Add parallel Print Page Options

Baraka za Mungu Huja Kwa Imani

Ninyi watu wa Galatia, je mmepoteza fahamu zenu? Nilidhani mmeelewa kwa nini Yesu Kristo alisulubiwa msalabani! Niliwaeleza wazi kabisa jambo hilo, kama vile kuchora na kupaka rangi picha mbele ya macho yenu. Je, kuna mtu yeyote aliyewaloga mkasahau? Niambieni jambo hili moja: Ni jinsi gani mlimpokea Roho? Je, mlimpokea Roho kwa kufuata sheria? Hapana, mlimpokea Roho kwa sababu ya ujumbe kuhusu Yesu unaoleta imani. Mliyaanza maisha yenu mapya pamoja na Roho. Inakuwaje sasa mdhani kuwa mnaweza kukamilishwa na kitu kinyonge kama tohara kilichofanyika katika miili yenu?[a] Basi mmepoteza fahamu zenu! Je, mlipata uzoefu huo mwingi pasipo manufaa yoyote? Sidhani kama hivyo ndivyo! Je, Mungu anawapa ninyi Roho na kutenda miujiza miongoni mwenu kwa kuwa mnaifuata sheria? Hapana sivyo! Mungu anawapa ninyi baraka hizi kwa njia ya ujumbe unaoleta imani katika kumwamini Yesu.

Maandiko yanasema kitu hicho hicho kuhusu Ibrahimu. “Ibrahimu alimwamini Mungu, na Mungu akaikubali imani yake na akamhesabia haki.”(A) Hivyo mnapaswa kuelewa kuwa watoto sahihi wa Ibrahimu ni wale walio na imani. Maandiko yalieleza ambacho kingetokea katika siku zijazo. Maandiko haya yalisema kwamba Mungu angewafanya wasio Wayahudi kuwa wenye haki kwa njia ya imani. Mungu alizisema Habari Njema hizi kwa Ibrahimu kabla haijatokea. Mungu alimwambia Ibrahimu, “Kwa kukubariki wewe, nitawabariki watu wote duniani.”(B) Kwa hiyo, wale wote wanaoweka imani yao kwa Mungu ndiyo wanaobarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwaminifu.

10 Lakini watu wale wanaodhani kuwa kutii sheria ndicho kitu muhimu sana daima hukaa chini ya tishio la laana. Kama vile Maandiko yanavyosema, “Amelaaniwa mtu yeyote atakayeacha kuzishika na kuzitii sheria hizi zote.”(C) 11 Hivyo ni dhahiri kuwa hakuna anayeweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Maandiko yanasema, “Mwenye haki mbele za Mungu ataishi kwa imani.”(D)

12 Sheria haitegemei imani. Hapana, inasema kuwa njia pekee ambayo mtu anaweza kupata uzima kwa njia ya sheria ni kwa kutii amri zake.[b] 13 Sheria inasema kuwa sisi Wayahudi tuko chini ya laana kwa kutokuitii daima. Lakini Kristo alituweka huru kutoka katika laana hiyo. Alikubali kulaaniwa na sheria ili atuokoe. Maandiko yanasema, “Yeyote anayening'inizwa mtini[c] yuko chini ya laana.”(E) 14 Kwa sababu ya yale aliyoyafanya Kristo Yesu, baraka ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu zilitolewa pia kwa wasio Wayahudi. Kristo alikufa ili kwamba kwa kumwamini sisi sote, Wayahudi na wasio Wayahudi, tuweze kumpokea Roho ambaye Mungu aliahidi.

Sheria na Ahadi

15 Ndugu zangu, hebu niwape mfano kutoka maisha ya kila siku: Fikiri kuhusu makubaliano ambayo mtu hukubaliana na mwingine. Baada ya makubaliano hayo kufanywa rasmi, hakuna anayeweza kuongeza chochote kwenye makubaliano hayo na hakuna anayeweza kulipuuza. 16 Mungu aliweka agano kwa Ibrahimu na uzao wake. Maandiko hayasemi, “na kwa ajili ya uzao wenu”. Hilo lingekuwa na maana ya watu wengi. Lakini linasema, “na kwa uzao wako”. Hiyo ina maana ya uzao mmoja tu, na uzao huo ni Kristo. 17 Hii ndiyo maana yangu: Agano ambalo Mungu aliliweka na Ibrahimu lilifanywa rasmi na Mungu muda mrefu kabla ya kuja kwa sheria. Sheria ilikuja miaka 430 baadaye. Hivyo sheria haingeweza kulifuta agano hilo na kuibadili ahadi ya Mungu.

18 Baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake hazipatikani kwa njia ya sheria. Ikiwa ingekuwa hivyo, basi isingekuwa ahadi ya Mungu inayotuletea sisi baraka hiyo. Lakini Mungu aliitoa bure baraka yake kwa Ibrahamu kama agano.

19 Hivyo kwa nini sheria ilitolewa? Sheria ililetwa baadaye kwa sababu ya makosa wanayotenda[d] watu. Lakini sheria ingeendelea kutumika hadi kuja kwa Uzao wa Ibrahimu. Huyu ni Uzao unaotajwa katika agano lililotolewa na Mungu. Lakini sheria ilitolewa kupitia malaika na malaika walimtumia Musa kama mpatanishi wa kuwapa watu sheria. 20 Hivyo mpatanishi anahitajika pale ambapo upande mmoja unapaswa kufikia mapatano. Lakini Mungu ambaye ni mmoja, hakumtumia mpatanishi alipompa ahadi Ibrahimu.[e]

Lengo la Sheria ya Musa

21 Je, hili lamaanisha kwamba sheria hutenda kazi kinyume na ahadi za Mungu? La hasha. Sheria iliyotolewa kamwe haikuwa na uwezo wa kuwaletea watu maisha mapya. Ingekuwa hivyo, basi tungehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. 22 Lakini hilo halikuwa kusudi la sheria. Maandiko yanauweka ulimwengu wote chini ya udhibiti wa dhambi kama aina ya kifungo gerezani. Ili kile ambacho Mungu aliahidi kipokelewe kwa njia ya imani katika[f] Yesu Kristo. Hii hutolewa kwa wale wanaomwamini.

23 Kabla ya aliye mwaminifu kuja, sheria ilituweka sisi kama wafungwa. Hatukuwa huru hadi imani hii inayokuja[g] ilipofunuliwa kwetu. 24 Nina maana kuwa sheria ilikuwa ni mlezi aliyetusimamia[h] tu hadi Kristo alipokuja. Baada ya kuja kwake, tungefanyika kuwa wenye haki mbele za Mungu kwa njia ya imani. 25 Sasa kwa sababu imani hii imekuja, hatuhitaji tena kusimamiwa na kulelewa na sheria.

26 Hii ni kwa sababu ninyi nyote ni mali ya Kristo Yesu na ni watoto wa Mungu kwa njia ya imani. 27 Ndiyo, nyote mlibatizwa ili muunganike na Kristo. Hivyo sasa Kristo anawafunika kabisa kama kubadilisha nguo mpya kabisa. 28 Sasa, ndani ya Kristo haijalishi kama wewe u Myahudi au Myunani, mtumwa au huru, mwanaume au mwanamke. Wote mko sawa katika Kristo Yesu. 29 Na kwa vile ninyi ni wa Kristo, hivyo ninyi wazaliwa wa Ibrahamu. Ninyi ndiyo mtakaopokea baraka zote ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu.

Footnotes

  1. 3:3 kitu kinyonge kama tohara … miili yenu Kwa maana ya kawaida, “katika mwili”. Paulo kila mara ametumia msemo huu akimaanisha udhaifu wa kutenda dhambi wa mwanadamu. Lakini katika barua hii, anatumia msemo huu hasa kwa maana ya tohara (6:12,13), jambo ambalo lilikuwa katika kitovu cha hoja za Paulo dhidi ya wale waliokuwa “wakiwayumbisha” waamini wa Galatia (tazama 1:7).
  2. 3:12 njia pekee … amri zake Tazama Law 18:5.
  3. 3:13 anayening'inizwa mtini Tazama Kum 21:22-23.
  4. 3:19 Sheria ililetwa … wanayotenda Sheria ilitambua kosa (tazama mstari wa 22) na pia ilizuia kosa lisitendeke (tazama mstari wa 23-24).
  5. 3:20 Kwa maana ya kawaida, “Lakini mpatanishi si kwa ajili ya mmoja, lakini Mungu ni mmoja.”
  6. 3:22 imani katika Au “uaminifu wake”.
  7. 3:23 imani hii inayokuja Au “imani ya Yesu”.
  8. 3:24 mlezi aliyetusimamia Ina maana kama ile ya mlezi wa watoto yaani yaya; Kwa Kiyunani namaanisha mtu, kwa kawaida aliyekuwa mtumwa, aliyemsindikiza mvulana mdogo kwenda shule toka nyumbani na kuhakikisha ya kwamba mvulana yule anaenenda vizuri na hapati matatizo.