Add parallel Print Page Options

Onyo kwa Matajiri na Wachoyo

Sikilizeni, ninyi matajiri! Ombolezeni na kulia kwa sauti kwa ajili ya dhiki inayowajia. Utajiri wenu umeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu zenu na fedha vimeliwa na kutu! Hiyo kutu itakuwa ni ushuhuda dhidi yenu, na itaila miili yenu kama kwa moto. Mmejilimbikizia mali kwa ajili yenu katika kizazi hiki cha siku za mwisho! Angalieni! Mmeyazuia malipo ya wafanyakazi waliopalilia mashamba yenu. Sasa wananililia! Na kilio cha hao wanaovuna pia kimeyafikia masikio ya Bwana Aliye na Nguvu.

Mmeishi maisha ya anasa duniani na kujifurahisha na kila kitu mlichotaka. Mmeinenepesha miili yenu, kama wanyama walio tayari kwa siku ya kuchinjwa. Mmehukumu na kuua wale watu wasio na hatia, na ambao hawakupingana nanyi.

Uwe Mstahimilivu

Hivyo kina kaka na kina dada, muwe na subira; hadi kuja kwa mara ya pili kwa Bwana. Kumbukeni kuwa mkulima huyasubiria mazao yake yenye thamani yakue ardhini. Huyangoja kwa subira mpaka yapate mvua za masika na za vuli.[a] Hata ninyi pia mnapaswa kungoja kwa subira. Muwe imara mioyoni mwenu, kwa sababu kuja kwa Bwana mara ya pili kumekaribia. Kaka na dada zangu, msiendelee kunung'unikiana ninyi kwa ninyi, ili msije kuhukumiwa kuwa na hatia. Tazameni! Hakimu anasimama mlangoni akiwa tayari kuingia ndani.

10 Kina kaka na kina dada, fuateni mfano wa manabii waliosema kwa jina la Bwana. Wao walipata mateso mengi mabaya lakini walivumilia. 11 Na tunatoa heshima kubwa sana kwa wale wote waliostahimili mateso. Mmesikia juu ya uvumilivu wa Ayubu,[b] na mnayajua ya kuwa baada ya yote hayo Bwana alimsaidia. Hii basi inaonesha ya kuwa Bwana ni mwenye wingi wa rehema na huruma.

Uwe Makini na Unayosema

12 Juu ya mambo yote kaka zangu na dada zangu, usitumie kiapo unapotoa ahadi, Usiape kwa mbingu wala kwa dunia, ama kwa kitu kingine chochote. “Ndiyo” yenu na iwe “Ndiyo halisi”, na “Hapana” yenu na iwe “Hapana halisi”, ili msije mkaingia katika hukumu ya Mungu.

Nguvu ya Maombi

13 Je, miongoni mwenu kuna aliye na shida? Anapaswa kuomba. Je, yupo yeyote mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. 14 Je, kuna yeyote kwenu aliye mgonjwa? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa kumwombea na kumpaka mafuta katika jina la Bwana. 15 Maombi yanayofanywa kwa imani yatamfanya mgonjwa apone, na Bwana atampa uzima. Kama atakuwa ametenda dhambi, Bwana atamsamehe.

16 Hivyo muungame dhambi ninyi kwa ninyi, na kuombeana ninyi kwa ninyi ili muweze kuponywa. Maombi yanayofanywa na mtu mwenye haki yana nguvu sana na yana matokeo makubwa sana. 17 Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi tulivyo. Aliomba kwamba mvua isinyeshe, na haikunyesha katika ardhi kwa miaka mitatu na nusu. 18 Kisha akaomba tena inyeshe, na anga ikatoa mvua, na ardhi ikatoa mazao.

Kuwasaidia Watu Wanapotenda Dhambi

19 Kaka na dada zangu Ndugu zangu, kama mmoja wenu atapotoka katika kweli, na mwingine akamrejeza, 20 yule aliyemrejeza atambue kuwa yule anayemrejeza mtenda dhambi kutoka katika njia yake mbaya ataiokoa roho ya huyo mtu kutoka katika kifo cha milele na atasababisha dhambi nyingi zisamehewe.

Footnotes

  1. 5:7 mvua za masika na za vuli “Mvua za masika” zilinyesha mwanzoni na “mvua za vuli” zilinyesha mwishoni.
  2. 5:11 uvumilivu wa Ayubu Tazama Kitabu cha Ayubu katika Agano la Kale.