana ile ile kama katika 2:5, yaani, ulimwengu unaokuja; ambamo Kristo ametajwa kama mfalme baada ya kufufuka kwake (tazama Flp 2:9-11).
  3. 1:6 Basi … yeye Maneno haya yanapatikana katika Kum 32:43 katika tafsiri za asili za Kiyunani na katika magombo ya Kiebrania ya Kumran.
  4. 1:7 upepo Hii pia yaweza kuwa na maana ya “roho”.
  5. 1:13 hadi nitakapowaweka … wako Kwa maana ya kawaida, “hadi nitakapowafanya adui zako mahali pa kukanyagia miguu yako”.