Add parallel Print Page Options

Yesu Aiosha Miguu ya Wafuasi wake

13 Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Yesu alijua kwamba wakati wake wa kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ulikuwa umefika. Daima Yesu aliwapenda watu wa ulimwengu huu waliokuwa wake. Huu ulikuwa wakati alipowaonesha upendo wake mkuu.

Yesu na wafuasi wake walikuwa wakila chakula cha jioni. Ibilisi alikuwa tayari amekwisha kumshawishi Yuda Iskariote kumsaliti Yesu kwa maadui zake. (Yuda alikuwa Mwana wa Simoni.) Baba alikuwa amempa Yesu uwezo juu ya kila kitu. Naye Yesu alilifahamu hili. Alijua pia kuwa yeye alitoka kwa Mungu. Tena alijua kuwa alikuwa anarudi kwa Mungu. Kwa hiyo walipokuwa wakila,[a] Yesu alisimama na kulivua vazi lake. Akachukua taulo na kuifunga kiunoni mwake. Kisha akamimina maji katika bakuli na kuanza kuwaosha miguu[b] wafuasi wake. Kisha akaifuta miguu yao kwa taulo aliolifunga kiunoni mwake.

Akamfikia Simoni Petro, naye Simoni Petro akamwambia, “Bwana, huwezi kuiosha miguu yangu.”

Yesu akamjibu, “Huyaelewi ninayofanya hivi sasa. Lakini utayaelewa baadaye.”

Petro akasema, “Hapana! Huwezi kamwe kuniosha miguu yangu kamwe.”

Yesu akamjibu, “Kama sitakuosha miguu yako, basi hutakuwa miongoni mwa watu wangu.”

Simoni Petro akasema, “Bwana, utakapomaliza miguu, unioshe mikono na kichwa pia!”

10 Yesu akamwambia, “Baada ya mtu kuoga, mwili wake wote huwa safi. Anahitaji tu kunawa miguu. Nanyi mko safi, lakini sio nyote.” 11 Yesu alimjua yule atakayemsaliti mbele ya adui zake. Ndiyo maana alisema, “Sio wote mlio safi.”

12 Yesu alipomaliza kuwaosha miguu wafuasi, alivaa nguo zake na kurudi pale mezani. Akawauliza, “Je, mmelielewa nililowafanyia? 13 Mnaniita mimi ‘Mwalimu’. Tena mnaniita mimi ‘Bwana’. Hayo ni sahihi, kwa sababu hivyo ndivyo nilivyo. 14 Mimi ni Bwana na Mwalimu wenu. Lakini niliwaosha miguu yenu kama mtumishi. Hivyo nanyi mnapaswa kuoshana miguu yenu. 15 Nilifanya hivyo kama mfano. Hivyo nanyi mnapaswa kuhudumiana ninyi kwa ninyi kama nilivyowahudumia. 16 Mniamini mimi, watumishi huwa sio wakubwa kuzidi bwana zao. Wale waliotumwa kufanya jambo fulani sio wakubwa kumzidi yule aliyewatuma. 17 Sasa, mkielewa maana ya yale niliyotenda, Mungu atawabariki mkiyatendea kazi.

18 Nami sizungumzii habari zenu nyote. Nawafahamu watu wale niliowachagua. Lakini Maandiko yanapaswa kutimia kama yanavyosema: ‘Mtu aliyekula chakula pamoja nami amenigeuka.’[c] 19 Ninawaambia hili sasa kabla halijatokea. Hivyo litakapotokea, mtaweza kuamini kuwa MIMI NDIYE.[d] 20 Hakika nawaambieni, yeyote anayempokea mtu yule niliyemtuma ananipokea mimi pia. Na yeyote anayenipokea mimi humpokea pia yeye aliyenituma.”

Yesu Amtaja Atakayemgeuka

(Mt 26:20-25; Mk 14:17-21; Lk 22:21-23)

21 Baada ya Yesu kuyasema mambo haya, alisumbuka sana moyoni. Akasema kwa uwazi, “Mniamini ninaposema kwamba mmoja wenu atanisaliti kwa maadui zangu.”

22 Wafuasi wake wote wakatazamana wao kwa wao. Hawakuelewa kuwa Yesu alikuwa anamzungumzia nani. 23 Mmoja wa wafuasi wake alikaa karibu na Yesu na alikuwa amemwegemea. Huyu alikuwa yule aliyependwa sana na Yesu. 24 Simoni Petro akaonyesha ishara kwa mfuasi huyo amwulize Yesu alikuwa anamzungumzia nani.

25 Yule mfuasi alisogea karibu sana na Yesu na kumwuliza, “Bwana, ni nani huyo?”

26 Yesu akamjibu, “Nitachovya mkate huu kwenye bakuli. Mtu yule nitakayempa mkate huo ndiye mwenyewe.” Kwa hiyo Yesu akachukua kipande cha mkate, akakichovya, na akampa Yuda Iskariote, Mwana wa Simoni. 27 Yuda alipoupokea mkate ule, Shetani akamwingia. Yesu akamwambia Yuda, “Yale unayotaka kuyafanya, yafanye haraka!” 28 Hakuna hata mmoja pale mezani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia Yuda hayo. 29 Kwa vile Yuda ndiye aliyekuwa msimamizi wa fedha[e] zao,[f] baadhi yao walidhani kuwa Yesu alikuwa na maana kuwa Yuda aende kununua vitu ambavyo wangehitaji kwa ajili ya sherehe. Au walidhani kuwa Yesu alitaka Yuda aende na kuwapa maskini cho chote.

30 Yuda akaula mkate aliopewa na Yesu. Kisha akatoka nje mara hiyo hiyo. Wakati huo ulikuwa ni usiku.

Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake

31 Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa ni wakati wa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu. Na Mungu ataupokea utukufu kupitia kwake. 32 Kama Mungu hupokea utukufu kupitia kwake, atampa Mwana Utukufu kupitia kwake yeye mwenyewe. Na hilo litatimia haraka sana.”

33 Yesu akasema, “Watoto wangu, nitakuwa nanyi kwa kipindi kifupi tu kijacho. Nanyi mtanitafuta, lakini nawaambia sasa yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: Kule niendako ninyi hamwezi kuja.”

34 “Nawapa amri mpya: Pendaneni ninyi kwa ninyi. Mnapaswa kupendana kama mimi nilivyowapenda ninyi. 35 Endapo mtapendana ninyi kwa ninyi watu wote watatambua kuwa ninyi ni wafuasi wangu.”

Yesu Asema Petro Atamkana

(Mt 26:31-35; Mk 14:27-31; Lk 22:31-34)

36 Simoni Petro akamwuliza Yesu, “Bwana, unaenda wapi?”

Yesu akajibu, “Kule niendako hamwezi kunifuata sasa. Lakini mtanifuata baadaye.”

37 Petro akauliza, “Bwana, kwa nini nisikufuate sasa? Mimi niko radhi kufa kwa ajili yako!”

38 Yesu akajibu, “Je, ni kweli utayatoa maisha yako kwa ajili yangu? Hakika nakwambia, kabla jogoo hajawika, utasema mara tatu kwamba hunijui mimi.”

Footnotes

  1. 13:4 wakila Wafuasi walikuwa kwenye makochi, wakiwa wameegemea kushoto kwao, na wakitumia mikono ya kulia kufikia vyombo vilivyokuwa mezani, vilivyowekwa mbele ya makochi. Yesu akamimina maji kwenye “jagi” (Wayunani huelezea kuwa hiki kilikuwa chombo kilichotumika maalumu kwa kusudi hilo) na kisha akaenda akimpitia mmoja mmoja nyuma ya kochi, ambako miguu ya wafuasi ilikuwa imenyooshwa.
  2. 13:5 kuwaosha miguu Utaratibu wa kijamii wa karne ya kwanza, kwa sababu watu walivaa viatu vya wazi katika barabara za vumbi jingi. Ulikuwa ni wajibu wa unyenyekevu, kawaida uliofanywa na mtumishi. Pia katika mstari wa 6-14.
  3. 13:18 amenigeuka Amenigeuka kwa hali halisi ina maana ya kuwa “Ameinua kisigino chake dhidi yangu.” Imenukuliwa kutoka Zab 41:9.
  4. 13:19 MIMI NDIYE Hili ni kama Jina la Mungu lililotumiwa katika Agano la Kale. Tazama Isa 41:4; 43:10; Kut 3:14. Hata hivyo, Inaweza kuwa na maana ya “Mimi Ndiye”, maana yake “Mimi Ndiye Masihi”. Pia katika mstari wa 28,58.
  5. 13:29 msimamizi wa fedha Mtunzaji wa fedha. Wafuasi walikuwa kama kundi moja walipokea michango na kuitunza pamoja kwa ajili ya mahitaji yao na kwa kuwasaidia maskini ila mmoja wao alisimamia sanduku la fedha.
  6. 13:29 zao Kiongozi wa mambo ya fedha ni sawa na kusema kwamba yeye alikuwa anatunza mfuko wa fedha za wafuasi walizopata hata kwa kuchangiwa na watu wengine.