Add parallel Print Page Options

Karamu ya Pasaka

(Mt 26:17-25; Lk 22:7-14,21-23; Yh 13:21-30)

12 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, ambapo kila mara mwana kondoo alitolewa sadaka kwa ajili ya Pasaka. Wanafunzi wa Yesu wakamwendea na kumwuliza, “Ni wapi unapotaka tuende kukuandalia ili uweze kuila Karamu ya Pasaka?”

13 Hivyo Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, naye akawaeleza, “ingieni mjini, na mtakutana na mtu mmoja aliyebeba gudulia la maji. Mfuateni, 14 popote pale atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba ile, ‘mwalimu anasema, utuonyeshe chumba ambacho yeye na wanafunzi wake wanaweza kuila Karamu ya Pasaka.’ 15 Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, klichoandaliwa tayari kwa ajili yetu. Basi mtuandalie chakula pale.”

16 Wanafunzi wa Yesu waliondoka na kuelekea mjini. Huko walikuta kila kitu kama vile Yesu alivyowaeleza Hivyo, waliandaa mlo wa Pasaka.

17 Wakati wa jioni Yesu alienda pamoja na wanafunzi wake kumi na mbili katika nyumba ile. 18 Wote walipokuwa wameketi mezani wakila, Yesu akasema, “Mniamini ninapowambia kwamba mmoja wenu, yule anayekula nami sasa atanitoa kwa maadui zangu.”

19 Wanafunzi walihuzunika sana kusikia jambo hili. Kila mmoja akamwambia Yesu, “Hakika siyo mimi?”

20 Akawaambia, “Ni mmoja wa wale kumi na mbili; na ni yule atakayechovya mkate katika bakuli pamoja nami. 21 Mwana wa Adamu atakiendea kifo chake kama ilivyoandikwa juu yake. Lakini itakuwa ya kutisha namna gani kwa mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu anasalitiwa. Itakuwa bora mtu huyu asingelikuwa amezaliwa.”

Read full chapter