Add parallel Print Page Options

Paulo Anayo Mambo ya Mwisho ya Kusema

16 Napenda mjue kuwa mnaweza kumwamini dada yetu Foebe. Ni mtumishi maalum wa kanisa la kule Kenkrea. Nawaomba mmkaribishe kama yule aliye wa Bwana. Mkaribisheni kwa jinsi ambayo watu wa Mungu wanapaswa. Msaidieni kwa chochote atakachohitaji kutoka kwenu. Yeye amekuwa kiongozi anayeheshimika ambaye amewasaidia watu wengine wengi, pamoja na mimi.

Mpeni salamu Priska na Akila, ambao wametumika pamoja nami kwa ajili ya Kristo Yesu. Waliyahatarisha maisha yao wenyewe ili wayaokoe maisha yangu. Nawashukuru hao, na makanisa yote ya wasio Wayahudi yanawashukuru wao.

Vilevile, fikisheni salamu katika kanisa linalokusanyikia nyumbani mwao.

Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto. Alikuwa mtu wa kwanza kumfuata Kristo kule Asia. Pia msalimieni Mariamu ambaye alifanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili yenu. Pia msalimieni Androniko na Yunia. Hao ni jamaa zangu, na walikuwa gerezani pamoja nami. Walikuwa wafuasi wa Kristo kabla yangu. Nao ni miongoni mwa wale walio muhimu sana waliotumwa na Kristo kuifanya kazi yake.[a]

Msalimuni Ampliato, rafiki yangu mpendwa miongoni mwa watu wa Bwana, na kwa Urbano. Aliyefanya kazi pamoja nasi kwa ajili ya Kristo. Pia fikisheni salamu kwa rafiki yangu mpendwa Stakisi

10 na Apele, aliyejithibitisha kuwa yeye ni mfuasi wa kweli wa Kristo.

Nisalimieni watu wote katika nyumba ya Aristobulo 11 na Herodioni, jamaa yangu.

Wasalimieni nyumba nzima ya Narkiso aliye wake Bwana 12 na Trifaina na Trifosa, wanawake wanaofanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili ya Bwana. Nisalimieni rafiki yangu mpendwa Persisi. Dada huyu amefanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili ya Bwana.

13 Pia msalimieni Rufo, mmoja wa wateule wa Bwana, na mama yake, ambaye amefanyika mama yangu pia.

14 Fikisheni salamu kwa Asinkrito, Flegoni, Hermesi, Patroba, Herma na waamini wote walio pamoja nao.

15 Msalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, Olimpa na watu wote wa Mungu walio pamoja nao.

16 Mpeni kila mmoja ile salamu maalum ya watu wa Mungu.[b]

Makanisa yote yaliyo ya Kristo yanatuma salamu zao kwenu.

17 Kaka na dada zangu, ninataka muwe macho na wale wanaosababisha mabishano na kuumiza imani za watu kwa kufundisha mambo ambayo ni kinyume cha yale mliyojifunza. Mjitenge nao. 18 Watu wa namna hiyo hawamtumikii Kristo Bwana wetu. Wanajifurahisha wenyewe tu. Wanatumia mazungumzo matamu na kusema mambo yanayopendeza ili kuwadanganya wale wasiojua kuhusu uovu. 19 Kila mtu amesikia juu ya utii wenu kwa Bwana, nami nafurahi sana juu ya hilo. Lakini ninataka muwe werevu kuhusu yaliyo mema na kutokujua lolote kuhusu yaliyo maovu.

20 Mungu mwenye kuleta amani atamwangamiza Shetani mapema na kuwapa nguvu juu yake.

Neema ya Bwana wetu Yesu iwe pamoja nanyi.

21 Timotheo, mtumishi pamoja nami, anawatumieni salamu. Pia Lukio, Yasoni na Sosipatro (hawa ni jamaa zangu) wanawatumieni salamu.

22 Mimi Tertio, ninayeandika barua hii kwa ajili ya Paulo. Ninawasalimu kama mmoja aliye wa Bwana.

23 Gayo ameniruhusu na kanisa lote hapa kuitumia nyumba yake. Anawatumia salamu zake. Erasto na kaka yetu Kwarto pia wanatuma salamu. Erasto ndiye mtunza hazina wa mji hapa. 24 [c]

25 Atukuzwe Mungu! Yeye ndiye anayeweza kuzitumia Habari Njema ninazozifundisha kuwaimarisha katika imani. Ni ujumbe ninaowaambia watu kuhusu Yesu Kristo. Ujumbe huo ni siri ya ukweli iliyofichwa kwa karne nyingi sana lakini sasa imefunuliwa. 26 Na kweli hiyo sasa imeonyeshwa kwetu. Ilijulishwa kwa yale ambayo manabii waliandika katika Maandiko, kama Mungu wa milele alivyoagiza. Na sasa imejulikana kwa mataifa yote ili waweze kuamini na kumtii yeye. 27 Utukufu wa milele ni kwa Mungu mwenye hekima pekee kwa njia ya Yesu Kristo. Amina.

Footnotes

  1. 16:7 muhimu sana … kazi yake Kwa maana ya kawaida, “muhimu miongoni (au kwa) mitume”.
  2. 16:16 salamu maalum ya watu wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “busu takatifu”.
  3. 16:24 Nakala zingine za Kiyunani zinaongeza mstari wa 24: “Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amina.” Nakala hizo zinamalizia barua kwa mstari wa 24 na labda zinakuwa hazina mstari 25-27 au huiweka mwishoni mwa sura ya 14.