Add parallel Print Page Options

Huduma ya Paulo kwa Wasio Wayahudi

Hivyo, mimi Paulo ni mfungwa kwa sababu ninamtumikia Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi msio Wayahudi. Mnajua hakika ya kuwa Mungu alinipa kazi hii kupitia neema yake ili niwasaidie. Mungu alinionyesha na nikaweza kuujua mpango wake wa siri. Nimekwisha kuandika kiasi fulani juu ya hili. Na ikiwa mtasoma nilichowaandikia, mtajua kuwa ninaielewa siri ya kweli kuhusu Kristo. Watu walioishi zamani hawakuambiwa siri hiyo. Lakini sasa, kupitia Roho, Mungu amewawezesha mitume na manabii wake watakatifu kuijua siri hiyo. Na siri hiyo ni hii: Kwa kuikubali Habari Njema, wale wasio Wayahudi watashiriki pamoja na Wayahudi katika baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake. Wao ni sehemu ya mwili mmoja, na wanashiriki manufaa ya ahadi ambayo Mungu aliitimiza kupitia Kristo Yesu.

Kwa kipawa cha neema ya Mungu, nilifanywa mtumishi wa kuihubiri Habari Njema. Alinipa neema hiyo kwa nguvu zake. Mimi nisiye na umuhimu zaidi miongoni mwa watu wa Mungu. Lakini alinipa kipawa hiki cha kuwahubiri wasio Wayahudi Habari Njema kuhusu utajiri alionao Kristo. Utajiri huu ni mkuu na si rahisi kuuelewa kikamilifu. Pia Mungu alinipa kazi ya kuwaambia watu kuhusu mpango wa siri yake ya kweli. Aliificha siri hii ya kweli ndani yake tangu mwanzo wa nyakati. Ndiye aliyeumba kila kitu. 10 Lengo lake lilikuwa kwamba watawala wote na mamlaka zote zilizo mbinguni zijue njia nyingi anazotumia kuionesha hekima yake. Watalijua hili kwa sababu ya kanisa. 11 Hii inaendana na mpango aliokuwa nao Mungu tangu mwanzo wa nyakati. Alitekeleza mpango wake kupitia Kristo Yesu Bwana wetu. 12 Kwa kuwa tu wake Kristo tunakuja mbele za Mungu tukiwa huru bila woga. Tunaweza kufanya hivi kwa sababu ya uaminifu wake Kristo.[a] 13 Hivyo ninawaomba msikate tamaa kutokana na yale yanayonipata. Mateso yangu ni faida kwenu, na pia ni kwa ajili ya heshima na utukufu wenu.

Upendo wa Kristo

14 Hivyo ninapiga magoti nikimwomba Baba. 15 Ambaye katika yeye kila familia iliyoko mbinguni na duniani inapewa jina. 16 Ninamwomba Baba kwa kadri ya utajiri wa utukufu wake awajaze nguvu za ndani kwa nguvu za Roho wake. 17 Ninaomba kwamba Kristo aishi katika mioyo yenu kwa sababu ya imani yenu. Ninaomba maisha yenu yawe na mizizi mirefu na misingi imara katika upendo. 18 Na ninaomba ili ninyi na watakatifu wote wa Mungu muwe na uwezo wa kuuelewa upana, urefu, kimo na kina cha ukuu wa upendo wa Kristo. 19 Upendo wa Kristo ni mkuu kuliko namna ambavyo mtu yeyote anaweza kujua, lakini ninawaombea ili mweze kuujua. Ndipo mtajazwa kwa kila kitu alichonacho Mungu kwa ajili yenu.

20 Tukiwa na nguvu za Mungu zinazotenda kazi ndani yetu, anaweza kufanya zaidi, zaidi ya kila kitu tunachoweza kuomba au kufikiri. 21 Atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kila wakati, milele na milele. Amina.

Footnotes

  1. 3:12 uaminifu wake Kristo Au “kwa sababu ya imani katika Kristo”.