Add parallel Print Page Options

Watoto na Wazazi Wao

Watoto, watiini wazazi wenu katika namna ambayo Bwana anataka, kwa sababu hili ni jambo sahihi kutenda. Amri husema, “Waheshimu baba yako na mama yako.”(A) Hii ndiyo amri ya kwanza iliyo na ahadi pamoja nayo. Na hii ndiyo ahadi: “Ndipo utakapofanikiwa, na utakuwa na maisha marefu duniani.”(B)

Wababa, msiwakasirishe watoto wenu, lakini waleeni kwa mafunzo na mausia mliyopokea kutoka kwa Bwana.

Watumwa na Bwana

Watumwa, watiini bwana zenu hapa duniani kwa hofu na heshima. Na fanyeni hivi kwa moyo ulio wa kweli, kama mnavyomtii Kristo. Mfanye hivi siyo tu kwa kuwafurahisha bwana zenu wakati wanapowaona, bali wakati wote. Kwa vile ninyi hakika ni watumwa wa Kristo, mfanye kwa mioyo yenu yale Mungu anayotaka. Fanyeni kazi zenu, na mfurahie kuzifanya. Fanyeni kana kwamba mnamtumikia Bwana, siyo tu bwana wa duniani. Kumbukeni kwamba Bwana atampa kila mmoja zawadi kwa kufanya vema. Kila mmoja, mtumwa au aliye huru, atapata zawadi kwa mambo mema aliyotenda.

Mabwana, kwa jinsi hiyo hiyo, muwe wema kwa watumwa wenu. Msiseme mambo ya kuwatisha. Mnajua kuwa yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, na humchukulia kila mmoja sawa.

Vaeni Silaha Zote za Mungu

10 Hapa lipo neno moja la mwisho la ushauri: Mtegemeeni Bwana kwa ajili ya nguvu zenu. Wekeni matumaini yenu katika nguvu zake kuu. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kupigana dhidi ya hila za Shetani. 12 Mapigano yetu si juu ya watu duniani. Tunapigana dhidi ya watawala, mamlaka na nguvu za giza za ulimwengu huu. Tunapigana dhidi ya nguvu za uovu katika ulimwengu wa roho. 13 Ndiyo sababu mnahitaji silaha zote za Mungu. Ili siku ya uovu, mweze kusimama imara. Na mtakapomaliza mapigano yote, mtaendelea kusimama.

14 Hivyo simameni imara mkiwa mmefungwa mkanda wa kweli viunoni mwenu, na katika vifua vyenu mkiwa mmevaa kinga ya maisha ya haki. 15 Miguuni mwenu vaeni Habari Njema za amani ili ziwasaidie msimame imara. 16 Pia itumieni ngao ya imani ambayo itatumika kuizuia mishale inayowaka moto inayotoka kwa yule Mwovu. 17 Upokeeni wokovu wa Mungu kama chapeo yenu. Na chukueni upanga wa Roho, yaani mafundisho ya Mungu. 18 Ombeni katika Roho kila wakati. Ombeni maombi ya aina zote, na ombeni kila mnachohitaji. Ili mfanye hivi ni lazima muwe tayari. Msikate tamaa. Waombeeni watu wa Mungu daima.

19 Pia ombeni kwa ajili yangu ili ninapoongea, Mungu anipe maneno ili niweze kusema siri ya kweli juu ya Habari Njema bila woga. 20 Ninayo kazi ya kuhubiri Habari Njema, na hicho ndicho ninachofanya sasa humu gerezani. Niombeeni ili ninapowahubiri watu Habari Njema, nihubiri kwa ujasiri kama inavyonipasa kuhubiri.

Salamu za Mwisho

21 Namtuma kwenu Tikiko, ndugu yetu mpendwa na msaidizi mwaminifu katika kazi ya Bwana. Atawaeleza kila kitu kinachonipata. Kisha mtaelewa jinsi nilivyo na ninachofanya. 22 Ndiyo sababu namtuma yeye ili awajulishe hali zetu na tuwatie moyo.

23 Namwomba Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo awape amani, upendo na imani ndugu zangu wote mlio huko. 24 Naomba neema ya Mungu iwe pamoja nanyi nyote mnaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa pendo lisilo na mwisho.