Add parallel Print Page Options

Kuhesabiwa Haki na Mungu

Tumehesabiwa haki mbele za Mungu kwa njia ya imani.[a] Hivyo sote[b] tuna amani pamoja na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kupitia imani yetu, Kristo ametufungulia mlango kuingia katika neema ya Mungu, tunayoifurahia sasa. Na tunashangilia sana kwa sababu ya tumaini tulilonalo la kushiriki utukufu wa Mungu. Na tunafurahia matatizo tunayoyapitia. Kwa nini? Kwa sababu tunajua kuwa mateso hutufundisha kuwa jasiri kipindi kigumu. Na ujasiri huu ni uthibitisho kuwa tuko imara. Na uthibitisho huu unatupa tumaini. Na tukiwa na tumaini hili, hatutakata tamaa kamwe. Tunajua hili kwa sababu Mungu ameumimina upendo wake na kuijaza mioyo yetu kupitia Roho Mtakatifu aliyetupa.

Yote haya ni kweli kutokana na aliyoyafanya Kristo. Wakati sahihi ulipotimia, tukiwa hatuwezi kujisaidia wenyewe na tusioonyesha heshima yoyote kwa Mungu, yeye Kristo, alikufa kwa ajili yetu. Ni watu wachache walio tayari kufa ili kuokoa maisha ya mtu mwingine, hata kama mtu huyo ni mwema. Mtu anaweza kuwa radhi kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema sana. Lakini Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa bado ni wenye dhambi, na kwa hili Mungu akatuonyesha jinsi anavyotupenda sana.

Tumehesabiwa haki mbele za Mungu kwa sababu ya sadaka ya damu ya Kristo. Hivyo kwa njia ya Kristo hakika tutaokolewa kutoka katika ghadhabu ya Mungu. 10 Nina maana kuwa tulipokuwa bado adui wa Mungu, Yeye alifanya urafiki nasi kwa njia ya kifo cha Mwanaye. Kutokana na ukweli kwamba sasa tumekuwa marafiki wa Mungu, basi tunaweza kupata uhakika zaidi kwamba Baba atatuokoa kupitia uhai wa Mwanaye. 11 Na si kuokolewa tu, bali pia, hata sasa tunafurahi kwa yale ambayo Mungu ametutendea kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kwa sababu ya Yesu sisi ni marafiki wa Mungu sasa.

Adamu na Kristo

12 Dhambi ilikuja ulimwenguni kwa sababu ya kile alichofanya mtu mmoja. Na dhambi ikaleta kifo. Kwa sababu hiyo ni lazima watu wote wafe, kwa kuwa watu wote wametenda dhambi. 13 Dhambi ilikuwepo ulimwenguni kabla ya Sheria ya Musa. Lakini Mungu hakutunza kumbukumbu ya dhambi ya watu wakati sheria haikuwepo. 14 Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Musa, mauti ilitawala juu ya kila mtu. Adamu alikufa kwa sababu alitenda dhambi kwa kutokutii amri ya Mungu. Lakini hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa njia hiyo hiyo walipaswa kufa.

Hivyo mtu mmoja Adamu anaweza kufananishwa na Kristo, Yeye ambaye angekuja baadaye. 15 Lakini kipawa cha Mungu hakifanani na dhambi ya Adamu. Watu wengi walikufa kwa sababu ya dhambi ya mtu huyo mmoja. Lakini neema waliyopokea watu kutoka kwa Mungu ilikuwa kuu zaidi. Wengi walikipokea kipawa cha Mungu cha uzima kwa neema ya huyu mtu mwingine, Yesu Kristo. 16 Baada ya Adamu kutenda dhambi mara moja, alihukumiwa kuwa na hatia. Lakini kipawa cha Mungu ni tofauti. Kipawa chake cha bure kilikuja baada ya dhambi nyingi, nacho kinawafanya watu wahesabiwe haki mbele za Mungu. 17 Mtu mmoja alitenda dhambi, hivyo kifo kikawatawala watu wote kwa sababu ya huyo mtu mmoja. Lakini sasa watu wengi wanaipokea neema ya Mungu iliyo nyingi sana na karama yake ya ajabu ya kufanyika wenye haki. Hakika watakuwa na uzima wa kweli na kutawala kupitia mtu mmoja, Yesu Kristo.

18 Hivyo dhambi hiyo moja ya Adamu ilileta adhabu ya kifo kwa watu wote. Lakini kwa njia hiyo hiyo, Kristo alifanya kitu chema zaidi kilichowezesha watu kufanyika wenye haki mbele za Mungu. Na hicho huwaletea uzima wa kweli. 19 Mtu mmoja hakumtiii Mungu na wengi wakafanyika wenye dhambi. Lakini kwa namna hiyo hiyo, mtu mmoja alipotii, wengi wamefanyika kuwa wenye haki. 20 Baada ya sheria kuja, zilikuwepo njia nyingi za watu kufanya makosa. Lakini kadri watu walivyozidi kufanya dhambi, ndivyo Mungu alivyomimina zaidi neema yake. 21 Hapo kale dhambi ilitumia kifo kututawala. Lakini sasa neema ya Mungu inatawala juu ya dhambi na kifo kwa sababu ya wema wake wenye uaminifu. Na hii inatuletea maisha ya milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

Footnotes

  1. 5:1 ya imani Au “uaminifu wake” au “uaminifu wa Yesu”.
  2. 5:1 sote Baadhi ya nakala muhimu za Kiyunani zina “hebu sote tuwe”.