Add parallel Print Page Options

Kutoka kwa Yakobo mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo.

Kwa makabila Kumi na Mawili[a] ya watu wa Mungu yaliyotawanyika kote ulimwenguni: Salamu!

Imani na Hekima

Kaka na dada zangu, jueni kuwa mtakutana na adha za kila aina. Lakini hilo liwape ninyi sababu ya kuwa na furaha zaidi. Kwa sababu mnajua kuwa imani yenu inapojaribiwa ndipo mnapojifunza kuwa wavumilivu. Na uvumilivu unapaswa kukamilisha kazi yake, ili kwamba muwe watu waliokomaa na wakamilifu msiopungukiwa na kitu cho chote.

Hivyo kama mmoja wenu atapungukiwa na hekima, anapaswa kumwomba Mungu anayewapa watu wote kwa ukarimu, naye atampa hekima. Lakini anapaswa kuwa na imani anapoomba pasipo mashaka yo yote, kwani yule aliye na mashaka ni kama wimbi la baharini, linalosukumwa na upepo na kusukwa sukwa. Mtu wa jinsi hiyo asidhani kuwa anaweza kupokea cho chote kutoka kwa Bwana; yeye ni mwenye mashaka na hufikiria mambo mawili tofauti kwa wakati mmoja.

Utajiri wa Kweli

Ndugu aliye maskini na awe na furaha sana kwamba Mungu amemchukulia kuwa mtu wa maana sana. 10 Na waaminio walio matajiri wawe na furaha sana tu pale Mungu anapowashusha chini. Kwani utajiri wao hautawazuia kufa kama maua ya porini. 11 Jua linapochomoza na kuwa kali zaidi, joto lake hukausha mimea na maua huanguka chini na kupukutika na kupoteza urembo wake. Kwa jinsi hiyo hiyo, mtu tajiri atafifia katika shughuli zake.

Majaribu Hayatoki kwa Mungu

12 Amebarikiwa mtu yule anayestahimili majaribu, maana anapofaulu mitihani atapokea taji yenye uzima ambayo Mungu amewaahidi wale wanaompenda. 13 Yeyote anayejaribiwa hapaswi kusema, “Jaribu hili linatoka kwa Mungu,” kwa sababu maovu hayamjaribu Mungu na hamjaribu mtu yeyote. 14 Bali kila mmoja anajaribiwa na tamaa zake mwenyewe, anapovutwa na kunaswa. 15 Kisha tamaa inapotunga mimba inazaa dhambi, na dhambi ikikomaa kabisa inazaa kifo.

16 Kaka zangu na dada zangu wapendwa msikubali kudanganywa, 17 Kila karama njema na kila tuzo kamilifu hutoka juu; hushuka chini kutoka kwa Baba aliyeumba nuru zote zilizoko mawinguni ambamo kwake yeye hakuna mabadiliko kama vile vivuli vinavyosababishwa na mzunguko wa sayari. 18 Kwa uamuzi wake mwenyewe Mungu alituzaa sisi na kuwa watoto wake kwa njia ya ujumbe wa kweli ili tuwe mazao ya kwanza[b] yenye heshima ya pekee miongoni mwa vyote alivyoviumba.

Kusikiliza na Kutii

19 Kumbukeni hili ndugu zangu wapendwa: Kila mtu awe mwepesi wa kusikia lakini awe mzito wa kusema, na mzito kukasirika, 20 kwa sababu hasira ya mwanadamu haitoi haki inayohitajiwa na Mungu toka kwetu. 21 Hivyo acheni matendo yote machafu na kila uovu uliokaa karibu yenu, na mpokee kwa unyenyekevu mafundisho yaliyopandwa ndani ya mioyo yenu. Neno hilo, lina uwezo wa kuleta wokovu wa roho zenu.

22 Usisikilize tu kile ambacho mafundisho ya Mungu yanakisema; bali fanya yale inayosema! Ikiwa utasikiliza tu, utajidanganya mwenyewe. 23 Kwani kama mtu atasikiliza mafundisho ya Mungu, lakini asitende yanayosemwa, yuko kama mtu anayeutazama uso wake kwenye kioo. 24 Anajiangalia mwenyewe kwa haraka na anapoondoka tu husahau anavyoonekana. 25 Lakini anayetazama kwa makini katika sheria kamilifu ya Mungu, inayowaletea watu uhuru, na akaendelea kufanya hivyo asiwe msikilizaji anayesahau, bali huyatunza mafundisho katika matendo, mtu huyo atakuwa na baraka katika kila analofanya.

Njia Sahihi ya Kumwabudu Mungu

26 Kama kuna anayedhani kuwa ni mshika dini, lakini bado hauzuii ulimi wake anajidanganya mwenyewe. Dini yake mtu huyu haina manufaa. 27 Dini safi na isiyo na lawama mbele za Mungu Baba, inahusisha haya: kuwatunza yatima na wajane katika mazingira mgumu na kujilinda asichafuliwe na ulimwengu.

Footnotes

  1. 1:1 Kumi na Mawili Maelezo ya watu wa Mungu walio wateule wake waliomo katika Agano la Kale. Yakobo anatumia jina hili kwa maana ya Wayahudi ama Wayahudi wanaoamini waliotawanyika kote katika dola ya Rumi.
  2. 1:18 mazao ya kwanza Kwa Waisraeli “mazao ya kwanza” yalikuwa sehemu ya kwanza ya mazao ambayo walileta kwa Kuhani kwa ajili ya kumtolea Mungu. Paulo amelitumia neno hili kwa kanisa. Hapa neno hili limetumika kwa maana ya heshima maalumu ambayo waaminio wanayo mbele ya Mungu tofauti na viumbe vyote. Hawa wanategemea uumbaji mpya na ukombozi ambao wanadamu watakutana nao katika mbingu mpya.