Add parallel Print Page Options

Yesu Amefufuka Kutoka Mauti

(Mt 28:1-10; Mk 16:1-8; Yh 20:1-10)

24 Asubuhi mapema sana siku ya Jumapili, wanawake walikwenda kaburini ulikolazwa mwili wa Yesu. Walibeba manukato yanayonukia vizuri waliyoyaandaa. Walikuta jiwe kubwa lililokuwa limeziba mlango wa kaburi limevingirishwa kutoka kwenye mlango wa kaburi. Waliingia kaburini, lakini hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. Hawakulielewa hili. Walipokuwa wangali wanashangaa, watu wawili waliovaa mavazi yaliyong'aa walisimama pembeni mwao. Wanawake waliogopa sana. Waliinama nyuso zao zikaelekea chini. Wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai hapa? Hapa ni mahali pa waliokufa. Yesu hayuko hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu. Mnakumbuka alivyosema alipokuwa Galilaya? Alisema kwamba, ‘Mwana wa Adamu lazima atatolewa kwa mamlaka ya watu wenye dhambi, lazima atauawa msalabani na kufufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu.’” Ndipo wanawake wakakumbuka Yesu alivyosema.

Wanawake wakaondoka kaburini na kurudi kwa mitume kumi na mmoja na wafuasi wengine. Waliwaeleza kila kitu kilichotokea kaburini. 10 Wanawake hawa walikuwa Mariamu Magdalena, Yoana, na Mariamu, mama yake Yakobo na wanawake wengine. Waliwaambia mitume kila kitu kilichotokea. 11 Lakini mitume hawakuamini yale waliyosema. Ilionekana kama upuuzi. 12 Lakini Petro alinyanyuka na kukimbia kwenda kaburini kuona. Alitazama ndani, lakini aliona nguo tu iliyotumika kuufunga mwili wa Yesu. Petro aliondoka kwenye kaburi akarudi nyumbani alikokuwa anakaa, akijiuliza nini kilichotokea.[a]

Njiani Kwenda Emausi

(Mk 16:12-13)

13 Siku hiyo hiyo, wafuasi wawili[b] wa Yesu walikuwa wanakwenda kwenye mji mdogo uitwao Emausi, uliokuwa yapata kilomita kumi na mbili[c] kutoka Yerusalemu. 14 Walikuwa wanazungumza kuhusu mambo yote yaliyotokea. 15 Walipokuwa wakizungumza, wakijadiliana juu ya mambo haya, Yesu mwenyewe aliwasogelea na akawa anatembea nao. 16 Lakini hawakuruhusiwa kumtambua. 17 Yesu akawauliza, “Ni mambo gani ninayosikia mnajadiliana mnapotembea?”

Wale wafuasi wawili wakasimama, sura zao zilionekana zenye huzuni. 18 Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa akasema, “Lazima wewe ni mtu pekee katika Yerusalemu ambaye hujui yaliyotokea huko.”

19 Yesu akasema, “Unasema kuhusu nini?”

Wakasema, “Ni kuhusu Yesu, kutoka Nazareti, alikuwa nabii mkuu mbele za Mungu na watu wote. Alisema na kutenda mambo makuu mengi. 20 Lakini viongozi wetu na viongozi wa makuhani walimtoa ili ahukumiwe na kuuawa. Wakampigilia msalabani. 21 Tulitegemea kuwa ndiye atakayeiweka huru Israeli. Lakini sasa haya yote yametokea.

Na sasa kitu kingine: Imekuwa ni siku tatu tangu alipouawa, 22 lakini leo baadhi ya wanawake kutoka kwenye kundi letu walituambia jambo la kushangaza. Mapema asubuhi hii walikwenda kaburini ambako mwili wa Yesu ulilazwa. 23 Lakini hawakuuona mwili wake pale. Walikuja na kutuambia kuwa wamewaona malaika. Malaika waliwaambia Yesu yu hai! 24 Hivyo baadhi ya watu walio katika kundi letu walikwenda kaburini pia. Ilikuwa kama wanawake walivyosema. Waliliona kaburi, lakini hawakumwona Yesu.”

25 Ndipo Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga na wazito wa kuyakubali yale waliyoandika manabii. 26 Manabii waliandika kwamba Masihi lazima ateseke kwa mambo haya kabla hajaingia katika utukufu wa ufalme wake.” 27 Kisha akaanza kufafanua kila kitu walichosema manabii kuhusu yeye. Alianzia katika vitabu vya Musa na kusema yale waliyosema manabii kuhusu yeye.

28 Wakakaribia mji wa Emausi, na Yesu akafanya kama vile alikuwa anaendelea mbele. 29 Lakini walimtaka akae, wakamsihi: “Kaa nasi. Tayari ni usiku. Mchana unakaribia kwisha.” Hivyo aliingia ndani kukaa nao.

30 Alipokuwa mezani pamoja nao ili kula chakula cha usiku, Yesu akachukua mkate na kushukuru. Kisha akaumega na kuwapa. 31 Baada ya kufanya hivyo, wafuasi wale wawili wakaruhusiwa kumtambua. Lakini walipojua yeye ni nani, alitoweka. 32 Wakasemezana, “Alivyokuwa anazungumza nasi tulipokuwa barabarani, tulijisikia kama moto unawaka ndani yetu. Ilitusisimua sana alipotufafanulia maana halisi ya Maandiko!”

33 Hivyo wafuasi wale wawili wa Bwana Yesu wakasimama na kurudi Yerusalemu haraka. Walipofika Yerusalemu waliwakuta mitume kumi na mmoja wamekusanyika pamoja na wafuasi wengine wa Bwana Yesu. 34 Kundi likawaambia wale wafuasi wawili, “Hakika Bwana amefufuka kutoka kwa wafu! Alimtokea Simoni.”

35 Ndipo wafuasi wawili wakaeleza kilichotokea barabarani. Wakaeleza jinsi walivyomtambua Yesu aliposhiriki mkate pamoja nao.

Yesu Awatokea Wafuasi Wake

(Mt 28:16-20; Mk 16:14-18; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)

36 Wakati wafuasi wawili wakiwa bado wanawaeleza mambo haya wafuasi wengine, Yesu mwenyewe akaja na kusimama katikati yao. Akawaambia, “Amani iwe kwenu.”

37 Wafuasi walishituka na wakaogopa. Walidhani wanaona mzimu. 38 Lakini Yesu akasema, “Kwa nini mnaogopa? Na kwa nini mnakitilia mashaka kile mnachokiona? 39 Angalieni mikono na miguu yangu. Hakika ni mimi. Niguseni. Mtaweza kuona kuwa nina mwili wenye nyama na mifupa; mzimu hauna mwili kama huu.”

40 Mara baada ya Yesu kusema haya, aliwaonesha mikono na miguu yake. 41 Wafuasi walishangaa na kufurahi sana walipoona kuwa Yesu alikuwa hai. Kwa kuwa bado walikuwa hawaamini wanachokiona, akawaambia, “Mna chakula chochote hapa?” 42 Wakampa kipande cha samaki aliyepikwa. 43 Wafuasi wake wakiwa wanaangalia akakichukua na kukila.

44 Yesu akawaambia, “Mnakumbuka nilipokuwa pamoja nanyi? Nilisema kila kitu kilichoandikwa kuhusu mimi katika Sheria ya Musa, vitabu vya manabii na Zaburi lazima kitimilike.”

45 Kisha Yesu akawafafanulia Maandiko ili waelewe maana yake halisi. 46 Yesu akawaambia, “Imeandikwa kuwa Masihi atauawa na atafufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu. 47-48 Mliona mambo haya yakitokea, ninyi ni mashahidi. Na maandiko yanasema inawapasa mwende na kuwahubiri watu kuwa ni lazima wabadilike na kumgeukia Mungu, ili awasamehe. Ni lazima mwanzie Yerusalemu na mhubiri ujumbe huu kwa jina langu kwa watu wa mataifa yote. 49 Kumbukeni kwamba nitamtuma kwenu yule ambaye Baba yangu aliahidi. Kaeni jijini mpaka mtakapopewa nguvu hiyo kutoka mbinguni.”

Yesu Arudi Mbinguni

(Mk 16:19-20; Mdo 1:9-11)

50 Yesu akawaongoza wafuasi wake kutoka nje ya Yerusalemu hadi karibu na Bethania. Akanyenyua mikono yake na kuwabariki wafuasi wake. 51 Alipokuwa anawabariki, alitenganishwa nao na kuchukuliwa mbinguni. 52 Wafuasi wake walimwabudu, kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha sana. 53 Walikuwa katika Hekalu wakati wote, wakimsifu Mungu.

Footnotes

  1. 24:12 Nakala chache za Kiyunani hazina mstari huu.
  2. 24:13 wafuasi wawili Kwa maana ya kawaida, “Miongoni mwa wafuasi”. Ni wazi kutokana na simulizi kuwa wote wawili ni wafuasi wa Yesu, lakini mmoja wao tu ndiye anayetajwa jina (mstari wa 18). Inawezekana akawa ndiye Kleopa, anayeelezwa katika Yh 19:25 kama mume wa mmoja wa wanawake anayeitwa Mariamu. Inawezekama mfuasi wa pili anayezungumzwa hapa ndiye huyu Mariamu.
  3. 24:13 kilomita kumi na mbili Kwa Kiyunani umbali huo ni sawa na “stadia 60”.