Add parallel Print Page Options

Yesu Akamatwa

(Mt 26:47-56; Mk 14:43-50; Lk 22:47-53)

18 Yesu alipomaliza kuomba, akaondoka pamoja na wafuasi wake kwenda ng'ambo kuvuka bonde la Kidroni. Akaenda katika bustani mahali hapo, akiwa bado pamoja na wafuasi wake.

Yuda, yule aliyehusika kumsaliti Yesu, alipafahamu mahali pale. Alipajua kwa sababu Yesu mara nyingi alikutana na wafuasi wake pale. Kwa hiyo Yuda akaongoza kundi la askari hadi katika bustani hiyo pamoja na walinzi wengine kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Hawa walikuwa wamebeba mienge, taa, na silaha.

Yesu alikwisha kujua yote ambayo yangempata. Hivyo aliwaendea na kuwauliza, “Je, ni nani mnayemtafuta?”

Wakamjibu, “Yesu kutoka Nazareti.”

Akawaambia, “Mimi ni Yesu.”[a] (Yuda yule aliyehusika kumsaliti Yesu alikuwa amesimama hapo pamoja nao.) Yesu aliposema, “Mimi ni Yesu,” wale watu walirudi nyuma na kuanguka chini.

Akawauliza tena, “Je, ni nani mnayemtafuta?”

Wakasema, “Yesu kutoka Nazareti.”

Yesu akasema, “Nimewaambia kwamba mimi ndiye Yesu. Hivyo kama mnanitafuta mimi, basi waacheni huru watu hawa waende zao.” Hii ilikuwa kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu mapema: “Sikumpoteza hata mmoja wa wale ulionipa.”

10 Simoni Petro akauchomoa upanga aliokuwa ameufunga kiunoni. Akampiga nao mtumishi wa Kuhani Mkuu, na kulikata sikio lake la kulia. (Jina la mtumishi huyo lilikuwa ni Maliko.) 11 Yesu akamwambia Petro, “Rudisha jambia lako mahali pake! Ninapaswa kunywa toka kikombe[b] ambacho Baba amenipa nikinywee.”

Yesu Aletwa Mbele ya Anasi

(Mt 26:57-58; Mk 14:53-54; Lk 22:54)

12 Kisha askari hao pamoja na mkuu wao na walinzi wa Kiyahudi wakamkamata Yesu. Wakamfunga, 13 nao wakampeleka kwanza kwa Anasi, baba mkwe wa Kayafa. Kayafa alikuwa Kuhani Mkuu kwa mwaka huo. 14 Naye ndiye aliyewashauri viongozi wengine wa Kiyahudi kwamba ingemfaa mtu mmoja afe[c] kwa ajili ya watu wote.

Petro Amkana Yesu

(Mt 26:69-70; Mk 14:66-68; Lk 22:55-57)

15 Simoni Petro na mmoja wa wafuasi wengine wa Yesu walienda pamoja na Yesu. Mfuasi huyu alimfahamu kuhani mkuu. Hivyo akaingia pamoja na Yesu ndani ya uwanja wa nyumba ya kuhani mkuu. 16 Lakini Petro alisubiri nje karibu na mlango. Yule mfuasi aliyemjua kuhani mkuu alirudi nje na kuongea na mlinda mlango. Kisha alimleta Petro ndani. 17 Msichana aliyekuwepo langoni alimwambia Petro, “Je! Wewe pia ni mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”

Petro akajibu, “Hapana, mimi siye!”

18 Ilikuwa baridi, hivyo watumishi na walinzi waliwasha moto wa kuni. Walikuwa wameuzunguka, wakipasha joto miili yao naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao.

Kuhani Mkuu Amhoji Yesu

(Mt 26:59-66; Mk 14:55-64; Lk 22:66-71)

19 Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu maswali kuhusu wafuasi wake pamoja na mafundisho aliyowapa. 20 Yesu akamjibu, “Daima nimesema wazi kwa watu wote. Siku zote nimefundisha kwenye masinagogi na kwenye eneo la Hekalu. Wayahudi wote hukusanyika pale. Sijawahi kusema jambo lo lote kwa siri. 21 Sasa kwa nini unaniuliza? Waulize watu waliosikia mafundisho yangu. Wao wanajua niliyosema!”

22 Yesu aliposema hivyo, mmoja wa walinzi aliyekuwa amesimama hapo akampiga. Mlinzi huyo akasema, “Hupaswi kusema hivyo kwa kuhani mkuu!”

23 Yesu akajibu, “Kama nimesema vibaya jambo lo lote, mwambie kila mtu hapa kosa lenyewe. Lakini kama niliyosema ni sahihi, kwa nini basi unanipiga?”

24 Hivyo Anasi akampeleka Yesu kwa Kayafa kuhani mkuu. Naye alikuwa bado amefungwa.

Petro Amkana Yesu tena

(Mt 26:71-75; Mk 14:69-72; Lk 22:58-62)

25 Simoni Petro alikuwa amesimama karibu na moto, akijipasha joto. Watu wengine wakamwambia Petro, “Je, wewe si mmoja wa wafuasi wa mtu yule?”

Petro alikataa hilo. Akasema, “Hapana, mimi siye.”

26 Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu alikuwapo pale. Naye alikuwa ni jamaa wa mtu yule aliyekatwa sikio na Petro. Mtumishi akamwambia Petro, “Nadhani nilikuona pamoja naye pale kwenye bustani!”

27 Lakini kwa mara nyingine Petro akasema, “Hapana, sikuwa pamoja naye!” Mara tu alipomaliza kusema hayo, jogoo akawika.

Yesu Apelekwa kwa Gavana Pilato

(Mt 27:1-2,11-31; Mk 15:1-20; Lk 23:1-25)

28 Kisha walinzi wakamchukua Yesu kutoka katika nyumba ya Kayafa kwenda kwenye jumba la mtawala wa Kirumi. Nayo ilikuwa ni mapema asubuhi. Wayahudi waliokuwa pale wasingeweza kuingia ndani ya jumba hilo. Wao hawakutaka kujinajisi wenyewe kwa sababu walitaka kuila karamu ya Pasaka. 29 Kwa hiyo Pilato akatoka nje kuwafuata na akawauliza, “Mnasema mtu huyu amefanya makosa gani?”

30 Wakajibu, “Yeye ni mtu mbaya. Ndiyo maana tumemleta kwako.”

31 Pilato akawaambia, “Mchukueni wenyewe na kumhukumu kufuatana na sheria yenu.” Viongozi wa Wayahudi wakamwambia, “Lakini sheria yako haituruhusu sisi kumwadhibu mtu yeyote kwa kumwua.” 32 (Hii ilikuwa ni kuonesha ukweli wa yale aliyosema Yesu juu ya jinsi ambavyo angekufa.)

33 Kisha Pilato alirudi ndani ya jumba lile. Aliagiza Yesu aje na akamuuliza, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?”

34 Yesu akajibu, “Je, hilo ni swali lako mwenyewe au watu wengine wamekuambia juu yangu?”

35 Pilato akajibu, “Mimi sio Myahudi! Ni watu wako mwenyewe na viongozi wa makuhani waliokuleta kwangu. Je, umefanya kosa gani?”

36 Yesu akajibu, “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ungekuwa hivyo, watumishi wangu wangenipigania ili nisikabidhiwe kwa viongozi wa Wayahudi. Hapana, ufalme wangu sio wa kidunia.”

37 Pilato akasema, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?”

Yesu akamjibu, “Uko sahihi unaposema kuwa mimi ni mfalme. Nami nilizaliwa kwa ajili ya hili: kuwaeleza watu juu ya kweli. Ni kwa sababu hii nalikuja ulimwenguni. Kila mmoja aliye wa upande wa kweli hunisikiliza.”

38 Pilato akasema, “Kweli ndiyo nini?” Kisha alitoka nje tena kwenda kwa viongozi wa Wayahudi na kuwaimbia, “Mimi sipati kitu chochote kibaya cha kumpinga mtu huyu. 39 Lakini ni moja ya desturi zenu kwangu mimi kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi’?”

40 Wakajibu kwa kupiga kelele wakisema, “Hapana, siyo yeye! Mwache huru Baraba!” (Baraba alikuwa jambazi.)

Footnotes

  1. 18:5 Mimi ni Yesu Kwa maana ya kawaida, “Mimi ndimi”, ambayo inaweza kuwa na maana ile ile hapa kama ilivyo katika 8:24,28,58; 13:19. Pia katika mstari wa 8.
  2. 18:11 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao.
  3. 18:14 mtu mmoja afe Kifo cha Yesu kilikuwa kwa ajili ya watu wote wa ulimwengu siyo kwa Wayahudi peke yao.