Add parallel Print Page Options

Msiwakosoe Wengine

14 Iweni tayari kuwakubali wenye mashaka kuhusu yale ambayo waamini wanaweza kufanya. Tena msibishane nao kuhusu mawazo yao tofauti. Baadhi ya watu wanaamini kuwa wanaweza kula aina yoyote ya chakula,[a] lakini wale walio na mashaka wanakula mboga za majani tu. Wale wanaojua kuwa wanaweza kula chakula cha aina yoyote hawapaswi kujisikia kuwa ni bora kuliko wale wanaokula mboga za majani tu. Na wale wanaokula mboga za majani tu hawapaswi kuamua kuwa wale wanaokula vyakula vyote wanakosea. Mungu amewakubali. Huwezi kuwahukumu watumishi wa mtu mwingine. Hilo linamhusu bwana wao mwenyewe ikiwa watafaulu au watashindwa. Na watakubaliwa, kwa sababu Bwana yuko tayari kuwafanya wafaulu.

Watu wengine wanaweza kuamini kuwa siku moja ni ya muhimu zaidi kuliko nyingine. Na wengine wanaweza kuwa na uhakika kuwa siku zote ziko sawa. Kila mtu anapaswa kujihakikisha juu ya imani yake katika akili zake wenyewe. Wale wanaofikiri kuwa siku moja ni ya muhimu kuliko siku zingine wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Na wale wanaokula vyakula vya aina zote wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Ndiyo, wanamshukuru Mungu kwa ajili ya chakula. Na wale wanaokataa kula vyakula fulani wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Nao pia wanamshukuru Mungu.

Hatuishi au kufa kwa ajili yetu sisi wenyewe tu. Kama tukiishi, tunaishi kwa ajili ya Bwana. Na kama tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Hivyo kuishi au kufa, sisi ni mali ya Bwana. Ndiyo sababu Kristo alikufa na kuishi tena ili awe Bwana juu ya wote waliokufa na wanaoishi.

10 Hivyo kwa nini unamhukumu kaka au dada yako katika familia ya Mungu? Au kwa nini unafikiri kuwa wewe ni bora kuliko wao? Sote tutasimama mbele za Mungu, naye atatuhukumu sisi sote. 11 Ndiyo, Maandiko yanasema,

“‘Hakika kama niishivyo’, asema Bwana,
    ‘kila mtu atapiga magoti mbele zangu,
    na kila mtu atasema kuwa mimi ni Mungu.’”(A)

12 Hivyo kila mmoja wetu ataeleza kuhusu matendo yake mbele za Mungu.

Msisababishe Wengine Wakatenda Dhambi

13 Hivyo tuache kuhukumiana sisi kwa sisi. Tuamue kutokufanya kitu ambacho kitasababisha matatizo kwa kaka au dada au kuathiri imani zao. 14 Najua kuwa hakuna chakula ambacho kwa namna yake chenyewe hakifai kuliwa. Bwana Yesu ndiye aliyenithibitisha juu ya jambo hilo. Lakini ikiwa mtu ataamini kuwa si sahihi kula chakula fulani, basi kwake yeye huyo hiyo haitakuwa sahihi akila chakula hicho.

15 Ikiwa utamuumiza kaka au dada yako kwa sababu ya chakula unachokula, hutakuwa unaifuata njia ya upendo. Kristo alikufa kwa ajili yao. Hivyo usiwaharibu kwa kula kitu wanachofikiri kuwa si sahihi kula. 16 Usiruhusu kile ambacho ni chema kwako kiwe kitu watakachosema ni kiovu. 17 Maisha katika ufalme wa Mungu siyo juu ya kile tunachokula na kunywa. Ufalme wa Mungu ni juu ya njia sahihi ya kuishi, amani na furaha. Vyote hii vinatoka kwa Roho Mtakatifu. 18 Yeyote anayemtumikia Kristo kwa kuishi namna hii anampendeza Mungu na ataheshimiwa na wengine.

19 Hivyo tujitahidi kwa kadri tuwezavyo kufanya kile kinacholeta amani. Tufanye kile kitakachomsaidia kila mtu kujengeka kiimani. 20 Msiruhusu kula vyakula kuiharibu kazi ya Mungu. Vyakula vyote ni sahihi kula, lakini ni makosa kwa yeyote kula kitu kinachomletea shida kaka au dada katika familia ya Mungu. 21 Ni heri kutokula nyama au kunywa divai au kufanya kitu chochote kinachoumiza imani ya kaka au dada yako.

22 Ilindeni imani yenu kuhusu mambo haya kama siri kati yenu na Mungu. Ni baraka kufanya kile unachofikiri ni sahihi bila kujihukumu mwenyewe. 23 Lakini ikiwa unakula kitu bila kuwa na uhakika kuwa ni sahihi, unakosea. Hii ni kwa sababu hukuamini kuwa ni sahihi. Na ukifanya chochote unachoamini kuwa si sahihi, hiyo ni dhambi.

Footnotes

  1. 14:2 aina yoyote ya chakula Sheria ya Kiyahudi ilisema kuwa kulikuwa na vyakula ambavyo Wayahudi wasingeweza kula. Walipofanyika wafuasi wa Kristo, baadhi yao hawakuelewa kuwa sasa wangeweza kula vyakula vyote.