Add parallel Print Page Options

Yesu Kristo ni wa Muhimu Zaidi

Kwa hiyo sasa, kaka na dada zangu, furahini kwa kuwa ninyi ni wa Bwana. Sisiti kuwaandikia mambo haya haya, kwa sababu yatawasaidia ninyi kuwa imara na salama.

Mjihadhari na mbwa, mjihadhari na wafanyakazi waovu, mjihadhari na watu wanaotaka kumkata kila mtu ambaye hajatahiriwa.[a] Lakini sisi ndiyo wenye tohara[b] ya kweli, tunaomwabudu Mungu kupitia Roho wake. Hatutumaini katika namna tulivyo kwa kuzaliwa au kwa yale tuliyoyakamilisha. Tunajivuna kuwa sisi ni milki ya Kristo Yesu. Hata kama ninaweza kujitumainisha mimi mwenyewe, bado sifanyi hivyo. Ikiwa kuna watu wanadhani wana sababu za kutumaini sifa za kibinadamu, wanapaswa kujua kuwa nina sababu zaidi za kufanya hivyo. Nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa. Mimi ni Myahudi wa kabila la Benjamini. Mimi ni Mwebrania halisi, hata wazazi wangu pia. Nikawa Farisayo na nilitii torati kwa uangalifu sana. Nilikuwa na hamu sana ya kumridhisha Mungu[c] hata nikalitesa kanisa. Kwa usahihi niliitii sheria ya Musa.

Wakati fulani mambo haya yote yalikuwa muhimu kwangu. Lakini kwa sababu ya Kristo, sasa ninayachukulia mambo haya yote kuwa yasiyo na thamani. Na si haya tu, lakini sasa ninaelewa kuwa kila kitu ni hasara tu ukilinganisha na thamani kuu zaidi ya kumjua Kristo Yesu, ambaye sasa ni Bwana wangu. Kwa ajili yake nilipoteza kila kitu. Na ninayachukulia yote kama kinyesi, ili nimpate Kristo. Ninataka niwe wake. Katika Kristo ninayo haki mbele za Mungu, lakini kuwa na haki mbele za Mungu hakuji kwa kuitii sheria, Bali inakuja toka kwa Mungu kupitia imani kwa[d] Kristo. Mungu anatumia imani yangu kwa Kristo kunihesabia haki. 10 Ninachotaka ni kumjua Kristo na nguvu iliyomfufua kutoka kwa wafu. Ninataka kushiriki katika mateso yake na kuwa kama yeye hata katika kifo chake. 11 Kisha mimi mwenyewe naweza kuwa na matumaini kwamba nitafufuliwa kutoka kwa wafu.

Kuyafikia Malengo

12 Sisemi kuwa nimekwisha kupata ujuzi huo au kuifikia shabaha ya mwisho. Lakini bado ninajitahidi kuifikia shabaha kwa kuwa ndivyo ambavyo Kristo Yesu anataka nifanye. Ndiyo sababu alinifanya kuwa wake. 13 Kaka na dada zangu, ninajua ya kuwa bado nina safari ndefu. Lakini kuna kitu kimoja ninachofanya, nacho ni kusahau yaliyopita na kujitahidi kwa kadri ninavyoweza kuyafikia malengo yaliyo mbele yangu. 14 Ninaendelea kupiga mbio kuelekea mwisho wa mashindano ili niweze kushinda tuzo ambayo Mungu ameniitia kutoka mbinguni kwa njia ya Kristo Yesu.

15 Sisi sote tuliokua kiroho tunapaswa kufikiri namna hii. Na ikiwa kuna jambo lolote ambalo hamkubaliani nalo, Mungu atalifunua kwenu. 16 Lakini tunapaswa kuendelea kuifuata kweli tuliyonayo tayari.

17 Kaka na dada zangu, unganeni pamoja na mfuate mfano wangu. Mtazame na mjifunze pia kutoka kwa wale wanaoishi katika namna tuliyoionesha kwenu. 18 Wapo wengi ambao mwenendo wao unaonesha kuwa ni adui za msalaba wa Kristo. Nimekwishawaambia kuhusu hao mara nyingi. Na inanifanya nitokwe machozi ninapowaambia kuhusu watu hao sasa. 19 Wanauendea uharibifu kwa namna wanavyoishi. Wanaabudu tamaa za mili yao kana kwamba hizo ndizo Mungu. Wanatenda mambo ya aibu na wanajivuna kwa kutenda mambo hayo. Wanayawazia mambo ya kidunia tu. 20 Lakini sisi tunatawaliwa na serikali iliyoko mbinguni. Tunamsubiri Mwokozi wetu, Bwana wetu Yesu Kristo atakayekuja kutoka mbinguni. 21 Ataibadilisha miili yetu minyenyekevu na kuifanya iwe kama mwili wake yeye mwenyewe, mwili wenye utukufu. Kristo atafanya hivi kwa nguvu yake inayomwezesha kutawala juu ya vyote.

Footnotes

  1. 3:2 wanaotaka … hajatahiriwa Neno la msingi hapa ni kama “tohara” (tazama Tahiri, kutahiriwa, tohara katika Orodha ya Maneno), Lakini hapa inamaanisha “kukata kiungo cha mwili” au “kukatakata vipande”.
  2. 3:3 tohara Neno hili limetumika hapa kumaanisha hali ya kiroho. Tazama Tahiri, kutahiriwa, tohara katika Orodha ya Maneno.
  3. 3:6 hamu sana ya kumridhisha Mungu Kabla Paulo hajawa mwamini katika Yesu kama Mfalme Aliyeteuliwa na Mungu, alidhani kuwa alikuwa na wajibu kama Farisayo mwema wa kuwapinga Wayahudi waliokuwa wafuasi wa Kristo.
  4. 3:9 imani kwa Au, “uaminifu wa”.