Add parallel Print Page Options

Kufa kwa Dhambi Lakini Hai Kwa Ajili ya Mungu

Hivyo, je, mnadhani inatupasa tuendelee kutenda dhambi ili Mungu atupe neema nyingi zaidi na zaidi? Hapana! Utu wetu wa zamani wa dhambi ulikwisha. Umekufa. Je, tutaendeleaje kuishi katika dhambi? Je, mmesahau kwamba sisi sote tulifanyika sehemu ya Kristo Yesu tulipobatizwa? Katika ubatizo wetu tulishiriki katika kifo chake. Hivyo, tulipobatizwa, tulizikwa pamoja na Kristo na kushiriki katika kifo chake. Na kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa nguvu ya ajabu ya Baba, ndivyo nasi tunaweza kuishi maisha mapya sasa.

Kristo alikufa, nasi tumeunganishwa pamoja naye kwa kufa kama yeye alivyokufa. Kwa hiyo tutaunganishwa pamoja naye kwa kufufuka kutoka katika kifo kama yeye alivyofanya. Tunajua kuwa utu wetu wa zamani ulikufa msalabani pamoja naye. Hivyo ndivyo maisha ya utumwa tuliyokuwa nayo yalivyoangamizwa ili tusiendelee kuitumikia dhambi tena. Yeyote aliyekufa amewekwa huru kutoka katika nguvu za dhambi.

Ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunajua kwamba tutaishi pamoja naye pia. Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na tunajua kuwa hawezi kufa tena. Sasa mauti haina nguvu juu yake. 10 Ndiyo, Kristo alipokufa, alikufa ili aishinde nguvu ya dhambi mara moja, na siyo mara nyingine tena. Sasa anao uzima mpya, na uzima wake huo upo kwa nguvu za Mungu. 11 Kwa namna hiyo hiyo, mnapaswa kujiona kama mliokufa kwa dhambi na mlio hai kwa nguvu za Mungu kupitia Kristo Yesu.

12 Mwili mlionao katika uhai wenu wa sasa hapa duniani utakufa. Msiruhusu dhambi iutawale na kuwafanya ninyi kuzitumikia tamaa zake. 13 Msiitoe sehemu ya miili yenu kwa dhambi kwa ajili ya kutumika kutenda maovu. Jitoeni kwa Mungu, kama watu waliokufa lakini walio hai. Toeni sehemu za miili yenu kwa Mungu ili zitumiwe kwa kutenda mema. 14 Dhambi haitakuwa mtawala wenu, kwa sababu hamko chini ya sheria. Sasa mnaishi chini ya neema ya Mungu.

Watumwa wa Haki

15 Hivyo tufanye nini? Je, tutende dhambi kwa sababu tuko chini ya neema na siyo chini ya sheria? Hapana! 16 Hakika mnajua kuwa unakuwa mtumwa wa jambo lolote unaojitoa kulifanya. Chochote au yeyote unayemtii atakuwa bwana wako. Unaweza kufuata dhambi, au kumtii Mungu. Kufuata dhambi kunaleta kifo cha kiroho, lakini kumtii Mungu kunakufanya uhesabiwe na Mungu. 17 Hapo zamani mlikuwa watumwa wa dhambi na dhambi iliwatawala. Lakini ashukuriwe Mungu, mlitii kwa hiyari mafundisho yote aliyowaelekeza. 18 Mliwekwa huru kutoka katika dhambi, na sasa ninyi ni watumwa wa uaminifu wa wema wa Mungu. 19 Natumia dhana hii ya utumwa kutoka katika maisha ya kila siku kwa sababu mnahitaji msaada katika kuielewa kweli hii ya kiroho. Zamani mliitoa sehemu ya miili yenu kuwa watumwa wa mawazo yenu yaliyo machafu na maovu. Matokeo yake mliishi kwa ajili ya dhambi tu. Kwa njia hiyo hiyo, sasa mnapaswa kujitoa wenyewe kama watumwa wa uaminifu wa wema wa Mungu ili mweze kufaa kabisa kwa utumishi kwake.

20 Zamani mlikuwa watumwa wa dhambi, na wala hamkufikiri juu ya kutenda haki. 21 Mlifanya mambo maovu, na sasa mnaaibishwa kwa yale mliyotenda. Je, mambo haya yaliwasaidia? Hapana, yalileta kifo tu. 22 Lakini sasa mko huru dhidi ya dhambi. Mmekuwa watumwa wa Mungu, na mnaishi kwa ajili ya Mungu tu. Hili litawaletea uzima wa milele. 23 Watu wanapotenda dhambi, wanapokea malipo ya dhambi, ambayo ni kifo. Lakini Mungu huwapa watu wake zawadi ya bure, yaani uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.