Add parallel Print Page Options

Salamu kutoka kwa Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu.[a]

Kwenu ninyi nyote, watakatifu wa Mungu mlioko Filipi, mlio wa Kristo Yesu, wakiwemo wazee[b] na mashemasi wenu.

Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu, Bwana wetu, iwe pamoja nanyi.

Maombi ya Paulo

Ninamshukuru Mungu kila wakati ninapowakumbuka. Kila wakati ninapowaombea ninyi nyote, daima ninawaombea kwa furaha. Ninamshukuru Mungu kwa namna mlivyonisaidia nilipokuwa ninawahubiri watu Habari Njema. Mlinisaidia tangu siku ya kwanza mlipoamini mpaka sasa. Nina uhakika kwamba Mungu, aliyeianzisha kazi njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka itakapomalizika siku ile ambayo Kristo Yesu atakuja tena.

Ninajua niko sahihi kwa namna ile ninayowawazia ninyi nyote kwa sababu mko karibu sana na moyo wangu. Mmechangia sehemu muhimu sana katika neema ya Mungu kwa ajili yangu wakati huu nikiwa gerezani, na wakati wowote ninapoutetea na kuuthibitisha ukweli wa Habari njema. Mungu anajua kwamba ninataka sana kuwaona. Ninawapenda nyote kwa upendo wa Kristo Yesu.

Hili ndiyo ombi langu kwa ajili yenu:

Ya kwamba mkue zaidi na zaidi katika hekima na ufahamu kamili pamoja na upendo; 10 ya kwamba mjue tofauti kati ya kitu kilicho muhimu na kisicho muhimu ili muwe safi msio na lawama, mkiwa tayari kwa siku atakayokuja Kristo; 11 Maisha yenu yajaye matendo mengi mema yanayozalishwa na Kristo Yesu ili kumletea Mungu utukufu na sifa.

Matatizo Ya Paulo Yesaidia Kazi ya Bwana

12 Ndugu zangu, ninataka mjue kwamba yote yaliyonipata yamesaidia katika kusambaza Habari Njema, ingawa ninyi mnaweza kuwa mlitarajia kinyume chake. 13 Walinzi wote wa Kirumi na wengine wote hapa wanafahamu kuwa nimefungwa kwa sababu ninamtumikia Kristo. 14 Kufungwa kwangu gerezani kumesababisha waamini walio wengi hapa kuweka tumaini lao kwa Bwana, na kuhubiri ujumbe wa Mungu kwa ujasiri mwingi pasipo woga.

15 Baadhi ya watu wanahubiri ujumbe wa Kristo kwa sababu wananionea wivu na wanataka watu wawafuate wao badala yangu. Wengine wanahubiri kwa sababu wanataka kusaidia. 16 Wanahubiri kwa sababu ya upendo. Wanafahamu kuwa Mungu ameniweka humu gerezani ili kuitetea Habari Njema. 17 Lakini wengine wanahubiri kuhusu Kristo kwa sababu wanataka kujikweza wenyewe. Chachu yao si safi. Wanafanya hivi kwa kudhani kuwa itanisababishia uchungu mwingi niwapo gerezani. 18 Lakini hiyo haijalishi. Kitu cha muhimu ni kuwa wanawahubiri watu kuhusu Kristo, wakiwa na chachu safi au isiyo safi. Ninafurahi wanafanya hivyo.

Nitaendelea kufurahi, 19 kwa sababu ninajua kwamba kupitia maombi yenu na kipawa cha Roho wa Yesu Kristo mazingira haya magumu hatimaye yataniletea uhuru wangu. 20 Nimejaa tumaini na uhakika, sina sababu yeyote ya kuona haya. Nina uhakika nitaendelea kuwa na ujasiri wa kuhubiri kwa uhuru kama ambavyo nimekuwa. Na Kristo atatukuzwa kwa ninayoyafanya katika mwili wangu, ikiwa nitaishi au nitakufa. 21 Sababu yangu pekee ya kuishi ni kumtumikia Kristo. Kifo kingekuwa bora zaidi. 22 Nikiendelea kuishi hapa ulimwenguni, nitaweza kumfanyia kazi Bwana. Lakini kati ya kufa na kuishi, sijui ningechagua kipi. 23 Ungekuwa uchaguzi mgumu. Ninataka kuyaacha maisha haya ili niwe na Kristo. Hiyo ingekuwa bora zaidi kwangu; 24 hata hivyo, mnanihitaji hapa nikiwa hai. 25 Nina uhakika juu ya hili, hivyo ninajua nitakaa hapa ili niwe nanyi na niwasaidie kukua na kuwa na furaha katika imani yenu. 26 Mtafurahi sana nitakapokuwa hapo pamoja nanyi tena kutokana na kile ambacho Kristo Yesu amefanya ili kunisaidia.

27 Zaidi ya yote, hakikisheni kuwa mnaishi pamoja kama jamii ya watu wa Mungu katika namna inayoiletea heshima Habari Njema kuhusu Kristo. Kisha, ikiwa nitakuja kuwatembelea au ikiwa nitakuwa mbali nanyi na kuyasikia tu mambo kuhusu ninyi, nitajua ya kuwa mmesimama pamoja katika roho moja na kwamba mnafanya kazi pamoja kwa moyo mmoja kama timu moja, katika kuwasaidia wengine kuiamini Habari Njema. 28 Na hamtawaogopa wale walio kinyume nanyi. Imani yenu thabiti itakuwa kama ishara kwao ya kuangamia kwenu. Lakini kwa hakika ni ishara ya wokovu wenu. Na hiki ni kipawa kutoka kwa Mungu. 29 Mungu amewabariki ninyi kwa heshima si ya kumwamini Kristo tu, lakini pia ya kupata mateso kwa ajili yake. 30 Mliyaona magumu mengi niliyokabiliana nayo, na mnasikia kwamba bado nakabiliwa na masumbufu mengi. Ninyi nanyi imewapasa kuyakabili masumbufu hayo pia.

Footnotes

  1. 1:1 Kristo Yesu Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32: Lk 23:2. Tazama pia Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno.
  2. 1:1 wazee Yaani, “Waangalizi”. Tazama Mzee, Wazee katika Orodha ya Maneno.