Add parallel Print Page Options

Yatoeni Maisha Yenu kwa Mungu

12 Hivyo, dada na kaka zangu, upokeeni wema mkuu ambao Mungu alituonyesha. Itoeni miili yenu[a] kama sadaka hai kwake. Ishini kwa ajili ya Mungu tu na mweze kumpendeza yeye. Mkizingatia kwa makini yale aliyoyatenda, ni sahihi na inapasa kumwabudu Mungu kwa njia hii. Msifikiri au kuenenda kama watu wa ulimwengu huu, bali mruhusuni Mungu aibadilishe namna yenu ya kufikiri ndani yenu. Ndipo mtaweza kuelewa na kuyathibitisha yale Mungu anayotaka kutoka kwenu; yote yaliyo mema, yanayompendeza yeye na yaliyo makamilifu.

Mungu amenipa mimi zawadi maalumu, na ndiyo sababu nina kitu cha kusema na kila mmoja wenu. Msifikiri kuwa ninyi ni bora kuliko jinsi mlivyo kwa asili. Mnapaswa kujiona kadri mlivyo. Mjipime wenyewe jinsi mlivyo kwa imani ambayo Mungu alimpa kila mmoja wetu. Kila mmoja wetu anao mwili mmoja, na mwili huo una viungo vingi. Viungo hivi vyote havifanyi mambo yanayofanana. Kwa jinsi hiyo hiyo, sisi ni watu wengi, lakini kwa sababu ni wa Kristo, sote ni mwili mmoja. Sisi sote ni viungo vya mwili huo, na kila kiungo ni sehemu ya viungo vingine vyote.

Sote tunazo karama tofauti tofauti. Kila karama ilikuja kwa sababu ya neema aliyotupa Mungu. Yule aliye na karama ya unabii anapaswa kuitumia karama hiyo kwa namna inayokubalika kiimani. Aliye na karama ya kuhudumia anapaswa kuhudumia. Aliye na karama ya kufundisha anapaswa kufundisha. Aliye na karama ya kufariji wengine anapaswa kufanya hivyo. Aliye na karama ya kuhudumia mahitaji ya wengine anapaswa kutoa kwa moyo mweupe. Aliye na karama ya kuongoza anapaswa kufanya kwa juhudi katika hiyo. Aliye na karama ya kuonesha wema kwa wengine anapaswa kufanya hivyo kwa furaha.

Upendo wenu unapaswa kuwa halisi. Uchukieni uovu. Fanyeni yaliyo mema tu. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kama wa familia moja. Na jitahidini kuwa wa kwanza katika kumpa heshima kila mmoja baina yenu. 11 Mnapoendelea kumtumikia Bwana, fanyeni kwa juhudi wala msiwe wavivu. Mchangamke juu ya utumishi wenu kwa Mungu.[b] 12 Mfurahi kwa sababu ya tumaini mlilonalo. Mvumilieni mnapokutana na mateso. Ombeni nyakati zote. 13 Washirikishe ulichonacho watu wa Mungu wanaohitaji msaada. Wakaribisheni katika nyumba zenu wale wanaosafiri au wanaohitaji msaada.

14 Watakieni mema wale wanaowafanyia mabaya. Mwombeni Mungu awabariki, na sio kuwalaani. 15 Furahini pamoja na wanaofurahi. Huzunikeni na wanaohuzunika. 16 Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, lakini iweni radhi kuwa rafiki wa wasio na umuhimu kwa wengine. Msijihesabu kuwa wenye akili kuliko wengine wote.

17 Mtu akikukosea, usimlipize ubaya. Mjaribu kufanya lile ambalo kila mtu anaona kuwa ni sahihi. 18 Mjitahidi kadri mwezavyo kuishi kwa amani na kila mtu. 19 Rafiki zangu, msijaribu kumwadhibu yeyote anayewakosea. Msubiri Mungu katika hasira yake awaadhibu. Katika Maandiko Bwana anasema, “Nitawaadhibu wao kwa ajili ya yale waliyofanya.”(A) 20 Badala yake,

“ikiwa una adui wenye njaa,
    wapeni chakula wale.
Ikiwa wana kiu,
    wapeni kinywaji wanywe.
Kwa kufanya hivyo mtawafanya wajisikie aibu.”[c](B)

21 Msiruhusu uovu uwashinde, bali ushindeni uovu kwa kutenda mema.

Footnotes

  1. 12:1 Itoeni miili yenu Paulo anatumia lugha ya Agano la Kale kuhusu sadaka ya mnyama kuonesha wazo la waamini kuyatoa maisha yao kwa Mungu kikamilifu.
  2. 12:11 Mchangamke … Mungu Au “Muwe katika moto wa Roho!”
  3. 12:20 mtawafanya wajisikie aibu Au, “Mtakuwa mnawawekea makaa ya moto vichwani mwao.” Mara nyingi, nyakati za Agano la Kale watu waliweka majivu katika vichwa vyao kuonesha huzuni au masikitiko yao.