Kristo alituweka sisi huru ili tuwe na uhuru. Kwa hiyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na minyororo ya utumwa. Sikilizeni! Mimi Paulo nawaambieni kwamba kama mkiku bali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia cho chote. Tena, napenda kumshuhudia kila mmoja wenu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria zote. Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria fahamuni kwamba mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu. Kwa maana, kwa msaada wa Roho wa Mungu, sisi tunangojea kwa matumaini kupata haki kwa njia ya imani. Kwa maana tukiwa ndani ya Kristo, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuleti faida yo yote, bali jambo la msingi ni kuwa na imani inayofanya kazi kwa upendo.

Mlikuwa mkienenda vizuri, sasa ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Kushawishiwa huku hakutokani na yule anayewaita. Hamira kidogo sana inaweza kuchachusha donge zima. 10 Nina hakika katika Bwana kwamba mtakubaliana na msimamo wangu. Huyo anayewasumbueni atapata hukumu anayostahili hata akiwa nani. 11 Lakini ndugu zangu, kama mimi ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini bado nateswa? Ingekuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingekuwa kikwazo tena. 12 Laiti hao wanaowavurugeni wangejikatakata wenyewe!

13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili muwe watu huru. Hata hivyo msitumie uhuru wenu kuendelea kufuata tamaa za mwili, bali tumi kianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 15 Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana, basi jihadhar ini, msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe.

Maisha Ya Kiroho

16 Kwa hiyo nasema, mruhusuni Roho atawale maisha yenu na msitafute kutimiza tamaa za mwili. 17 Kwa maana tamaa za mwili hushindana na Roho; na Roho hushindana na tamaa za mwili. Roho na mwili hupingana, na kwa sababu hiyo ninyi hamwezi kufanya yale mnayotaka. 18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko tena chini ya sheria.

19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, mafarakano, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha waonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama haya, hawataurithi Ufalme wa Mungu. 22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumili vu, wema, fadhili, uaminifu, 23 upole, kiasi. Hakuna sheria inayopinga mambo kama haya.

24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa kuongozwa na Roho wa Mungu, basi tufuate uongozi wake. 26 Tusiwe watu wenye maji vuno, tusichokozane na wala tusioneane wivu. Kuchukuliana Mizigo

Utunzeni Uhuru Wenu

Sasa tuko huru, kwa sababu Kristo alituweka huru ili tuweze kuishi tukiufurahia uhuru huo. Hivyo muwe imara katika uhuru huo. Msimruhusu mtu yeyote awaingize utumwani tena. Sikilizeni! Mimi Paulo nawaambia kwamba ikiwa mtakubali kutahiriwa, basi Kristo hatakuwa na manufaa kwenu. Tena, ninamwonya kila mtu atakayeruhusu atahiriwe, kwamba akifanya hivyo itampasa aifuate sheria yote. Ikiwa utajaribu kufanyika mwenye haki mbele za Mungu kwa njia ya sheria, maisha yako na Kristo yamepotea, kwani umeiacha neema ya Mungu. Ninasema hivi kwa sababu tumaini letu la kufanywa wenye haki mbele za Mungu huja kwa imani. Na kwa nguvu ya Roho kwa njia ya imani, tunangoja kwa utulivu na kwa matumaini yenye ujasiri hukumu ya Mungu inayotuweka huru. Mtu anapokuwa wa Kristo Yesu, vyote kutahiriwa ama kutotahiriwa havina nguvu ya kuleta manufaa yoyote. Lakini kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu imani inatenda kazi kupitia upendo.

Mlikuwa mnapiga mbio vizuri sana. Ni nani aliyewafanya mkaacha kuitii kweli? Hakika hakuwa yule aliyewachagua. Mjihadhari! “Chachu ndogo tu hufanya mkate wote mzima uumuke.”[a] 10 Nimeridhika moyoni mbele za Bwana kuwa hamtafikiri vinginevyo. Mtu yule anayewasumbua atahukumiwa hata angekuwa nani?

11 Kaka na dada zangu, sifundishi kuwa ni lazima mwanaume atahiriwe. Kama nitaendelea kuwafundisha wanaume watahiriwe, kwa nini watu bado wanaendelea kunitesa? Ikiwa bado nafundisha tohara, basi ujumbe wangu kuhusu msalaba hautaendelea kuwa tatizo. 12 Natamani watu hao wanaowasumbua wangeongeza na kuhasi[b] juu ya tohara yao.

13 Ndugu na dada zangu, Mungu aliwaita ili muwe huru. Lakini msiutumie uhuru wenu kama udhuru wa kutimiza yale yote mnayoyapenda, badala yake, msaidiane ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Sheria yote imepewa muhtasari katika amri hii moja tu, “Mpende jirani yako[c] kama unavyojipenda mwenyewe.”(A) 15 Ikiwa mtaendelea kuumizana na kuraruana, muwe waangalifu, vinginevyo mtaangamizana ninyi kwa ninyi.

Roho na Asili ya Kibinadamu

16 Hivyo ninawaambieni, ishini kama Roho anavyowaongoza. Hapo hamtatenda dhambi kutokana na tamaa zenu mbaya. 17 Utu wenu wa dhambi unapenda yale yaliyo kinyume cha Roho, na Roho anataka yale yaliyo kinyume na utu wa dhambi. Hao siku zote hushindana wao kwa wao. Kwa jinsi hiyo ninyi hamko huru kufanya chochote mnachotaka kufanya. 18 Lakini mkimruhusu Roho awaongoze, hamtakuwa chini ya sheria.[d]

19 Mambo mabaya yanayofanywa na mwili wa dhambi ni dhahiri: uasherati, tabia chafu, kufanya mambo yenye kuleta aibu, 20 kuabudu miungu wa uongo, kushiriki mambo ya uchawi, kuwachukia watu, kuanzisha mafarakano, kuwa na wivu, hasira ama choyo, kusababisha mabishano na kujigawa kimakundi na kuwatenga wengine, 21 kujawa na husuda, kulewa pombe, kushiriki karamu zenye ulafi na uasi mwingi na kufanya mambo yanayofanana na hayo. Ninawatahadharisha mapema kama nilivyowatahadharisha mwanzo: Watu wanaofanya mambo hayo hawatahesabiwa kama watoto watakaourithi ufalme wa Mungu. 22 Lakini tunda linalozaliwa na Roho katika maisha ya mtu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, 23 upole, na kiasi. Hakuna sheria juu ya mambo kama haya. 24 Wale walio wa Kristo Yesu wameusulubisha udhaifu wao wa kibinadamu pamoja na tamaa zake za dhambi na zile za mwili. Wameachana na utu wao wa kale wenye hisia za ubinafsi na uliotaka kufanya mambo maovu. 25 Tunayapata maisha yetu mapya kutoka kwa Roho, hivyo tunapaswa kuufuata uongozi wa Roho. 26 Tusijivune na kujisifu juu yetu wenyewe. Hatupaswi kuchokozana kwa mashindano baina yetu ama kuoneana wivu.

Footnotes

  1. 5:9 Chachu … uumuke Mithali inayomaanisha kwamba jambo dogo (kama fundisho dogo lililopotoka) linaweza kuleta tatizo kubwa au mtu mmoja tu anaweza kuleta madhara kwa kundi zima.
  2. 5:12 wangeongeza na kuhasi Paulo anatumia neno lenye maana ya “kukata na kuondoa kabisa” badala ya neno “kutahiriwa”, yenye maana ya “kukata pembeni kuzunguka”, ili kuonesha jinsi alivyokasirishwa na walimu wa uongo wanaowalazimisha wale wasio Wayahudi kutahiriwa.
  3. 5:14 jirani yako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.
  4. 5:18 sheria Yaani, mfumo wa sheria, kama Sheria ya Musa.