Add parallel Print Page Options

Mfano Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Chakula

(Mt 22:1-10)

15 Basi mmoja wa watu waliokuwa mezani pamoja naye aliposikia hayo akamwambia Yesu, “Wamebarikiwa watakaokula karamu katika ufalme wa Mungu.”

16 Yesu akamwambia, “Mtu mmoja aliandaa sherehe kubwa, na kuwaalika watu wengi. 17 Wakati wa kuanza sherehe ulipofika, alimtuma mtumishi wake awaambie wale walioalikwa, ‘Tafadhalini njooni sasa. Kila kitu kiko tayari.’ 18 Lakini wageni waalikwa wote walisema kuwa hawawezi kuja. Kila mmoja alitoa udhuru. Wa kwanza alisema, ‘Nimenunua shamba, hivyo ni lazima niende nikalitazame. Tafadhali unisamehe.’ 19 Mwingine alisema, ‘Nimenunua ng'ombe wa kulimia jozi tano; ni lazima niende kuwajaribu. Tafadhali unisamehe.’ 20 Na mtu wa tatu alisema, ‘Nimeoa mke, kwa sababu hiyo siwezi kuja.’

21 Hivyo mtumishi alirudi na kumjulisha bwana kilichotokea. Bwana wake akakasirika, akamwambia mtumishi wake, ‘Fanya haraka! Nenda mitaani na katika vichochoro vya mji. Niletee maskini, vilema, wasiyeona na walemavu wa miguu!’

22 Baadaye mtumishi akamwambia, ‘Mkuu nimefanya kama ulivyoniagiza, lakini bado tuna nafasi kwa ajili ya watu wengine zaidi.’ 23 Hivyo bwana wake akamwambia mtumishi, ‘Toka nje uende kwenye barabara zinazoelekea vijijini na kando kando ya mashamba. Waambie watu huko waje, ninataka nyumba yangu ijae! 24 Ninakwambia, sitaki mtu hata mmoja kati ya wale niliowaalika kwanza atakayekula chakula hiki nilichoandaa.’”

Read full chapter