Add parallel Print Page Options

Yesu Ni Mkuu Kuliko Musa

Hivyo, kaka na dada zangu, ninyi mliochaguliwa na Mungu muwe watu wake watakatifu, mfikirieni Yesu. Yeye ndiye tunayeamini kuwa Mungu alimtuma kuja kutuokoa na awe kuhani wetu mkuu. Mungu akamfanya kuhani wetu mkuu, naye akawa mwaminifu kwa Mungu kama Musa alivyokuwa. Naye alifanya kila kitu ambacho Mungu alimtaka akifanye katika nyumba ya Mungu. Mtu anapojenga nyumba, watu watamheshimu mjenzi zaidi kuliko ile nyumba. Ndivyo ilivyo kwa Yesu. Anastahili heshima kubwa kuliko Musa. Kila nyumba huwa imejengwa na mtu fulani, lakini Mungu alijenga kila kitu. Musa alikuwa mwaminifu kama mtumishi katika nyumba yote ya Mungu. Aliwajulisha watu yale ambayo Mungu angeyasema katika siku zijazo. Lakini Kristo ni mwaminifu katika kuitawala nyumba ya Mungu kama Mwana. Nasi tu nyumba ya Mungu, kama tukibaki wajasiri katika tumaini kuu tunalofurahia kusema kuwa tunalo.

Tunapaswa Kuendelea Kumfuata Mungu

Ni kama vile anavyosema Roho Mtakatifu:

“Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu,
    msiifanye migumu mioyo yenu kama hapo zamani,
mlipomgeuka Mungu.
    Hiyo ndiyo siku ulipomjaribu Mungu mle jangwani.
Kwa miaka 40 jangwani, watu wako wakaona niliyoyatenda.
    Lakini walinijaribu na ustahimilivu wangu.
10 Hivyo nikawakasirikia.
    Nikasema, ‘Mawazo yao siku zote hayako sahihi.
    Hawajawahi kamwe kuzielewa njia zangu.’
11 Hivyo nilikasirika na kuweka ahadi:
    ‘Kamwe hawataingia katika sehemu yangu ya pumziko.’”(A)

12 Hivyo ndugu na dada, muwe makini ili asiwepo miongoni mwenu atakayekuwa na mawazo maovu yanayosababisha mashaka mengi ya kuwafanya muache kumfuata Mungu aliye hai. 13 Bali mhimizane ninyi kwa ninyi kila siku, maadamu mna kitu kinachoitwa “leo.”[a] Msaidiane ninyi kwa ninyi ili asiwepo miongoni mwenu atakayedanganywa na dhambi akawa mgumu sana kubadilika. 14 Tunayo heshima ya kushirikishana katika yote aliyo nayo Kristo endapo tutaendelea hadi mwisho kuwa na imani ya uhakika tuliyokuwa nayo mwanzoni. 15 Ndiyo sababu Roho anasema:

“Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu,
    msiifanye migumu mioyo yenu kama hapo zamani,
    wakati mlipogeuka mbali na Mungu.”(B)

16 Ni nani hawa walioisikia sauti ya Mungu na kugeuka kinyume naye? Walikuwa watu wote ambao Musa aliwaongoza kutoka Misri. 17 Na ni kina nani waliokasirikiwa na Mungu kwa miaka 40? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi. Na maiti zao zikaachwa jangwani. 18 Na ni watu gani ambao Mungu alikuwa akisema nao alipotoa ahadi kuwa kamwe wasingeingia mahali penye mapumziko? Alikuwa anazungumza nao ambao hawakumtii. 19 Hivyo tunaona kuwa hawakuruhusiwa kuingia na kupata pumziko la Mungu, kwa sababu hawakuamini.

Footnotes

  1. 3:13 leo Neno hili limechukuliwa kutoka mstari wa 7. Unamaanisha kuwa ni muhimu kufanya hivi sasa, wakati bado kuna fursa.