Add parallel Print Page Options

Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000

(Mt 14:13-21; Mk 6:30-44; Lk 9:10-17)

Baadaye, Yesu akavuka Ziwa Galilaya (ambalo pia linaitwa Ziwa Tiberia). Umati mkubwa wa watu ukamfuata kwa sababu waliona ishara za miujiza alizofanya kwa kuponya wagonjwa. Yesu akapanda mlimani na kukaa pale pamoja na wafuasi wake. Siku hizo sherehe ya Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

Yesu akainua macho yake na kuuona umati wa watu ukija kwake. Akamwambia Filipo, “Tunaweza kununua wapi mikate ya kuwatosha watu hawa wote?” Alimwuliza Filipo swali hili ili kumjaribu. Yesu alikwishajua kile alichopanga kufanya.

Filipo akajibu, “Wote tunapaswa kufanya kazi kwa mwezi mmoja ili kununua mikate ya kutosha na kumpa kila mmoja aliyepo angalau kipande kidogo.”

Mfuasi mwingine aliyekuwepo alikuwa Andrea, ndugu yake Simoni Petro. Andrea akasema, “Yupo hapa kijana mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wadogo wawili. Lakini hiyo haitoshi kwa umati huu wa watu.”

10 Yesu akasema, “Mwambieni kila mtu akae chini.” Sehemu hiyo ilikuwa yenye nyasi nyingi, na wanaume wapatao 5,000 walikaa hapo. 11 Yesu akaichukua ile mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya hiyo. Kisha akawapa watu waliokuwa wakisubiri kula. Alifanya vivyo hivyo kwa samaki. Akawapa watu kadiri walivyohitaji.

12 Wote hao wakawa na chakula cha kutosha. Walipomaliza kula, Yesu akawaambia wafuasi wake, “Kusanyeni vipande vya samaki vilivyobaki na mikate ambayo haikuliwa. Msipoteze chochote.” 13 Hivyo wakakusanya vipande vilivyobaki wakajaza vikapu 12 vikubwa vya mikate ya ngano iliyowabakia wale waliokula. Watu walikuwa wameanza kula wakiwa na vipande vitano tu vya mikate ya ngano.

14 Watu waliiona ishara hii aliyoifanya Yesu na kusema, “Huyu atakuwa ndiye yule Nabii[a] anayekuja ulimwenguni!”

15 Yesu akajua kwamba watu walipanga kuja kumchukua na kumfanya kuwa mfalme wao baada ya kuona muujiza alioufanya. Hivyo akaondoka na kwenda milimani peke yake.

Yesu Atembea Juu ya Maji

(Mt 14:22-27; Mk 6:45-52)

16 Jioni ile wafuasi wake wakashuka kwenda ziwani. 17 Ilikuwa giza sasa, wakati huo Yesu hakuwa pamoja na wafuasi wake. Wakapanda kwenye mashua na kuanza safari kuvuka ziwa kwenda Kapernaumu. 18 Upepo ulikuwa unavuma kwa nguvu sana. Mawimbi ziwani yakawa makubwa. 19 Wakaiendesha mashua kiasi cha kilomita tano au sita. Kisha wakamwona Yesu. Yeye alikuwa anatembea juu ya maji, akiifuata mashua. Nao wakaogopa. 20 Lakini Yesu akawaambia, “Msiogope. Ni mimi.” 21 Baada ya kusema hivyo, wakamkaribisha kwenye mashua. Kisha mashua ikafika ufukweni katika sehemu waliyotaka kwenda.

Watu Wamtafuta Yesu

22 Siku iliyofuata watu wengi walikuwa wamekaa upande mwingine wa ziwa. Nao walijua kuwa Yesu hakwenda pamoja na wafuasi wake kwenye mashua. Kwani walifahamu kuwa wafuasi wake waliondoka na mashua peke yao. Walijua pia kuwa ile ilikuwa ni mashua pekee iliyokuwepo pale. 23 Lakini baadaye mashua zingine kutoka Tiberia zilifika na kusimama karibu na mahali walipokula chakula jana yake. Hapo ni mahali pale walipokula mikate baada ya Yesu kushukuru. 24 Watu wakaona kuwa Yesu na wafuasi wake hawakuwa hapo. Hivyo wakaingia katika mashua zao na kuelekea Kapernaumu kumtafuta Yesu.

Yesu, Mkate wa Uzima

25 Watu wakamwona Yesu akiwa upande mwingine wa ziwa. Wakamwuliza, “Mwalimu, ulifika huku lini?”

26 Akawajibu, “Kwa nini mnanitafuta? Ni kwa sababu mliona ishara na miujiza iliyotendeka? Ukweli ni kwamba, mnanitafuta kwa vile mlikula ile mikate mkashiba. 27 Lakini chakula cha kidunia kinaharibika na hakidumu. Ninyi msifanye kazi ili kupata chakula cha aina hiyo kinachoharibika. Isipokuwa fanyeni kazi ili mpate chakula kinachodumu na kinachowapa uzima wa milele. Mwana wa Adamu atawapa hicho chakula. Yeye ndiye pekee aliyethibitishwa na Mungu Baba kuwapa.”

28 Watu wakamwuliza Yesu, “Mungu anatutaka tufanye nini?”

29 Yesu akajibu, “Kazi anayoitaka Mungu muifanye ni hii: kumwamini yule aliyemtuma.”

30 Hivyo watu wakamwuliza, “Ni ishara gani utakayotufanyia? Ili nasi tutakapokuona unafanya ishara basi tukuamini? Je, utafanya nini? 31 Baba zetu walipewa mana kula jangwani. Kama Maandiko yanavyosema, ‘Aliwapa mkate wa kula kutoka mbinguni.’”(A)

32 Yesu akasema, “Naweza kuwahakikishia kwamba Musa siye aliyewapa watu wenu mkate kutoka mbinguni. Bali Baba yangu huwapa ninyi mkate halisi unaotoka mbinguni. 33 Mkate wa Mungu ni ule unaoshuka kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”

34 Watu wakasema, “Bwana, kuanzia sasa na kuendelea tupe mkate wa aina hiyo.”

35 Kisha Yesu akasema, “Mimi ndiye mkate unaoleta uzima. Hakuna ajaye kwangu atakayehisi njaa. Hakuna anayeniamini atakayepata kiu kamwe. 36 Nilikwisha kuwaambia mapema kuwa mmeona kile ambacho naweza kufanya,[b] lakini bado hamuniamini. 37 Vyote anavyonipa Baba vitakuja kwangu hata hivyo yeyote Yule atakayekuja kwangu sitamkataa kabisa. Nami kwa hakika daima nitawapokea. 38 Nilishuka kutoka mbinguni kuja kufanya yale Mungu anayopenda, siyo ninayoyapenda mimi. 39 Nami sitampoteza hata mmoja wa wale alionipa Mungu. Bali nataka nimfufue katika siku ya mwisho. Haya ndiyo Baba yangu anayoyataka. 40 Kila anayemtazama Mwana na kumwamini anao uzima wa milele. Nami nitamfufua katika siku ya mwisho. Hayo ndiyo anayoyataka Baba yangu.”

41 Baadhi ya Wayahudi walianza kumlalamikia Yesu kwa vile alisema, “Mimi ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni.” 42 Wakasema, “Huyu ni Yesu. Tunawajua baba na mama yake. Yeye ni mtoto wa Yusufu. Anawezaje kusema, ‘Nilishuka kutoka mbinguni’?”

43 Lakini Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unika miongoni mwenu. 44 Baba ndiye aliyenituma, na ndiye anayewaleta watu kwangu. Nami nitawafufua siku ya mwisho. Hakuna mtu anayeweza kuja kwangu asipoletwa na Baba yangu. 45 Hii iliandikwa katika vitabu vya manabii: ‘Mungu atawafundisha wote.’(B) Watu humsikiliza Baba na hujifunza kutoka kwake. Hao ndiyo wanaokuja kwangu. 46 Sina maana kwamba yupo yeyote aliyemwona Baba. Yule pekee aliyekwisha kumwona Baba ni yule aliyetoka kwa Mungu. Huyo amemwona Baba.

47 Hakika nawaambieni kila anayeamini anao uzima wa milele. 48 Maana mimi ni mkate unaoleta uzima. 49 Baba zenu walikula mana waliyopewa na Mungu kule jangwani, lakini haikuwazuia kufa. 50 Hapa upo mkate unaotoka mbinguni. Yeyote anayekula mkate huu hatakufa kamwe. 51 Mimi ni mkate ulio hai ulioshuka kutoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu. Nitautoa mwili wangu ili watu wa ulimwengu huu waweze kupata uzima.”

52 Kisha Wayahudi hawa wakaanza kubishana wao kwa wao. Wakasema, “Yawezekanaje mtu huyu akatupa mwili wake tuule?”

53 Yesu akasema, “Mniamini ninaposema kwamba mnapaswa kuula mwili wa Mwana wa Adamu, na mnapaswa kuinywa damu yake. Msipofanya hivyo, hamtakuwa na uzima wa kweli. 54 Wale wanaoula mwili wangu na kuinywa damu yangu wanao uzima wa milele. Nitawafufua siku ya mwisho. 55 Mwili wangu ni chakula halisi, na damu yangu ni kinywaji halisi. 56 Wale waulao[c] mwili wangu na kuinywa damu yangu wanaishi ndani yangu, nami naishi ndani yao.

57 Baba alinituma. Yeye anaishi, nami naishi kwa sababu yake. Hivyo kila anayenila mimi ataishi kwa sababu yangu. 58 Mimi siyo kama ule mkate walioula baba zenu. Wao waliula mkate huo, lakini bado walikufa baadaye. Mimi ni mkate uliotoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele.”

59 Yesu aliyasema haya yote alipokuwa akifundisha kwenye Sinagogi katika mji wa Kapernaumu.

Wafuasi Wengi Wamwacha Yesu

60 Wafuasi wa Yesu waliposikia haya, wengi wao wakasema, “Fundisho hili ni gumu sana. Nani awezaye kulipokea?”

61 Yesu alikwishatambua kuwa wafuasi wake walikuwa wanalalamika juu ya hili. Hivyo akasema, “Je, fundisho hili ni tatizo kwenu? 62 Ikiwa ni hivyo mtafikiri nini mtakapomwona Mwana wa Adamu akipanda kurudi kule alikotoka? 63 Roho ndiye anayeleta uzima. Sio mwili. Lakini maneno niliyowaambia yanatoka kwa Roho, hivyo yanaleta uzima.” 64 Lakini baadhi yenu hamuamini. (Yesu aliwafahamu wale ambao hawakuamini. Alijua haya tangu mwanzo. Na alimjua yule ambaye angemsaliti kwa adui zake.) 65 Yesu akasema, “Ndiyo maana nilisema, ‘Hayupo hata mmoja ambaye anaweza kuja kwangu pasipo kusaidiwa na baba.’”

66 Baada ya Yesu kusema mambo hayo, wafuasi wake wengi wakamkimbia na wakaacha kumfuata.

67 Yesu akawauliza wale mitume kumi na wawili, “Nanyi pia mnataka kuondoka?”

68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutaenda wapi? Wewe unayo maneno yanayoleta uzima wa milele. 69 Sisi tunakuamini wewe. Tunafahamu kwamba wewe ndiye Yule Mtakatifu atokaye kwa Mungu.”

70 Kisha Yesu akajibu, “Niliwachagua nyote kumi na wawili. Lakini mmoja wenu ni Ibilisi.” 71 Alikuwa anazungumza juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Yuda alikuwa miongoni mwa mitume kumi na wawili, lakini baadaye angemkabidhi Yesu kwa adui zake.

Footnotes

  1. 6:14 Nabii Huenda walikuwa na maana nabii ambaye Mungu, alimwambia Musa ya kwamba atamtuma. Tazama Kum 18:15-19.
  2. 6:36 kile ambacho naweza kufanya Au “mimi ninachoweza kufanya”, ambayo ipo katika nakala nyingi za Kiyunani, lakini haipo katika nakala mbili kati ya zile bora zaidi.
  3. 6:56 waulao Kukaa kula Maana yake, “kutafuna kwa kelele” au “kutafuna kwa nguvu”. Ni neno la kufurahia kula, kunywa na ushirika baada ya mlo mkuu. Sehemu hii ya mlo pia ilijulikana kama “meza ya pili”.