Add parallel Print Page Options

Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu

(Mt 21:23-27; Mk 11:27-33)

20 Siku moja Yesu alikuwa anawafundisha watu katika eneo la Hekalu. Alikuwa anawahubiri Habari njema. Viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikwenda kuzungumza na Yesu. Wakamwambia, “Tuambie, una mamlaka gani kutenda mambo haya! Ni nani aliyekupa mamlaka hii?”

Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali pia. Niambieni: Yohana alipobatiza watu, mamlaka yake ilitoka kwa Mungu au kwa watu fulani?”

Makuhani, walimu wa sheria na viongozi wa Kiyahudi wakajadiliana kwa pamoja kuhusu hili. Wakasema, “Kama tukijibu ‘Ubatizo wa Yohana ulitoka kwa Mungu,’ atasema, ‘Sasa kwa nini hamkumwamini Yohana?’ Lakini kama tukisema ulitoka kwa watu fulani, watu hawa watatupiga kwa mawe mpaka tufe. Kwa sababu wote wanaamini Yohana alikuwa nabii.” Hivyo wakajibu, “Hatujui.”

Ndipo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni nani alinipa mamlaka kufanya mambo haya.”

Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu

(Mt 21:33-46; Mk 12:1-12)

Yesu akawaambia watu kisa hiki; “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Kisha akalikodisha kwa wakulima, kisha akasafiri kwa muda mrefu. 10 Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, alimtuma mmoja wa watumishi wake kwa wakulima wale ili wampe sehemu yake ya zabibu. Lakini wakulima wale walimpiga yule mtumishi na wakamfukuza bila kumpa kitu. 11 Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi mwingine. Wakulima walimpiga mtumishi huyu pia, wakamwaibisha na kumfukuza bila kumpa kitu. 12 Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi wa tatu. Wakulima wakampiga sana mtumishi huyu na wakamtupa nje ya shamba la mizabibu.

13 Mmiliki wa shamba la mizabibu akasema, ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa. Yumkini watamheshimu.’ 14 Lakini wakulima walipomwona mwana wa mwenye shamba, wakajadiliana wakisema, ‘Huyu ni mwana wa mmiliki wa shamba. Shamba hili la mizabibu litakuwa lake. Tukimwua, litakuwa letu.’ 15 Hivyo wakulima wakamtupa mwana wa mmiliki wa shamba nje ya shamba la mizabibu na wakamwua.

Je, mmiliki wa shamba la mizabibu atafanya nini? 16 Atakuja na atawaua wale wakulima, kisha atalikodisha shamba kwa wakulima wengine.”

Watu waliposikia mfano huu, wakasema, “Hili lisije kutokea!” 17 Lakini Yesu akawakazia macho na akasema, “Hivyo basi, Maandiko haya yanamaanisha nini:

‘Jiwe lililokataliwa na wajenzi,
    limekuwa jiwe kuu la pembeni?’[a]

18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika na ikiwa jiwe hilo litaangukia, litakusaga!”

19 Walimu wa sheria na wakuu wa makuhani waliposikia kisa hiki, walijua unawahusu wao. Hivyo walitaka kumkamata Yesu wakati huo huo, lakini waliogopa watu wangewadhuru.

Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego

(Mt 22:15-22; Mk 12:13-17)

20 Hivyo viongozi wa Kiyahudi walitafuta namna ya kumtega Yesu. Walituma watu waliojifanya kuwa wenye haki, ili waweze kumnasa ikiwa angesema jambo ambalo wangeweza kutumia kinyume naye. Ikiwa angesema jambo lolote baya, wangemkamata na kumpeleka kwa gavana wa Kirumi, mwenye mamlaka ya kumhukumu na kumwadhibu. 21 Hivyo wale watu wakamwambia Yesu, “Mwalimu, tunafahamu kwamba yale unayosema na kufundisha ni kweli. Haijalishi ni nani anasikiliza, unafundisha sawa kwa watu wote. Daima unafundisha ukweli kuhusu njia ya Mungu. 22 Tuambie, ni sahihi sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au si sahihi?”

23 Lakini Yesu alitambua watu hawa walikuwa wanajaribu kumtega. Akawaambia, 24 “Nionesheni sarafu ya fedha,” Kisha akauliza, “Jina na picha katika sarafu hii ni ya nani?”

Wakamjibu, “Ya Kaisari.”

25 Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari vilivyo vya Kaisari, na mpeni Mungu vilivyo vya Mungu.”

26 Watu wale wakashangaa jibu lake la hekima. Hawakusema kitu. Hawakuweza kumtega Yesu pale mbele za watu. Hakusema chochote kibaya ambacho wangekitumia ili kumnasa.

Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu

(Mt 22:23-33; Mk 12:18-27)

27 Baadhi ya Masadukayo walimwendea Yesu. (Masadukayo wanaamini watu hawatafufuka kutoka kwa wafu.) Wakamwuliza, 28 “Mwalimu, Musa aliandika kwamba mtu aliyeoa akifa na hakuwa na watoto, kaka au mdogo wake amwoe mjane wake, ili wawe na watoto kwa ajili ya yule aliyekufa.[b] 29 Walikuwepo ndugu saba. Wa kwanza alioa mke lakini akafa bila ya kuwa na watoto. 30 Wa pili akamuoa yule mwanamke kisha akafa. 31 Na wa tatu akamwoa mwanamke na akafa. Kitu kile kile kikawatokea ndugu wote saba. Walikufa bila ya kuwa na watoto. 32 Mwanamke akawa wa mwisho kufa. 33 Lakini ndugu wote saba walimwoa. Sasa, watu watakapofufuka kutoka kwa wafu, atakuwa mke wa yupi?”

34 Yesu akawaambia Masadukayo, “Watu huoana katika ulimwengu huu. 35 Baadhi ya watu watastahili kufufuliwa kutoka kwa wafu na kuishi tena katika ulimwengu ujao. Katika maisha yale hawataoa kamwe. 36 Katika maisha hayo, watu watakuwa kama malaika na hawatakufa. Ni watoto wa Mungu, kwa sababu wamefufuliwa kutoka kwa wafu. 37 Musa alionesha dhahiri kwamba watu hufufuliwa kutoka kwa wafu. Alipoandika kuhusu kichaka kilichokuwa kinaungua,[c] alisema kwamba Bwana ni ‘Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo.’(A) 38 Ni Mungu wa wanaoishi tu. Hivyo watu hawa kwa hakika hawakuwa wamekufa. Ndiyo, kwa Mungu watu wote bado wako hai.”

39 Baadhi ya walimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, jibu lako ni zuri.” 40 Hakuna hata mmoja aliyekuwa na ujasiri wa kumwuliza swali jingine.

Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?

(Mt 22:41-46; Mk 12:35-37)

41 Kisha Yesu akasema, “Kwa nini watu husema kwamba Masihi ni Mwana wa Daudi? 42 Katika kitabu cha Zaburi, Daudi mwenyewe anasema,

‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kulia,
43     na nitawaweka adui zako chini ya mamlaka yako.’[d](B)

44 Hivyo ikiwa Daudi anamwita Masihi, ‘Bwana’. Inawezekanaje Masihi awe mwana wa Daudi?”

Tahadhali Juu ya Walimu wa Sheria

(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 11:37-54)

45 Watu wote walipokuwa wanamsikiliza Yesu, akawaambia wafuasi wake, 46 “Iweni waangalifu dhidi ya walimu wa sheria. Wanapenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi yanayoonekana ya heshima. Na wanapenda pale watu wanapowasalimu kwa heshima maeneo ya masoko. Wanapenda kukaa sehemu za heshima katika masinagogi na sehemu za watu maarufu katika sherehe. 47 Lakini huwalaghai wajane na kuchukua nyumba zao. Kisha kujionesha kuwa waongofu wa mioyo kuomba sala ndefu. Mungu atawaadhibu kwa hukumu kuu.”

Footnotes

  1. 20:17 Zab 118:22. Yesu, ambaye ndiye “Jiwe” katika Zaburi hii, anajitambulisha mwenyewe kama mwana katika simulizi hii ambapo anauawa na wakulima wale. Tazama Mdo 4:11.
  2. 20:28 kwa ajili ya yule aliyekufa Tazama Kum 25:5-6.
  3. 20:37 kichaka kilichokuwa kinaungua Tazama Kut 3:1-12.
  4. 20:43 chini ya mamlaka yako Kwa maana ya kawaida, “mpaka nitakapowafanya maadui zako kuwa kiti cha kuweka miguu yako”.