Add parallel Print Page Options

Arusi Katika Mji wa Kana

Siku tatu baadaye kulikuwa na arusi katika mji wa Kana huko Galilaya, mama yake Yesu naye pia alikuwapo. Yesu na wafuasi wake nao walialikwa. Hapo arusini divai ilipungua, mama yake Yesu akamwambia mwanaye, “Hawana divai ya kutosha.”

Yesu akajibu, “Mama, kwa nini unaniambia mambo hayo? Wakati sahihi kwangu kufanya kazi haujafika bado.”

Mama yake akawaambia wahudumu wa arusi, “Fanyeni lo lote lile atakalowaambia.”

Mahali hapo ilikuwepo mitungi mikubwa sita iliyotengenezwa kwa mawe iliyotumiwa na Wayahudi katika desturi yao maalumu ya kunawa.[a] Kila mtungi mmoja ulikuwa na ujazo wa lita 80 au 120.[b]

Yesu akawaambia wale wahudumu, “Ijazeni maji hiyo mitungi.” Nao wakaijaza maji mpaka juu.

Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kiasi na mumpelekee mkuu wa sherehe.” Nao wakafanya kama walivyoambiwa. Mkuu wa sherehe akayaonja yale maji, ambayo tayari yamegeuka na kuwa divai. Naye hakujua wapi ilikotoka hiyo divai, bali wahudumu walioleta yale maji wao walijua. Akamwita bwana arusi 10 na kumwambia, “Watu wanapoandaa huleta kwanza divai iliyo bora zaidi. Baadaye, wageni wanapokuwa wametosheka, huleta divai iliyo na ubora pungufu. Lakini wewe umeandaa divai bora zaidi hadi sasa.”

11 Ishara hii ilikuwa ya kwanza aliyoifanya Yesu katika mji wa Kana ya Galilaya. Kwa hili Yesu alionesha ukuu wake wa kimungu, na wafuasi wake wakamwamini.

12 Kisha Yesu akashuka kwenda katika mji wa Kapernaumu. Mama yake, ndugu zake, na wafuasi wake nao walienda pamoja naye. Wote wakakaa huko kwa siku chache.

Yesu Asafisha Eneo la Hekalu

(Mt 21:12-13; Mk 11:15-17; Lk 19:45-46)

13 Kipindi hicho wakati wa kusherehekea Pasaka ya Wayahudi ulikaribia, hivyo ikampasa Yesu kwenda Yerusalemu. 14 Katika eneo la Hekalu aliwaona watu wakiuza ng'ombe, mbuzi na njiwa. Aliwaona wengine wakikalia meza na kufanya biashara ya kubadili fedha za watu. 15 Yesu akatengeneza kiboko kwa kutumia vipande vya kamba. Kisha akawafukuza watu wote, kondoo na ng'ombe watoke katika eneo la Hekalu. Akazipindua meza za wafanya biashara wa kubadilisha fedha na kuzitawanya fedha zao. 16 Baada ya hapo akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, “Viondoeni humu vitu hivi! Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa kununua na kuuza!”

17 Haya yaliwafanya wafuasi wake kukumbuka maneno yaliyoandikwa kwenye Maandiko: “Upendo wangu mkuu kwa Hekalu lako utaniangamiza.”(A)

18 Baadhi ya Wayahudi wakamwambia Yesu, “Tuoneshe muujiza mmoja kama ishara kutoka kwa Mungu. Thibitisha kwamba unayo haki ya kufanya mambo haya.”

19 Yesu akajibu, “Bomoeni hekalu hili nami nitalijenga tena kwa muda wa siku tatu.” 20 Wakajibu, “Watu walifanya kazi kwa miaka 46 kulijenga Hekalu hili! Je, ni kweli unaamini kwamba unaweza kulijenga tena kwa siku tatu?”

21 Lakini Yesu aliposema “hekalu hili”, alikuwa anazungumzia mwili wake. 22 Baada ya kufufuliwa kutoka katika wafu, wafuasi wake wakakumbuka kwamba alikuwa ameyasema hayo. Hivyo wakayaamini Maandiko, na pia wakayaamini yale aliyoyasema Yesu.

23 Yesu alikuwa Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. Watu wengi wakamwamini kwa sababu waliona ishara na miujiza alioitenda. 24 Lakini Yesu hakuwaamini wao, kwa sababu alijua jinsi watu wote wanavyofikiri. 25 Hakuhitaji mtu yeyote amwambie jinsi mtu fulani alivyo. Kwa sababu alikwishamjua tayari.

Footnotes

  1. 2:6 desturi yao maalumu ya kunawa Wayahudi walikuwa na sheria za kidini za kunawa maji kwa namna maalumu kabla ya kula, kabla ya kufanya ibada katika Hekalu, na pia nyakati zingine maalumu.
  2. 2:6 lita 80 au 120 Kwa maana ya kawaida, “metretas 2 au 3”.