Add parallel Print Page Options

Mfano wa Ibrahimu

Basi tuseme nini kuhusu Ibrahimu,[a] baba wa watu wetu? Ikiwa Ibrahimu alifanywa kuwa mwenye haki kutokana na matendo yake, hicho ni kitu cha kujivunia! Lakini kama Mungu aonavyo, hakuwa na sababu ya kujivuna. Hili ni wazi kama Maandiko yanavyosema, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na kwa sababu ya kuamini kwake, Mungu alimhesabu kuwa mwenye haki.”[b]

Watu wanapofanya kazi, mshahara wao hautolewi kama zawadi. Ni kitu wanachopata kutokana na kazi waliyofanya. Lakini watu hawawezi kufanya kazi yoyote itakayowafanya wahesabiwe kuwa wenye haki mbele za Mungu. Hivyo ni lazima wamtumaini Yeye. Kisha huikubali imani yao na kuwahesabia haki. Yeye ndiye anayewahesabia haki hata waovu. Daudi alisema mambo hayo hayo alipozungumzia baraka wanazopata watu pale Mungu anapowahesabia haki pasipo kuangalia matendo yao:

“Ni heri kwa watu
    wanaposamehewa kutokana na mabaya waliyotenda,
    dhambi zao zinapofutwa!
Ni heri kwa watu,
    Bwana anapozifuta dhambi zao kutoka katika kumbukumbu yake!”(A)

Je, baraka hii ni kwa ajili ya waliotahiriwa tu? Au pia ni kwa ajili ya wale wasiotahiriwa? Tumekwisha sema ya kwamba Ibrahimu alikubaliwa kuwa ni mwenye haki mbele za Mungu kutokana na imani yake. 10 Sasa katika mazingira gani hili lilitokea? Je, Mungu alimkubali Ibrahimu na kumhesabia haki kabla au baada ya kutahiriwa? Mungu alimkubali kabla ya kutahiriwa kwake. 11 Ibrahimu alitahiriwa baadaye ili kuonesha kuwa Mungu amemkubali kuwa mwenye haki. Tohara yake ilikuwa uthibitisho kwamba Mungu alimhesabia haki kwa njia ya imani hata kabla ya kutahiriwa. Hivyo Ibrahimu ni baba wa wote wanaoamini lakini hawajatahiriwa. Kama Ibrahimu, wao pia wamekubaliwa na Mungu kuwa wenye haki kwa sababu ya imani yao tu. 12 Pia Ibrahimu ni baba wa waliotahiriwa, lakini si kwa sababu ya kutahiriwa kwao. Ni baba yao kwa sababu wao nao wamemwamini Mungu vile vile kama Ibrahimu alivyofanya kabla hajatahiriwa.

Ahadi ya Mungu Hupokelewa kwa Imani

13 Mungu aliweka ahadi kwa Ibrahimu na wazaliwa wake ya kuwapa ulimwengu wote. Lakini kwa nini Mungu aliweka ahadi hii? Haikuwa kwa sababu Ibrahimu aliifuata sheria. Ni kwa sababu aliiweka imani yake katika Mungu na akakubaliwa kuwa mwenye haki. 14 Watu wa Mungu watarithi yote ambayo Mungu alimwahidi Ibrahimu, lakini si kwa sababu wanaifuata sheria. Ikiwa ni lazima tuitii sheria ili tupate kile alichoahidi Mungu, badi imani ya Ibrahimu haina maana yoyote na ahadi ya Mungu haina manufaa. 15 Ninasema hivi kwa sababu sheria ndiyo huleta hasira ya Mungu kwa wale wasioitii. Lakini ikiwa sheria haipo, basi hakuna hatia ya kutoitii.

16 Hivyo watu hupokea ahadi ya Mungu kwa imani. Hili hutokea ili ahadi hiyo iwe kipawa cha bure. Na ikiwa ahadi ni kipawa cha bure, basi watu wote wa Ibrahimu watapata ahadi hiyo. Ahadi hii si tu kwa ajili ya wale wanaoishi chini ya Sheria ya Musa. Bali ni kwa ajili ya wote wanaoishi kwa kuweka imani yao kwa Mungu kama Ibrahimu alivyofanya. Ni baba yetu sote. 17 Kama Maandiko yanavyosema, “Nimekufanya uwe baba wa mataifa mengi.”(B) Ibrahimu aliposikia ahadi hii, aliiweka imani yake kwa Mungu. Mungu ndiye awapaye uhai waliokufa na kwa amri yake huumba kisichokuwepo.

18 Halikuwepo tumaini kwamba Ibrahimu angepata watoto, lakini alimwamini Mungu na akaendelea kutumaini. Na ndiyo sababu akafanyika kuwa baba wa mataifa mengi. Kama Mungu alivyomwambia kuwa, “Utakuwa na wazaliwa wengi.”(C) 19 Ibrahimu alikuwa na umri uliokaribia miaka 100, hivyo alikuwa amevuka umri wa kupata watoto. Pia, Sara hakuweza kuwa na watoto. Ibrahimu alilijua hili vizuri, lakini imani yake kwa Mungu haikudhoofika. 20 Hakutilia shaka kuwa Mungu angetenda kile alichoahidi. Hakuacha kuamini. Kwa hakika, aliendelea kuimarika katika imani yake. Alitukuza Mungu 21 na alikuwa na uhakika kuwa Mungu anaweza kutenda alichoahidi. 22 Ndiyo sababu “Mungu alimkubali kuwa ni mwenye haki”. 23 Maneno haya, “alikubaliwa”, yaliandikwa siyo tu kwa ajili ya Ibrahimu. 24 Pia yaliandikwa kwa ajili yetu. Mungu atatukubali sisi pia kwa sababu tunaamini. Tunamwamini yule aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu. 25 Yesu alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, na akafufuliwa kutoka kifo ili Mungu atuhesabie haki.

Footnotes

  1. 4:1 Basi tuseme nini kuhusu Ibrahimu Au, “Tuseme tumeona nini [katika Sheria] kuhusu Ibrahimu?”
  2. 4:3 Mwa 15:6. Pia katika mstari wa 9 na 22.