Add parallel Print Page Options

Mpango wa Kumwua Yesu

(Mt 26:1-5; Lk 22:1-2; Yh 11:45-53)

14 Ilikuwa yapata siku mbili kabla ya Sikukuu ya Pasaka na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Wakuu wa makuhani na walimu wa Sheria walikuwa wakitafuta njia, kwa ujanja fulani, ya kumkamata na kumuua Yesu. Kwani walikuwa wakisema “tusifanye hivi wakati wa sherehe, ama sivyo watu watafanya fujo.”

Mwanamke Ampa Yesu Heshima

(Mt 26:6-13; Yh 12:1-8)

Yesu alikuwa Bethania, katika nyumba ya Simoni mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Wakati ameketi mezani mwanamke mmoja alimwijia. Naye alikuwa na gudulia la mawe lililojaa manukato ya bei ghali yaliyotengenezwa kwa nardo safi. Mwanamke huyo alilifungua gudulia lile kwa kulivunja na kumwagia Yesu manukato kichwani mwake.

Baadhi ya watu waliokuwa pale walikasirika na kulalamika miongoni mwao, “Kwa nini kuwepo na ufujaji wa manukato namna hii? Gharama yake ni sawa na mshahara wa mwaka[a] mzima. Manukato haya yangeweza kuuzwa na fedha hiyo kupewa walio maskini.” Kisha wakamkosoa yule mwanamke kwa hasira kwa jambo alilolifanya.

“Lakini Yesu alisema mwacheni peke yake. Kwa nini mnamsumbua? Yeye amenifanyia kitendo chema. Kwani siku zote mnao maskini pamoja nanyi na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini hamtakuwa pamoja nami siku zote. Yeye amefanya kile alichokiweza kufanya. Ameumwagia manukato mwili wangu kabla ya wakati kuuandaa kwa ajili ya maziko. Ninawaambia kweli: Popote injili itakapohubiriwa ulimwenguni, kile alichokifanya kitasimuliwa kwa kumkumbuka.”

Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu

(Mt 26:14-16; Lk 22:3-6)

10 Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na mbili, aliwaendea viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao. 11 Nao walifurahi kusikia hivyo, na wakaahidi kumpa fedha. Kwa hiyo Yuda akaanza kutafuta wakati unaofaa wa kumsaliti.

Karamu ya Pasaka

(Mt 26:17-25; Lk 22:7-14,21-23; Yh 13:21-30)

12 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, ambapo kila mara mwana kondoo alitolewa sadaka kwa ajili ya Pasaka. Wanafunzi wa Yesu wakamwendea na kumwuliza, “Ni wapi unapotaka tuende kukuandalia ili uweze kuila Karamu ya Pasaka?”

13 Hivyo Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, naye akawaeleza, “ingieni mjini, na mtakutana na mtu mmoja aliyebeba gudulia la maji. Mfuateni, 14 popote pale atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba ile, ‘mwalimu anasema, utuonyeshe chumba ambacho yeye na wanafunzi wake wanaweza kuila Karamu ya Pasaka.’ 15 Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, klichoandaliwa tayari kwa ajili yetu. Basi mtuandalie chakula pale.”

16 Wanafunzi wa Yesu waliondoka na kuelekea mjini. Huko walikuta kila kitu kama vile Yesu alivyowaeleza Hivyo, waliandaa mlo wa Pasaka.

17 Wakati wa jioni Yesu alienda pamoja na wanafunzi wake kumi na mbili katika nyumba ile. 18 Wote walipokuwa wameketi mezani wakila, Yesu akasema, “Mniamini ninapowambia kwamba mmoja wenu, yule anayekula nami sasa atanitoa kwa maadui zangu.”

19 Wanafunzi walihuzunika sana kusikia jambo hili. Kila mmoja akamwambia Yesu, “Hakika siyo mimi?”

20 Akawaambia, “Ni mmoja wa wale kumi na mbili; na ni yule atakayechovya mkate katika bakuli pamoja nami. 21 Mwana wa Adamu atakiendea kifo chake kama ilivyoandikwa juu yake. Lakini itakuwa ya kutisha namna gani kwa mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu anasalitiwa. Itakuwa bora mtu huyu asingelikuwa amezaliwa.”

Chakula cha Bwana

(Mt 26:26-30; Lk 22:15-20; 1 Kor 11:23-25)

22 Na walipokuwa wakila Yesu aliuchukua mkate, akamshukuru Mungu kwa huo. Akamega vipande, akawapa wanafunzi wake, na kusema, “Chukueni na mle mkate huu. Ni mwili wangu.”

23 Kisha akakichukua kikombe chenye divai, akamshukuru Mungu kwa hicho, akawapa. Wote wakanywa toka kile kikombe. 24 Kisha akasema, “Kinywaji hiki ni damu yangu ambayo kwayo Mungu anafanya agano na watu wake. Damu yangu inamwagika kwa manufaa ya watu wengi. 25 Ninawaambia kweli sitakunywa diva tena mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya katika Ufalme wa Mungu.”

26 Na wao wakaimba mwimbo wa sifa na kutoka na kuelekea kwenye Mlima wa Miti ya Mizeituni.

Yesu Asema Wafuasi Wake Watamwacha

(Mt 26:31-35; Lk 22:31-34; Yh 13:36-38)

27 Yesu akawaambia, “Nyote mtaniacha, kwani imeandikwa,

‘Nitamuua mchungaji,
    na kondoo watatawanyika.’(A)

28 Lakini baada ya kuuawa, nitafufuka kutoka kwa wafu. Kisha nitaenda Galilaya. Nitakuwa pale kabla ninyi hamjafika.”

29 Lakini Petro akamwambia, “Hata kama wengine wote watapoteza imani yao, mimi sitapoteza imani yangu.”

30 Ndipo Yesu akamjibu kusema, “Ukweli ni kwamba, usiku wa leo utasema kuwa hunijui. Utasema hivyo mara tatu kabla ya jogoo kuwika mara mbili.”

31 Petro akasema kwa kusisitiza zaidi, “Hata kama itanipasa kufa nawe, sitasema kuwa sikujui.” Na wengine wakasema hivyo.

Yesu Aomba Akiwa Peke Yake

(Mt 26:36-46; Lk 22:39-46)

32 Kisha wakafika mahali palipoitwa Gethsemane. Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati ninaomba.” 33 Naye Yesu akamchukua Petro, Yakobo, na Yohana pamoja naye, naye akaanza kusumbuka sana. 34 Akawaambia, “Nina huzuni sana na ninafikiri inaweza kuniua. Kaeni hapa, na mjihadhari.”

35 Akiendelea mbele kidogo, alianguka chini, na akaomba ikiwezekana angeiepuka saa ya mateso. 36 Akasema, “Aba,[b] yaani Baba, vyote vinawezekana kwako wewe. Hebu kiondoe kikombe[c] hiki kutoka kwangu, Lakini usifanye kama ninavyopenda mimi, lakini kama unavyopenda wewe.”

37 Kisha Yesu akaja na kuwakuta wamelala, na akamwuliza Petro, “Simoni, je umelala? Je, hukuweza kukaa macho kwa muda wa saa moja tu? 38 Kaeni macho na kuomba, ili msije mkaingia majaribuni. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.”

39 Yesu akaondoka kwenda kuomba tena, akilisema jambo lile lile. 40 Kisha akarudi tena na kuwakuta wamelala, kwani macho yao yalikuwa yamechoka. Wao hawakujua la kusema kwake.

41 Alirudi mara ya tatu na kuwaambia, “Je, bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imefika. Mwana wa Adamu atasalitiwa mikononi mwa watenda dhambi. 42 Amkeni! Twendeni! Tazama! Yule atakayenisaliti amekaribia.”

Yesu Akamatwa

(Mt 26:47-56; Lk 22:47-53; Yh 18:3-12)

43 Mara moja, wakati Yesu akali akizungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na mbili, alitokea. Pamoja naye walikuwa kundi kubwa la watu waliokuwa na majambia na marungu wakitoka kwa viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na wazee.

44 Msaliti alikuwa tayari amewapa ishara: “Yule ambaye nitambusu ndiye mwenyewe. Mkamateni, mlindeni na muwe waangalifu mnapomwondoa.” 45 Mara tu Yuda alipowasili, alimwendea Yesu. Alipomkaribia alisema, “Mwalimu!” Kisha akambusu. 46 Ndipo walipomkamata na kumshikilia. 47 Mmoja wa wale waliosimama naye karibu akautoa upanga wake alani, akampiga nao mtumishi wa kuhani mkuu na kulikata sikio lake.

48 Kisha Yesu akawaambia, “Je, mlikuja kunikamata kwa upanga na marungu, kama vile mimi nimekuwa jambazi? 49 Kila siku nilikuwa nanyi, nikifundisha Hekaluni na hamkujaribu kunikamata wakati huo. Lakini Maandiko lazima yatimie.” 50 Wafuasi wake wote walimwacha na kumkimbia.

51 Miongoni mwa watu waliomfuata Yesu alikuwa kijana mmoja aliyevaa kipande cha nguo. Watu walipotaka kumkamata 52 alikiacha kile kipande cha nguo mikononi mwao na kukimbia akiwa uchi.

Yesu Akiwa Mbele ya Viongozi wa Kidini

(Mt 26:57-68; Lk 22:54-55,63-71; Yh 18:13-14,19-24)

53 Nao wakamwongoza Yesu kumpeleka kwa kuhani mkuu, na viongozi wote wa makuhani, wazee, na walimu wa Sheria walikutanika. 54 Petro akamfuata Yesu kwa mbali kidogo hadi ndani ya baraza la nyumba ya kuhani mkuu. Petro alikuwa ameketi na wale walinzi akijipasha joto na moto walioukoka.

55 Viongozi wa makuhani na Baraza lote la Wayahudi walikuwa wakitafuta ushahidi dhidi ya Yesu wa kuweza kumhukumu kifo, lakini hawakupata kitu chochote. 56 Watu wengi walikuja na kutoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini wote walisema vitu tofauti. Ushahidi wao ulipingana.

57 Kisha wengine walisimama na kushuhudia kinyume chake kwa uongo, wakisema, 58 “Tulimsikia mtu huyu[d] akisema, ‘Nitaliharibu Hekalu hili lililotengenezwa kwa mikono ya wanadamu, na kwa siku tatu nitajenga lingine ambalo halikujengwa kwa mikono.’” 59 Lakini hata katika ushahidi wao huu hawakukubaliana.

60 Kisha kuhani mkuu akasimama mbele yao na akamwuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Nini ushahidi huu ambao watu wanaleta dhidi yako?” 61 Lakini Yesu alinyamaza kimya na hakutoa jibu lolote.

Kwa mara nyingine kuhani mkuu akamwuliza, “Je, wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu anayesifiwa?”

62 Yesu akasema, “Mimi ndiye. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye uweza wote akija pamoja na mawingu ya mbinguni.”[e]

63 Kuhani mkuu alichana mavazi yake na kusema, “Tuna haja gani ya kuleta mashahidi zaidi? 64 Ninyi wote mmesikia akimtolea Mungu matusi.”

Wote walimhukumu na kumwona kwa anastahili kifo. 65 Na wengine walianza kutema mate, na kufunika uso wake, na kumpiga, na kumwambia, “Uwe nabii na utuambie nani aliyekupiga.” Kisha wale walinzi walimchukua na kuendelea kumpiga.

Petro Amkana Yesu

(Mt 26:69-75; Lk 22:56-62; Yh 18:15-18,25-27)

66 Wakati Petro alipokuwa bado barazani, mtumishi wa kike wa kuhani mkuu alifika pale. 67 Alipomwona Petro akijipasha moto, alimkazia macho na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

68 Lakini Petro alisema, “Hii si kweli, mie sifahamu wala kuelewa kile unachokisema.” Baada ya hapo Petro alitoka na kwenda barazani na hapo hapo jogoo akawika.

69 Yule mtumishi wa kike alipomwona alirudia tena kuwaeleza wale waliokuwa wamesimama pale, “Mtu huyu ni mmoja wao!” 70 Kwa mara nyingine tena Petro alikataa.

Baada ya muda mfupi wale waliokuwa wamesimama pale wakarudia tena kumwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa sababu wewe pia ni Mgalilaya.”

71 Petro akaanza kutoa maneno makali na kusema, “Naapa kwa Mungu, simjui mtu huyu mnayemzungumzia!”

72 Mara jogoo akawika kwa mara ya pili, na Petro akakumbuka lile neno la Yesu alilomwambia: “Kabla kogoo hajawika mara ya pili utanikana mara tatu.” Naye akavunjika moyo na kuanza kulia.

Footnotes

  1. 14:5 mshahara wa mwaka Wa mwaka wa mtu kwa hali halisi “dinari 300” (sarafu za fedha). Sarafu moja, dinari ya Kirumi, ilikuwa ni wastani wa mshahara wa mtu wa siku moja.
  2. 14:36 Aba Ni neno la Kiaramu lililotumiwa na watoto wa Kiyahudi kama jina la kuwaita baba zao.
  3. 14:36 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao.
  4. 14:58 mtu huyu Yaani, Yesu. Adui zake walikuwa wanakwepa kutamka jina lake.
  5. 14:62 Mwana wa Adamu … ya mbinguni Tazama Dan 7:13 na Zab 110:1.