Add parallel Print Page Options

Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa sababu Mungu mwenyewe alitaka.

Kwa watakatifu wa Mungu walioko katika mji wa Efeso,[b] waamini walio wa Kristo Yesu.

Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.

Baraka za Rohoni katika Kristo

Sifa kwake Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika Kristo, Mungu ametupa baraka zote za rohoni zilizoko mbinguni. Kwa kuwa anatupenda alituchagua katika Kristo kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu ili tuwe watakatifu wake, tusio na hatia tunaoweza kusimama mbele zake. Aliamua tangu mwanzo kutufanya kuwa watoto wake kupitia Yesu Kristo. Hivi ndivyo Mungu alivyotaka na ilimpendeza yeye kufanya hivyo. Sifa kwake Mungu kwa sababu ya neema yake ya ajabu aliyotupa bure kupitia Kristo anayempenda.

Tumewekwa huru katika Kristo kupitia sadaka ya damu yake. Tumesamehewa dhambi kwa sababu ya wingi na ukuu wa neema ya Mungu. Mungu alitupa bure neema hiyo yote, pamoja na hekima na uelewa wote, na ametuwezesha kuujua mpango wake wa siri. Hivi ndivyo Mungu alitaka, na alipanga kuutekeleza kupitia Kristo. 10 Lengo la Mungu lilikuwa kuukamilisha mpango wake muda sahihi utakapofika. Alipanga kuwa vitu vyote vilivyoko mbinguni na duniani viunganishwe pamoja na Kristo kama kichwa.

11 Tulichaguliwa katika Kristo ili tuwe milki ya Mungu. Mungu alikwisha panga ili tuwe watu wake, kwa sababu ndivyo alivyotaka. Na ndiye ambaye hufanya kila kitu kifanyike kulingana na utashi na maamuzi yake. 12 Sisi Wayahudi ndiyo tuliokuwa wa kwanza kutumaini katika Kristo. Na tulichaguliwa ili tuweze kumletea sifa Mungu katika utukufu wake wote. 13 Ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi. Mliusikia ujumbe wa kweli, yaani Habari Njema kuhusu namna ambavyo Mungu anavyowaokoa. Mlipoisikia Habari Njema hiyo, mkamwamini Kristo. Na katika Kristo, Mungu aliwatia alama maalum kwa kuwapa Roho Mtakatifu aliyeahidi. 14 Roho ni malipo ya kwanza yanayothibitisha kuwa Mungu atawapa watu wake kila kitu alichonacho kwa ajili yao. Sisi sote tutaufurahia uhuru kamili uliowekwa tayari kwa ajili ya walio wake. Na hili litamletea Mungu sifa katika utukufu wake wote.

Sala ya Paulo

15-16 Ndiyo sababu daima ninawakumbuka katika maombi yangu na ninamshukuru Mungu kwa ajili yenu. Nimekuwa nikifanya hivi tangu niliposikia kuhusu imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watu wote wa Mungu. 17 Daima ninamwomba Baba aliye mkuu na mwenye utukufu, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ninaomba awape Roho anakayewawezesha kuijua kweli kuhusu Mungu na awasaidie kuzielewa kweli hizo ili mweze kumjua vyema.

18 Ninaomba Mungu afungue mioyo yenu ili mwone kweli yake. Kisha mtalijua tumaini alilochagua kwa ajili yetu. Mtajua kuwa baraka ambazo Mungu amewaahidi watu wake ni nyingi na zimejaa utukufu. 19 Na mtajua kuwa uweza wa Mungu ni mkuu sana kwetu sisi tunaoamini. Ni sawa na nguvu zake kuu 20 alizotumia kumfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumweka akae upande wa kulia wa kiti chake cha enzi huko mbinguni. 21 Amemweka Kristo juu ya watawala wote, mamlaka zote, nguvu zote na wafalme wote. Amempa mamlaka juu ya kila kitu chenye nguvu katika ulimwengu huu na ujao. 22 Mungu alikiweka kila kitu chini ya nguvu za Kristo na kumfanya kuwa kichwa cha kila kitu kwa manufaa ya kanisa. 23 Kanisa ndiyo mwili wa Kristo, yeye ndiye amejaa ndani ya kanisa. Anakikamilisha kila kitu katika kila namna.

Footnotes

  1. 1:1 Kristo Yesu Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32: Lk 23:2. Tazama pia Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno.
  2. 1:1 katika mji wa Efeso Nakala zingine za Kiyunani hayana maneno “katika mji wa Efeso”.