Add parallel Print Page Options

Mpango wa Kumwua Yesu

(Mt 26:1-5; Mk 14:1-2; Yh 11:47-53)

22 Ilikuwa karibu ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, inayoitwa Pasaka. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walitaka kumwua Yesu kwa siri kwa sababu waliogopa kile ambacho watu wangefanya.

Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu

(Mt 26:14-16; Mk 14:10-11)

Mmoja wa mitume kumi na wawili wa Yesu aliitwa Yuda Iskariote. Shetani alimwingia Yuda, akaondoka, akaenda kuongea na viongozi wa makuhani na baadhi ya wakuu wa askari walinzi wa Hekalu. Aliongea nao kuhusu namna ya kumkabidhi Yesu kwao. Makuhani walifurahia sana hili. Wakaahidi kumlipa Yuda pesa ikiwa angefanya hivi. Akakubali, kisha alianza kusubiri muda mzuri wa kumkabidhi Yesu kwao. Alitaka kumkabidhi Yesu kwao wakati hakuna kundi la watu ambao wangeona.

Karamu ya Pasaka

(Mt 26:17-25; Mk 14:12-21; Yh 13:21-30)

Siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu[a] ilifika. Hii ni siku ambayo Wayahudi daima walichinja kondoo kwa ajili ya Pasaka. Yesu aliwaambia Petro na Yohana, “Nendeni mkaandae mlo wa Pasaka ili tule.”

Wakamwambia, “Unataka tukauandae wapi?”

Akawaambia, 10 “Mtakapokuwa mnaingia mjini, mtakutana na mtu amebeba mtungi wa maji. Mfuateni. Ataingia katika nyumba. 11 Mwambieni mmiliki wa nyumba, ‘Mwalimu anakuomba tafadhali utuoneshe chumba ambacho yeye na wafuasi wake wanaweza kulia mlo wa Pasaka.’ 12 Mmiliki atawaonesha chumba kikubwa ghorofani kilicho tayari kwa ajili yetu. Andaeni mlo humo.”

13 Hivyo Petro na Yohana wakaondoka. Kila kitu kilitokea kama Yesu alivyosema. Na hivyo wakauandaa mlo wa Pasaka.

Chakula cha Bwana

(Mt 26:26-30; Mk 14:22-26; 1 Kor 11:23-25)

14 Wakati ulifika kwa wao kula mlo wa Pasaka. Yesu na mitume walikuwa wamekaa pamoja kuzunguka meza ya chakula. 15 Yesu akawaambia, “Nilitaka sana kula mlo huu wa Pasaka pamoja nanyi kabla sijafa. 16 Sitakula mlo mwingine wa Pasaka mpaka itakapopewa maana yake kamili katika ufalme wa Mungu.”

17 Kisha Yesu akachukua kikombe kilichokuwa na divai. Akamshukuru Mungu, na akasema, “Chukueni kikombe hiki na kila mmoja anywe. 18 Sitakunywa divai tena mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja.”

19 Kisha akaichukua baadhi ya mkate na akamshukuru Mungu. Akaigawa vipande vipande, akawapa vipande mitume na kusema, “Mkate huu ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili yenu. Kuleni kwa kunikumbuka.” 20 Katika namna ile ile, baada ya kula chakula, Yesu akachukua kikombe chenye divai na akasema, “Divai hii inawakilisha Agano Jipya kutoka kwa Mungu kwa watu wake. Litaanza pale damu yangu itakapomwagika kwa ajili yenu.”[b]

Nani Atamsaliti Yesu?

21 Yesu akasema, “Lakini hapa mezani kuna mkono wa yule atakayenisaliti kwa adui zangu. 22 Mwana wa Adamu atakufa kama Mungu alivyoamua. Lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Adamu ili auawe.”

23 Ndipo mitume wakaulizana, “Ni nani miongoni mwetu atafanya hivyo?”

Iweni Kama Mtumishi

24 Baadaye, mitume wakaanza kubishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu. 25 Lakini Yesu akawaambia, “Wafalme wa mataifa wanawatawala watu kama watumwa wao, na wenye mamlaka juu ya wengine wanataka kuitwa, ‘Wafadhili Wakuu’. 26 Lakini ni lazima msiwe hivyo. Aliye na mamlaka zaidi miongoni mwenu lazima awe kama asiye na mamlaka. Anayeongoza anapaswa kuwa kama anayetumika. 27 Nani ni mkuu zaidi: Yule anayetumika au yule aliyekaa mezani na kuhudumiwa? Kila mtu hudhani ni yule aliyekaa mezani akihudumiwa, sawa? Lakini nimekuwa pamoja nanyi kama ninayetumika.

28 Na ninyi ndiyo mliobaki pamoja nami katika mahangaiko mengi. 29 Hivyo ninawapa mamlaka kutawala pamoja nami katika ufalme ambao Baba yangu amenipa. 30 Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme huo. Mtakaa katika viti vya enzi na kuwahukumu makabila kumi na mbili ya Israeli.

Petro Atajaribiwa na Kushindwa

(Mt 26:31-35; Mk 14:27-31; Yh 13:36-38)

31 Shetani ameomba ili awapepete kwa nguvu kama mkulima anavyopepeta ngano kwenye ungo ili mwanguke. Simoni, Simoni,[c] 32 nimekuombea ili usipoteze imani yako! Wasaidie ndugu zako kuwa imara utakaponirudia.”

33 Lakini Petro akamwambia Yesu, “Bwana, niko tayari kufungwa gerezani pamoja nawe. Hata kufa pamoja nawe!”

34 Lakini Yesu akasema, “Petro, asubuhi kabla jogoo hajawika, utakuwa umenikana mara tatu.”

Iweni Tayari kwa Matatizo

35 Kisha Yesu akawaambia mitume, “Kumbukeni nilipowatuma bila pesa, mkoba, wala viatu. Je, mlipungukiwa chochote?”

Mitume wakajibu, “Hapana.”

36 Yesu akawaambia, “Lakini sasa kama una pesa au mkoba, uchukue pamoja nawe. Kama huna upanga, uza koti lako ukanunue. 37 Maandiko yanasema, ‘Alidhaniwa kuwa mhalifu.’(A) Maandiko haya lazima yatimizwe. Yaliyoandikwa kuhusu mimi yanatimilika sasa.”

38 Wafuasi wakasema, “Tazama Bwana, hapa kuna panga mbili.”

Yesu akawaambia, “Nyamazeni, acheni mazungumzo ya namna hiyo!”

Yesu Aomba Akiwa Peke Yake

(Mt 26:36-46; Mk 14:32-42)

39-40 Yesu akaondoka mjini akaenda Mlima wa Mizeituni. Wafuasi wake wakaenda pamoja naye. (Alikuwa akienda huko mara kwa mara.) Akawaambia wafuasi wake, “Ombeni ili mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.”

41 Kisha Yesu akaenda kama hatua hamsini mbali nao. Akapiga magoti na akaomba akisema, 42 “Baba, ukiwa radhi, tafadhali usinifanye ninywe katika kikombe[d] hiki. Lakini fanya unalotaka wewe, siyo ninalotaka mimi.” 43 Kisha malaika kutoka mbinguni akaja akamtia nguvu. 44 Yesu aliomba kwa nguvu zaidi na kustahimili zaidi kama mpiganaji wa mieleka akiwa katika mapambano makali. Jasho kama matone ya damu likadondoka kutoka kwenye uso wake.[e] 45 Alipomaliza kuomba, alikwenda kwa wafuasi wake. Akawakuta wamelala, wamechoka kwa sababu ya huzuni. 46 Yesu akawaambia, “Kwa nini mnalala? Amkeni, ombeni mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.”

Yesu Akamatwa

(Mt 26:47-56; Mk 14:43-50; Yh 18:3-11)

47 Yesu alipokuwa anaongea, kundi likaja. Lilikuwa linaongozwa na Yuda, mmoja wa mitume kumi na wawili. Akamwendea Yesu ili ambusu.

48 Lakini Yesu akamwambia, “Yuda unatumia busu la urafiki kumsaliti Mwana wa Adamu kwa adui zake?” 49 Wafuasi wa Yesu walikuwa wamesimama pale pia. Walipoona kilichokuwa kinatokea, wakamwambia Yesu, “Bwana, tutumie panga zetu?” 50 Na mmoja wao akautumia upanga wake. Akakata sikio la kulia la mtumishi wa kuhani mkuu.

51 Yesu akasema, “Acha!” Kisha akaligusa sikio la mtumishi na akamponya.

52 Yesu akaliambia lile kundi lililokuja kumkamata. Walikuwa viongozi wa makuhani, viongozi wa wazee wa Kiyahudi na askari walinzi wa Hekalu. Akawaambia, “Kwa nini mmekuja hapa mkiwa na mapanga na marungu? Mnadhani mimi ni mhalifu? 53 Nilikuwa pamoja nanyi kila siku katika eneo la Hekalu. Kwa nini hamkujaribu kunikamata pale? Lakini sasa ni wakati wenu, wakati ambao giza linatawala.”

Petro Amkana Yesu

(Mt 26:57-58,69-75; Mk 14:53-54,66-72; Yh 18:12-18,25-27)

54 Walimkamata Yesu na kumpeleka nyumbani kwa kuhani mkuu. Petro alimfuata Yesu lakini alikaa nyuma kwa mbali. 55 Baadhi ya watu walikoka moto katikati ya ua kisha wakaketi pamoja. Petro naye aliketi pamoja nao. 56 Kutokana na mwanga wa moto, mtumishi wa kike alimwona Petro amekaa pale. Akamtazama Petro usoni kwa makini. Kisha akasema, “Huyu pia alikuwa na yule mtu.”

57 Lakini Petro akasema si kweli. Akasema, “Mwanamke, simfahamu mtu huyo!” 58 Muda mfupi baadaye, mtu mwingine akamwona Petro na akasema, “Wewe pia ni mmoja wa lile kundi!”

Lakini Petro akasema, “Wewe, mimi si mmoja wao!”

59 Baada ya kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasema, “Ni kweli, nina uhakika mtu huyu alikuwa pamoja naye, kwa sababu yeye pia anatoka Galilaya.”

60 Lakini Petro akasema, “Wewe, wala sijui unazungumza kuhusu nini!”

Alipokuwa bado anazungumza, jogoo aliwika. 61 Bwana aligeuka akamtazama Petro kwenye macho yake. Kisha Petro akakumbuka Bwana alivyokuwa amesema ya kwamba, “Kabla ya jogoo kuwika asubuhi, utakuwa umenikana mara tatu.” 62 Kisha Petro akatoka nje na kulia kwa uchungu.

Walinzi Wamdhalilisha Yesu

(Mt 26:67-68; Mk 14:65)

63 Walinzi waliokuwa wanamlinda Yesu walimfanyia mizaha na kumpiga. 64 Wakayafunika macho yake ili asiwaone. Kisha wakampiga na wakasema, “Tabiri, tuambie nani amekupiga!” 65 Walimtukana pia matusi ya kila aina.

Yesu Akiwa Mbele ya Viongozi wa Kidini

(Mt 26:59-66; Mk 14:55-64; Yh 18:19-24)

66 Alfajiri, viongozi wazee wa watu, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikusanyika. Walimpeleka Yesu kwenye baraza lao kuu. 67 Wakamwambia, “Tuambie ikiwa wewe ni Masihi.”

Yesu akawaambia, “Hamtaniamini ikiwa nitawaambia kuwa mimi ni Masihi. 68 Na ikiwa nitawauliza swali, hakika mtakataa kunijibu. 69 Lakini kuanzia sasa, Mwana wa Adamu atakaa upande wa kuume wa Mungu Mwenye Nguvu.”

70 Wote wakasema, “Kwa hiyo wewe ni Mwana wa Mungu?” Akawajibu, “Mnaweza kusema kuwa mimi ni Mwana wa Mungu.”

71 Wakasema, “Je, tunahitaji mashahidi wengine zaidi? Sote tumesikia alichosema yeye mwenyewe!”

Footnotes

  1. 22:7 Siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu Pasaka.
  2. 22:20 Nakala chache za Kiyunani hazina maneno ya Yesu katika sehemu ya mwisho ya mstari wa 19 na mstari wote wa 20.
  3. 22:31 Simoni Jina jingine la Simoni lilikuwa Petro.
  4. 22:42 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao.
  5. 22:44 Nakala zingine za Kiyunani hazina mstari wa 43 na 44.