Add parallel Print Page Options

Usiku ule Yesu akaenda katika mlima wa Mizeituni. Mapema asubuhi akarudi katika eneo la Hekalu. Watu wengi wakaja kwake, naye akakaa pamoja nao na kuwafundisha.

Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta kwake mwanamke waliyemfumania akizini. Wakamlazimisha asimame mbele ya watu. Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, mwanamke huyu amekamatwa akifanya zinaa. Sheria ya Musa inatuagiza kumponda kwa mawe mpaka afe mwanamke wa jinsi hiyo. Je, Unasema tufanye nini?”

Watu hao waliyasema haya ili kumtega Yesu. Walitaka kumkamata akisema mambo tofauti ili wapate mashtaka ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama chini na kuanza kuandika kwenye udongo kwa kidole chake. Viongozi wa Kiyahudi waliendelea kumuuliza swali lao hilo. Naye akainuka na kusema, “Yeyote hapa ambaye hajawahi kutenda dhambi awe wa kwanza kumponda jiwe mwanamke huyu.” Kisha Yesu akainama chini tena na kuendelea kuandika katika udongo.

Waliposikia hayo, wale watu walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine. Wanaume wazee wakitangulia kwanza, na kisha wengine wakifuata. Wakamwacha Yesu peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake. 10 Kisha Yesu akainua uso wake tena na kumwambia, “Wameenda wapi hao wote? Je, hakuna aliyekuhukumu kuwa una hatia?” 11 Mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja aliyenihukumu, Bwana.”[a]

Kisha Yesu akasema, “Hata mimi sikuhukumu. Unaweza kwenda sasa, lakini usifanye dhambi tena.”

Yesu ni Nuru ya Ulimwengu

12 Baadaye Yesu akazungumza tena na watu. Akasema, “Mimi ndiye nuru ya ulimwengu. Yeyote atakayenifuata mimi hataishi gizani kamwe. Atakuwa na nuru inayoleta uzima.”

13 Lakini Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Unapojishuhudia mwenyewe, unakuwa ni wewe peke yako unayethibitisha kuwa mambo haya ni kweli. Hivyo hatuwezi kuyaamini unayosema.”

14 Yesu akajibu, “Ndiyo, nasema mambo haya juu yangu mwenyewe. Lakini watu wanaweza kuamini ninayosema, kwa sababu mimi najua nilikotoka. Pia najua ninakoenda. Lakini ninyi hamjui mimi ninakotoka wala ninakoenda. 15 Mnanihukumu kama watu wanavyowahukumu wengine. Mimi simhukumu mtu yeyote. 16 Lakini ikiwa ninahukumu, basi hukumu yangu ni ya kweli, kwa sababu ninapohukumu sifanyi hivyo peke yangu. Baba aliyenituma yuko pamoja nami. 17 Sheria yenu inasema kwamba mashahidi wawili wakilisema jambo hilo hilo, basi mnapaswa kukubali wanayosema. 18 Mimi shahidi ninayeshuhudia mambo yangu mwenyewe. Na Baba yangu aliyenituma ndiye shahidi wangu mwingine.”

19 Watu wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?”

Yesu akajibu, “Hamnijui mimi wala Baba yangu hamumjui. Lakini mngenijua mimi, mngemjua Baba pia.”

20 Yesu alisema maneno haya alipokuwa anafundisha katika eneo la Hekalu, karibu na chumba ambamo sadaka za Hekaluni zilitunzwa. Hata hivyo hakuna hata mmoja aliyemkamata, kwa sababu wakati sahihi wa kufanya hivyo ulikuwa bado haujafika.

Baadhi ya Wayahudi Hawamwelewi Yesu

21 Kwa mara nyingine, Yesu akawaambia watu, “Mimi nitawaacha. Nanyi mtanitafuta, lakini pamoja na hayo mtakufa katika dhambi zenu. Kwani hamuwezi kuja kule niendako.”

22 Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakaulizana wenyewe, “Je, atajiua mwenyewe? Je, ndiyo maana alisema, ‘Hamuwezi kuja kule niendako’?”

23 Lakini Yesu akawaambia, “Ninyi watu ni wa hapa chini, lakini mimi ni wa kule juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu, lakini mimi si wa ulimwengu huu. 24 Niliwaambia kwamba mnaweza kufa katika dhambi zenu. Ndiyo, kama hamtaamini kuwa MIMI NDIYE,[b] mtakufa katika dhambi zenu.”

25 Wakamwuliza, “Sasa wewe ni nani?”

Yesu akajibu, “Mimi ni yule niliyekwisha kuwaambia tangu mwanzo kuwa ni nani. 26 Ninayo mengi zaidi ya kusema na ya kuwahukumu. Lakini nawaambia watu yale tu niliyosikia kutoka kwake aliyenituma, naye daima husema kweli.”

27 Wale watu hawakuelewa alikuwa anazungumza habari za nani. Kwani Yeye alikuwa anawaambia habari za Baba. 28 Naye akawaambia, “Mtamwinua juu[c] Mwana wa Adamu. Ndipo mtakapojua kuwa MIMI NDIYE. Mtajua kuwa lo lote nilifanyalo silifanyi kwa mamlaka yangu. Mtajua kuwa nayasema tu yale Baba yangu aliyonifundisha. 29 Yeye aliyenituma yuko pamoja nami. Siku zote nafanya yale yanayompendeza. Naye hajawahi kuniacha peke yangu.” 30 Yesu alipokuwa akisema mambo haya, watu wengi wakamwamini.

Yesu Azungumzia Uhuru kutokana na Dhambi

31 Hivyo Yesu akawaambia Wayahudi waliomwamini, “Kama mtaendelea kuyakubali na kuyatii mafundisho yangu, mtakuwa wafuasi wangu wa kweli. 32 Mtaijua kweli, na kweli hiyo itawafanya muwe huru.”

33 Wakamjibu, “Sisi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Na hatujawahi kamwe kuwa watumwa. Sasa kwa nini unasema kuwa tutapata uhuru?”

34 Yesu akasema, “Ukweli ni huu, kila anayefanya dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Mtumwa hakai na jamaa yake siku zote. Lakini mwana hukaa na jamaa yake siku zote. 36 Hivyo kama Mwana atawapa uhuru, mtakuwa mmepata uhuru wa kweli. 37 Najua kuwa ninyi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Lakini mmekusudia kuniua, kwa sababu hamtaki kuyakubali mafundisho yangu. 38 Nawaambia yale ambayo Baba yangu amenionyesha. Lakini ninyi mnayafanya yale mliyoambiwa na baba yenu.”

39 Wakasema, “Baba yetu ni Ibrahimu.”

Yesu akasema, “Kama mngekuwa wazaliwa wa Ibrahimu kweli, mngefanya yale aliyofanya Ibrahimu. 40 Mimi ni mtu niliyewaambia ukweli niliousikia kutoka kwa Mungu. Lakini Ibrahimu hakufanya kama hayo mnayotaka kufanya. 41 Mnafanya yale aliyofanya baba yenu.”

Lakini wakasema, “Sisi sio kama watoto ambao hawajawahi kumjua baba yao ni nani. Mungu ni Baba yetu. Ni baba pekee tuliye naye.”

42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu kweli, mngenipenda. Nilitoka kwa Mungu, na sasa niko hapa. Sikujileta kwa mamlaka yangu mwenyewe. Mungu alinituma. 43 Hamuyaelewi mambo ninayosema, kwa sababu hamuwezi kuyakubali mafundisho yangu. 44 Baba yenu ni ibilisi. Ninyi ni wa kwake. Nanyi mnataka kufanya anayotaka. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo. Siku zote alikuwa kinyume na ukweli. Hakuna ukweli ndani yake. Yuko kama uongo anaousema. Ndiyo, ibilisi ni mwongo. Na ni baba wa uongo.

45 Nawaambieni ukweli, na ndiyo maana hamniamini. 46 Kuna mtu miongoni mwenu anayeweza kunishuhudia kuwa mimi nina hatia ya dhambi? Kama nawaeleza ukweli, kwa nini hamniamini? 47 Yeyote aliye wa Mungu huyapokea anayosema. Lakini ninyi hamuyapokei anayosema Mungu, kwa sababu ninyi si wa Mungu.”

Yesu Azungumza Juu yake na Ibrahimu

48 Wayahudi wakajibu, “Sisi tunasema kuwa wewe ni Msamaria na pepo anakufanya uwe mwendawazimu! Je, hatuko sahihi kusema hivyo?”

49 Yesu akajibu, “Sina pepo ndani yangu. Nampa heshima Baba yangu, lakini ninyi hamnipi heshima. 50 Sijaribu kujitukuza mimi mwenyewe. Yupo mmoja anayetaka kunitukuza. Ndiye hakimu. 51 Nawaahidi, yeyote anayeendelea kutii mafundisho yangu, hatakufa milele.”

52 Wayahudi wakamwambia Yesu, “Sasa tunatambua kuwa una pepo ndani yako! Hata Ibrahimu na manabii walikufa. Lakini unasema, ‘Yeyote anayetii mafundisho yangu, hatakufa kamwe.’ 53 Wewe si mkuu zaidi ya baba yetu Ibrahimu! Yeye alikufa na manabii nao walikufa. Unadhani wewe ni nani?”

54 Yesu akajibu, “Kama ningejipa heshima mwenyewe, heshima hiyo isingelifaa kwa namna yoyote ile. Yule anayenipa mimi heshima ni Baba yangu. Ninyi mnasema kuwa ndiye Mungu wenu. 55 Lakini kwa hakika hamumjui yeye. Mimi namjua. Kama ningesema simjui, basi ningekuwa mwongo kama ninyi. Lakini namjua, na kuyatii anayosema. 56 Baba yenu Ibrahimu alifurahi sana kwamba angeiona siku nilipokuja duniani. Hakika aliiona na akafurahi sana.”

57 Wayahudi wakamwambia Yesu, “Ati nini? Wawezaje kusema ulimwona Ibrahimu? Wewe bado hujafikisha hata umri wa miaka hamsini!”

58 Yesu akajibu, “Ukweli ni kwamba, kabla Ibrahimu hajazaliwa MIMI NIPO.” 59 Aliposema haya, wakachukua mawe ili wamponde. Lakini Yesu akajificha, na kisha akaondoka katika eneo la Hekalu.

Footnotes

  1. 8:11 Nakala za kale na bora za Kiyunani hazina mistari 7:53-8:11. Nakala zingine zina sehemu hii katika maeneo mbalimbali kitabuni.
  2. 8:24 MIMI NDIYE Hili ni kama Jina la Mungu lililotumiwa katika Agano la Kale. Tazama Isa 41:4; 43:10; Kut 3:14. Hata hivyo, Inaweza kuwa na maana ya “Mimi Ndiye”, maana yake “Mimi Ndiye Masihi”. Pia katika mstari wa 28,58.
  3. 8:28 Mtamwinua juu Ina maana kugongomelewa msalabani na “kuinuliwa juu yake ili kufa”. Inaweza kuwa pia kuwa na maana ya pili: “Kuinuliwa juu”.