Add parallel Print Page Options

Kuyamudu Mambo Tunayosema

Kaka na dada zangu, msiwe walimu wengi miongoni mwenu. Mnajua kuwa sisi tulio walimu tutahukumiwa zaidi tena kwa umakini kweli.

Ninawatahadharisha kwa sababu sote tunakosa mara kwa mara. Na kama kuna mtu asiyekosa kwa maneno yake, huyo ni mkamilifu, huyo anaweza kuumudu mwili wake wote. Tunawaweka lijamu katika midomo ya farasi, ili waweze kututii sisi. Kwa lijamu hizo tunaweza kuidhibiti miili yao. Au tuchukue meli kama mfano: Hata kama ni kubwa mno na husukumwa na upepo mkali, zinaongozwa kwa usukani mdogo sana na kwenda po pote alikokusudia nahodha kuipeleka. Kwa jinsi hiyo hiyo, ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini unaweza kujivuna kuwa umetenda mambo makubwa sana.

Fikiri jinsi ambavyo msitu mkubwa unaweza kuwashwa moto kwa mwali mdogo tu! Ndiyo, ulimi ni mwali wa moto. Ulimi unawakilisha ulimwengu wa uovu miongoni mwa viungo vya mwili wetu. Ulimi huo huo huuchafua mwili wote, na unaweza kuwasha moto maisha yote ya mtu. Nao unapata moto wake kutoka Jehanamu.

Aina zote za wanyama na ndege, mijusi na viumbe vya baharini wanaweza kufugwa na wanadamu wamekuwa wanawafuga. Lakini hakuna mtu aliyefaulu kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia na umejaa sumu ya kuua. Kwa ulimi huo tunambariki Bwana na Baba, na kwa huo huo tunawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu! 10 Kutoka katika kinywa hicho hicho hutoka baraka na laana. Kaka na dada zangu, haipaswi kuwa hivyo. 11 Chemichemi ya maji haiwezi kutoa maji matamu na maji machungu kutoka katika tundu moja, je inawezekana? 12 Ndugu zangu, je mtini unaweza kuzaa zeituni? Au mzabibu waweza kuzaa tini? Kwa hakika haiwezekani! Wala chemichemi ya maji chumvi haiwezi kutoa maji matamu.

Hekima ya Kweli

13 Nani miongoni mwenu aliye na hekima na ufahamu? Na aoneshe hekima yake kwa mwenendo mzuri, kwa matendo yake yanayofanywa kwa unyenyekevu unaoletwa na hekima. 14 Lakini kama mtakuwa na wivu wenye uchungu na ubinafsi ndani ya mioyo yenu, hamwezi kujivunia hekima yenu; kwamba kujivuna kwenu kungekuwa ni uongo unaoficha ukweli. 15 Hii sio aina ya hekima inayotoka juu mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyotoka kwa Roho wa Mungu bali ni ya kishetani. 16 Kwa sababu pale penye wivu na ubinafsi, basi panakuwepo vurugu na kila aina ya matendo maovu. 17 Lakini hekima inayotoka mbinguni juu kwanza juu ya yote ni safi, kisha ni ya amani ina upole na ina busara. Imejaa rehema na huzaa mavuno ya matendo mema. Haina upendeleo wala unafiki. 18 Wale wenye bidii ya kuleta amani na wanaopanda mbegu zao kwa matendo ya amani, watavuna haki kama mavuno yao.