Add parallel Print Page Options

Wapende Watu Wote

Kaka zangu na dada zangu, ninyi ni wenye imani katika Bwana wetu mtukufu Yesu Kristo. Kwa hiyo msiwachukulie baadhi ya watu kuwa wa maana zaidi kuliko wengine. Tuchukulie mtu mmoja anakuja katika mkutano wenu akiwa amevaa pete ya dhahabu ama akiwa amevaa mavazi ya thamani, na mtu maskini aliyevaa mavazi yaliyochakaa na machafu naye akaja ndani. Na tuchukulie kuwa mnaonyesha kumjali zaidi yule mtu aliyevaa mavazi mazuri na kusema, “Wewe keti hapa katika kiti hiki kizuri.” Lakini unamwambia yule mtu maskini, “Wewe simama pale,” au, “Keti chini karibu na miguu yetu.” Je, hiyo haioneshi kwamba mnafikiri miongoni mwenu kuwa baadhi ya watu ni bora kuliko wengine? Mmesimama kama mahakimu wenye maamuzi mabaya?

Sikilizeni kaka na dada zangu wapendwa! Mungu aliwachagua wale walio maskini machoni pa watu kuwa matajiri katika imani. Aliwachagua kuwa warithi wa Ufalme, ambao Mungu aliwaahidi wale wanaompenda? Lakini ninyi mmewadhalilisha walio maskini! Na kwa nini mnawapa heshima kubwa watu walio matajiri? Hawa ndiyo wale ambao daima wanajaribu kuyadhibiti maisha yenu. Si ndiyo hao wanaowapeleka ninyi mahakamani? Je, si ndiyo hao hao wanaolitukana Jina zuri la Bwana wenu?[a]

Kama kweli mnaitunza sheria ya ufalme inayopatikana katika Maandiko, “Mpende jirani yako[b] kama unavyojipenda mwenyewe,”(A) mtakuwa mnafanya vizuri. Lakini kama mtakuwa mnaonyesha upendeleo, mtakuwa mnafanya dhambi na mtahukumiwa kuwa na hatia kama wavunja sheria.

10 Ninasema hivi kwa sababu yeyote anayeitunza Sheria yote, lakini akaikosea hata mmoja tu atakuwa na hatia ya kuihalifu Sheria yote. 11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,”(B) pia ndiye aliyesema, “Usiue.”(C) Hivyo, kama hutazini lakini ukaua utakuwa umevunja Sheria yote ya Mungu.

12 Mseme na kutenda kama watu watakaokuja kuhukumiwa kwa sheria inayoleta uhuru. 13 Kwa kuwa hukumu ya Mungu haitakuwa na huruma kwake yeye ambaye hakuwa na rehema. Lakini rehema huishinda hukumu!

Imani na Kazi Njema

14 Ndugu zangu, ikiwa mtu atasema kuwa anayo imani lakini hafanyi kitu, imani hiyo haina manufaa yoyote. Imani ya jinsi hiyo haiwezi kumwokoa mtu yeyote. 15 Kama ndugu au dada anahitaji mavazi na anapungukiwa chakula cha kila siku, 16 na ukawaambia, “Mungu awe nanyi! Mkahifadhiwe mahala pa joto na mle vizuri!” Hiyo ina manufaa gani kwao? Usipowapa vitu wanavyovihitaji, maneno yako yanakosa maana! 17 Kwa jinsi hiyo hiyo, imani isipokuwa na matendo itakuwa imekufa.

18 Lakini mtu anaweza kuleta hoja kusema, “Watu wengine wanayo imani, na wengine wanayo matendo mema.” Jibu langu litakuwa, huwezi kunionyesha imani yako pasipo kufanya tendo lolote. Lakini mimi nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. 19 Je, mnaamini kwamba kuna Mungu mmoja tu? Vema! Hata mapepo yanaamini na kutetemeka kwa hofu.

20 Wewe mjinga! Je, unahitaji uthibitisho kwamba imani bila matendo haina manufaa? 21 Je, si baba yetu Ibrahimu alihesabiwa haki na Mungu kwa matendo yake alipomtoa sadaka mwanae Isaka juu ya madhabahu? 22 Kwa hakika unaweza kuiona imani hiyo ilifanya kazi pamoja na matendo yake. Kwa hiyo imani yake ilikamilishwa na matendo yake. 23 Ndipo yakatimizwa yale yaliyo kwenye Maandiko kuwa, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na kwa imani hiyo akafanywa kuwa mwenye haki[c] kwa Mungu,”(D) na kwa sababu hiyo akaitwa “Rafiki wa Mungu”.(E) 24 Mnamwona mtu huyo amefanywa kuwa mwenye haki kwa Mungu kwa matendo yake wala siyo kwa imani peke yake.

25 Je, Rahabu[d] yule kahaba si alifanywa kuwa mwenye haki na Mungu kwa matendo aliyofanya, alipowasaidia wale waliokuwa wakipeleleza nchi kwa niaba ya watu wa Mungu. Aliwakaribisha nyumbani mwake na kuwawezesha kutoroka kwa njia nyingine.

26 Hivyo, kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo, imani imekufa ikiwa haina matendo.

Footnotes

  1. 2:7 Bwana wenu Au “ambaye ninyi ni watu wake”.
  2. 2:8 jirani yako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji.
  3. 2:23 akafanywa kuwa mwenye haki Ama alithibitishwa kuwa mwenye haki kama vile tafsiri zingine za walimu wa Biblia wangependa kutumia.
  4. 2:25 Rahabu Simulizi juu ya Rahabu inapatikana katika Yos 2:1-21.