Add parallel Print Page Options

Ninyi ni watoto wa Mungu wapendwao, hivyo jitahidini kuwa kama yeye. Ishini maisha ya upendo. Wapendeni wengine kama Kristo alivyotupenda sisi. Alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu na kuwa sadaka ya harufu ya manukato mazuri na dhabihu kwa Mungu.

Lakini hakupaswi kuwepo dhambi ya zinaa kati yenu. Hakupaswi kuwepo aina yoyote ya uasherati au matamanio ya zinaa, kwa sababu mambo kama hayo hayastahili kwa watakatifu wa Mungu. Vivyo hivyo, pasiwepo na mazungumzo maovu miongoni mwenu. Msizungumze mambo ya kipuuzi au ya uchafu. Hayo siyo kwa ajili yenu. Bali mnatakiwa kutoa shukrani kwa Mungu. Mnaweza kuwa na uhakika wa hili: Hakuna atakayepata sehemu katika ufalme wa Kristo na wa Mungu kama mtu huyo atakuwa anafanya dhambi ya uzinzi, au akitenda mambo maovu, au kama atakuwa mtu wa kutamani vitu zaidi na zaidi. Mtu mwenye choyo kama huyo atakuwa anamtumikia mungu wa uongo.

Msimruhusu mtu yeyote awadanganye kwa maneno yasiyo ya kweli. Mungu huwakasirikia sana watu wasipomtii kama hivyo. Hivyo msiwe na jambo lolote pamoja nao. Hapo zamani mlijaa giza, lakini sasa mmejaa nuru katika Bwana. Hivyo ishini kama watoto wa nuru. Nuru hii huleta kila aina ya wema, maisha ya haki, na kweli. 10 Jaribuni kutafuta yale yanayompendeza Bwana. 11 Msishiriki katika mambo yanayotendwa na watu wa giza, yasiyosababisha jambo lolote zuri. Badala yake, mwambieni kila mtu jinsi mambo hayo yasivyokuwa sahihi. 12 Hakika, ni aibu hata kuyazungumzia mambo haya wanayoyatenda sirini. 13 Lakini nuru inaonesha wazi jinsi mambo hayo yasivyokuwa sahihi. 14 Ndiyo, kila kitu kinawekwa wazi na nuru. Ndiyo maana tunasema,

“Amka, wewe unayelala!
    Fufuka kutoka kwa wafu,
    na Kristo atakuangazia nuru yake.”

15 Hivyo, muwe makini sana jinsi mnavyoishi. Ishini kwa busara, si kama wajinga. 16 Nasema kwamba jitahidini kutumia kila fursa mliyo nayo katika kutenda mema, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Hivyo msiwe kama wajinga katika maisha yenu, bali mfahamu yale ambayo Bwana anapenda ninyi mfanye. 18 Msilewe kwa mvinyo, ambao utaharibu maisha yenu, bali mjazwe Roho. 19 Mhimizane ninyi kwa ninyi katika zaburi, nyimbo za sifa, na nyimbo zinazoongozwa na Roho. Imbeni na msifuni Bwana katika mioyo yenu. 20 Siku zote mshukuruni Mungu Baba kwa mambo yote katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

Ushauiri Kwa Mke na Mume

21 Mwe radhi kuhudumiana ninyi kwa ninyi kwa kuwa mnamheshimu Kristo.

22 Wake, muwe radhi kuwahudumia waume zenu kama mlivyo radhi kumtumikia Bwana. 23 Mume ni kichwa cha mke wake, kama Kristo alivyo kichwa cha kanisa. Kristo ni Mwokozi wa kanisa, ambalo ni mwili wake. 24 Kanisa hutumika chini ya Kristo, hivyo ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi wake. Mnapaswa kuwa radhi kuwahudumia waume zenu katika kila jambo.

25 Waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa na kuyatoa maisha yake kwa ajili yake. 26 Alikufa ili alitakase kanisa lake. Alitumia ujumbe wa Habari Njema kulisafisha kanisa kwa kuliosha katika maji. 27 Kristo alikufa ili aweze kujiletea mwenyewe kanisa lililo kama bibi harusi katika uzuri wake wote. Alikufa ili kanisa liweze kuwa takatifu na lisilo na dosari, lisilokuwa na uovu au dhambi au chochote kilicho kibaya ndani yake.

28 Na waume wawapende hivyo wake zao. Wawapende wake zao kama vile ni miili yao wenyewe. Mtu anayempenda mkewe anajipenda mwenyewe, 29 kwa sababu kamwe hakuna anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza. Na hivyo ndivyo Kristo anavyolifanyia kanisa 30 kwa sababu sisi sote ni viungo vya mwili wake. 31 Maandiko yanasema, “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake na kuungana na mkewe, nao hao wawili watafanyika mwili mmoja.”(A) 32 Siri hiyo ya kweli ni ya muhimu sana, ninazungumza juu ya Kristo na kanisa. 33 Lakini kila mmoja wenu anapaswa kumpenda mkewe kama anavyojipenda mwenyewe. Na mke anapaswa kumheshimu mume wake.